Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Messi v Dembele Kombe la Dunia la Klabu ni bonge moja la mechi

Muktasari:

  • Mechi hiyo ya kibabe itafanyika kwenye Uwanja wa Bank of America mjini Charlotte. Timu hizo mbili zimesheheni mastaa wa maana kwenye safu ya ushambuliaji, kitu kinachofanya mashabiki wengi kuamini itakuwa mechi ya mabao mechi.

CHARLOTTE, MAREKANI: BONGE la mechi ndicho unachoweza kusema, wakati mashabiki wakisubiri kipute cha maana cha mabingwa wa Ulaya, Paris Saint-Germain watakapokumbana na miamba ya Marekani, Inter Miami kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora katika fainali za Kombe la Dunia la Klabu usiku wa Jumapili.

Mechi hiyo ya kibabe itafanyika kwenye Uwanja wa Bank of America mjini Charlotte. Timu hizo mbili zimesheheni mastaa wa maana kwenye safu ya ushambuliaji, kitu kinachofanya mashabiki wengi kuamini itakuwa mechi ya mabao mechi.

Kitamu zaidi, supastaa wa Inter Miami, Lionel Messi atakutana na klabu yake ya zamani ya PSG kwa mara ya kwanza tangu alipoachana nayo. Messi ataungana na mtu mwingine anayefahamiana naye vyema, kocha wa PSG, Luis Enrique. Wawili hao walikuwa pamoja Barcelona na kupata mafanikio makubwa, ikiwamo ushindi wa kihistoria wa mabao 6-1 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati ilipopindua meza dhidi ya PSG mwaka 2017, kufuatia Barca kupoteza mechi ya kwanza kwa mabao 4-0 katika hatua ya 16 bora.

Kipute cha usiku wa Jumapili kitashuhudia mastaa wa maana kabisa, ambako kwenye kikosi cha Inter Miami kuna wakali kama Messi, Luis Suarez, Sergio Busquets na Jordi Alba. Miamba hiyo ikivuka hapo itakwenda kumenyana na ama Bayern Munich au Flamengo kwenye raundi inayofuata na wachezaji hao watapata nafasi ya kukutana na mastaa wengine waliowahi kucheza nao, endapo watakipiga huko Atlanta.

Ikitokea kunyakua mataji matatu ndani ya msimu mmoja, ikiwamo Ligue 1, Coupe de France na Ligi ya Mabingwa Ulaya, PSG ipo kwenye kiwango bora kabisa. Miamba hiyo ya Ufaransa itahitaji kunyakua taji la dunia pia, huku kikosi hicho cha kocha Enrique kikiwa na wastani wa kumiliki mpira kwa asilimia 73 katika mechi za makundi, ilhali mabao yake yakifungwa na wachezaji sita tofauti.

Kwenye safu ya ulinzi, PSG imeruhusu bao moja katika mechi tano za mwisho. Imekuwa na beki ngumu, lakini imekuwa na safu matata ya ushambuliaji ikiundwa na Khvicha Kvaratskhelia na Ousmane Dembele na wengine kibao kwa kuwataja tu kwa uchache.

Mechi hiyo ya Inter Miami na PSG ni ya kujuana, ambapo ukiweka kando wachezaji wa kikosi cha miamba hiyo ya Marekani kocha wake ni Javier Mascherano, ambaye ana uzoefu mkubwa wa soka la Ulaya baada ya kutamba kwenye vikosi vya Liverpool na Barcelona.

Ukiweka kando kipute hicho, kasheshe jingine litakuwa huko uwanjani Hard Rock, wakati wakali wa Brazil, Flamengo watakuwa na shughuli pevu kukabiliana na mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich. Flamengo ni moja ya timu za Brazil zinazofanya vizuri kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia la Klabu jambo ambalo linawafanya Bayern, wenye huduma ya straika Harry Kane kukuna kichwa katika kukabiliana nao katika hatua hiyo ya mtoano. Mambo ni moto.