Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha wa Yanga aanza na Simba


SIMBA inahamisha hesabu zao kimataifa ikitakiwa kuwafuata Mighty Wanderers, lakini wapinzani wao hao kutoka Malawi wamefanya mabadiliko ya benchi la ufundi na kumkabidhi mikoba kocha mmoja wa zamani wa Yanga.


Mabosi wa Mighty Wanderers wamempa ajira ya muda kocha Patrick Mabedi, kusaidiana na kaimu kocha mkuu, MacDonald Nginde Mtetemera kuiongoza timu hiyo huku kibarua chao cha kwanza ni dhidi ya Simba, mchezo utakaopigwa Septemba 6, 2026 kwenye Uwanja wa Bingu nchini humo, ikiwa ni wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali.

Mabedi kama umemsahau ni yule ambaye alitua Yanga siku chache kabla ya mabingwa hao wa Tanzania kuachana na aliyekuwa kocha wao Romain Folz, kisha kuiongoza timu hiyo kuwang’oa Wiliete ya Angola.

Baada ya hapo, Yanga haikumtosa, akasalia na kuwa sehemu ya benchi la ufundi la kocha Pedro Goncalves, kisha hata alipoondolewa Mreno huyo, Mabedi aliendelea kuwa sehemu ya benchi hilo akisaidiana na Abdihamid Moalin ambao waliipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2025-2026, mwisho wa msimu huo akasepa.

Akizungumzia mchezo huo, Mabedi alisema haitakuwa rahisi sana kufanya makubwa katika mchezo huo ambapo kwasasa kitu muhimu ni kujua ubora wa Simba na kutafuta mkakati wa kuwazuia.

“Unaona namna muda ambao upo kuelekea mchezo wenyewe, huwezi kusema utafanya mambo makubwa sana, lakini tunatakiwa kufanya hesabu zetu sahihi kwanza kuwajua wapinzani wetu kwa uhalisia ili tujue namna ya kukabiliana nao,” alisema Mabedi.

“Simba ni timu kubwa lakini kitu muhimu ni sisi kuamua safari yetu kwa kutafuta kitu kizuri hapa nyumbani kabla ya mech ya marudiano.”


ILIVYOBADILISHA BENCHI LA UFUNDI

Mighty Wanderers imemteua MacDonald Nginde Mtetemera kuwa kocha mkuu wa muda, siku moja tu baada ya kumsimamisha kazi kocha wake, Bob Mpinganjira.

Uamuzi huo umefanywa na Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, huku barua iliyosainiwa na Katibu wa Bodi, Chancy Gondwe, ikithibitisha uteuzi wa Mtetemera kufuatia kikao cha viongozi wa klabu.

Mpinganjira alisimamishwa kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika Ligi Kuu ya FDH Bank Premiership, sambamba na kushindwa kutwaa ubingwa wa Airtel Top 8.

Wanderers walipoteza fainali ya Airtel Top 8 kwa mabao 2-1 dhidi ya Ekhaya FC, matokeo ambayo yaliongeza presha kwa benchi la ufundi.

Kipigo hicho kilikuwa pigo kubwa kwa Wanderers kwa kuwa Ekhaya FC ilikuwa ikishiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza na iliingia kwenye fainali ikiwa haikupewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri dhidi ya Wanderers, ambao wana uzoefu mkubwa na rasilimali zaidi katika soka la kiwango cha juu nchini Malawi.

Viongozi wa Wanderers wamekuwa wakikerwa na mwenendo usio na utulivu wa timu hiyo msimu huu, huku matokeo yao katika ligi yakishindwa kufikia matarajio yaliyowekwa mwanzoni mwa msimu.

Awali, klabu hiyo ilithibitisha kumteua Patrick Mabedi, aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Yanga, kama mshauri wa kiufundi wa kusaidia katika mfumo wa benchi la ufundi.

Sasa Mtetemera atafanya kazi pamoja na Mabedi huku Wanderers wakijaribu kurejesha utulivu na kubadili mwenendo wa timu, si katika mashindano ya ndani pekee bali pia katika mechi zao zijazo za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Simba.

Pia haijafafanua iwapo Mtetemera atabaki kwenye nafasi hiyo kwa muda mfupi tu au kama anaweza kupewa nafasi ya kuendelea iwapo atafanikiwa kubadili matokeo ya timu katika wiki zijazo.


TAHADHARI YATOLEWA

Wakati huohuo, taarifa kutoka Malawi zinabainisha kwamba, mchezo huo unakabiliwa na mazingira ya kiusalama yasiyotabirika nchini Malawi baada ya kubainika kuwa Uwanja wa Bingu unaotarajiwa kuandaa mchezo huo una upungufu mkubwa kwenye uzio wake.

Hofu imeibuka baada ya mashabiki kuonekana wakitumia mianya katika uzio wa uwanja huo kuingia bila tiketi wakati wa mchezo wa fainali ya Airtel Top 8 uliochezwa Agosti 30, 2026. Hali hiyo imezua maswali mazito kuhusu usalama wa mchezo huo wa kimataifa, huku idadi kubwa ya mashabiki ikitarajiwa kujitokeza.

Taarifa zinabainisha kuwa, baadhi ya maeneo ya uzio wa Uwanja wa Bingu yana mapengo ambayo yanaweza kuruhusu mashabiki kuingia uwanjani bila kupitia milango rasmi. Tatizo hilo lilidhihirika katika fainali iliyowakutanisha Mighty Wanderers na Ekhaya uliochezwa uwanjani hapo Agosti 31, 2026, ambapo baadhi ya mashabiki walitumia mianya hiyo kukwepa kulipa tiketi.


MKWARA WA WANDERERS

Licha ya kukutana na Simba, moja ya vigogo vya soka Tanzania, Wanderers imeonyesha kujiamini, huku Mkurugenzi wake wa Soka, David Kanyenda, akisisitiza kuwa timu hiyo ina kikosi chenye uwezo wa kushindana na timu bora barani Afrika.

Kanyenda ametaja baadhi ya nyota wa timu hiyo wanaotarajiwa kuwa sehemu ya kikosi, akiwemo wachezaji wa timu ya taifa ya Malawi, Emmanuel Nyirenda, Blessings Singini na Stanley Sanudi.

Akizungumza kuhusu mchezo huo, Kanyenda alisema Wanderers haina sababu ya kuiogopa Simba kwa kuwa wenyewe ni mabingwa wa Malawi.

“Tuna kikosi kizuri sana na hakuna timu yenye kikosi bora kutuzidi Malawi. Lengo letu ni kufika hatua ya makundi. Simba si mabingwa Tanzania (Mabingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB); sisi ni mabingwa hapa. Hatuwaogopi,”  alisema Kanyenda.