Messi apata pigo kifo cha Baba yake
Muktasari:
- Jorge amefariki siku mbili tu baada ya familia ya Messi kufichua kuwa alikuwa amelazwa hospitalini kutokana na hali ya kiafya iliyokuwa ikiendelea kumsumbua.
BUENOS AIRES, ARGENTINA: JORGE Messi, baba mzazi na mtu aliyekuwa nguzo muhimu katika maisha na safari ya soka ya Lionel Messi, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 68.
Jorge amefariki siku mbili tu baada ya familia ya Messi kufichua kuwa alikuwa amelazwa hospitalini kutokana na hali ya kiafya iliyokuwa ikiendelea kumsumbua.
Taarifa za kifo chake ziliripotiwa kwanza na vyombo vya habari vya Argentina kabla ya kuthibitishwa na baadhi ya klabu ambazo zimewahi kuwa sehemu ya safari ya Lionel Messi, akiwemo klabu yake ya kwanza Newell's Old Boys.
Jorge alifariki katika hospitali iliyopo Rosario, karibu na nyumbani kwa familia hiyo, majira ya saa nne usiku Ijumaa, Agosti 7.
Newell's Old Boys ilikuwa miongoni mwa taasisi za kwanza kutoa salamu za rambirambi, ikieleza kwa masikitiko makubwa kumpoteza Jorge ambaye alitajwa kuwa shabiki mkubwa wa klabu hiyo, mfanyabiashara na baba wa nahodha wa timu ya taifa ya Argentina.
Klabu hiyo ilisema Jorge alikuwa nguzo muhimu katika maisha ya Lionel na mtu aliyekuwa nyuma ya safari yake yote ya soka, akishirikiana kwa karibu na mke wake Celia Cuccittini.
Uongozi wa Newell's Old Boys ulisema Jorge alitoa msaada, ushauri na uongozi kwa Lionel tangu akiwa mtoto hadi kufikia kilele cha soka duniani.
“Uwepo wake wa karibu na uongozi wake nyuma ya pazia ulikuwa muhimu katika kumuunga mkono Lionel katika kila hatua, tangu mwanzo wake hadi kufikia kilele cha utukufu wa soka duniani,” ilisema sehemu ya salamu hizo.
Baada ya taarifa hiyo, Barcelona na Shirikisho la Soka la Argentina pia zilituma salamu za pole kwa familia ya Messi.
Timu ya taifa ya Argentina iliandika kupitia mtandao wa X: “Kuwa na nguvu Leo Messi na familia. Tupo pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu na tunawatuma kumbatio letu la dhati.”
Barcelona nayo ilitoa salamu za rambirambi kwa familia ya Messi huku ikimshukuru Jorge kwa mchango wake katika safari ya Lionel na uhusiano wake na klabu hiyo.
“Barcelona inamshukuru Jorge Messi kwa kujitolea kwake kwa klabu yetu na kwa kutuamini katika hatua za mwanzo na miaka yenye mafanikio makubwa ya soka ya mwanawe Leo,” ilisema Barcelona.
Shirikisho la Soka la Amerika Kusini, CONMEBOL, pia liliungana na familia hiyo katika maombolezo, likisema linamsindikiza Lionel, familia yake, marafiki na wapendwa wake katika kipindi hicho cha huzuni kubwa.
Hadi sasa, chanzo rasmi cha kifo cha Jorge hakijawekwa wazi.
Alikuwa zaidi ya baba
Jorge hakuwa baba wa Lionel Messi pekee, bali alikuwa mmoja wa watu muhimu zaidi katika maisha na kazi ya nyota huyo.
Kwa miaka mingi alikuwa wakala wa Messi na pia msimamizi wa masuala mengi ya kibiashara yaliyomhusu mwanawe, akisimamia kwa karibu masuala ya mikataba, biashara na mali zilizojengwa na Lionel kutokana na mafanikio yake makubwa katika soka.
Uhusiano wa baba na mwana ulikuwa wa karibu sana, huku Jorge akiwa pamoja na Lionel katika hatua mbalimbali za safari yake, kuanzia utotoni Argentina hadi kufikia kuwa mmoja wa wachezaji wakubwa zaidi katika historia ya soka.
Katika miezi ya hivi karibuni, hata hivyo, Jorge alikuwa akikabiliwa na matatizo ya kiafya ambayo hayakuwa yamewekwa wazi kwa umma.
Hali hiyo ilianza kuzungumzwa zaidi baada ya Lionel kuonekana akilia katika Kombe la Dunia, jambo ambalo lilikuwa nadra sana kwa nyota huyo kuonyesha hadharani hisia zake.
Baada ya kufunga hat-trick katika mchezo wa kwanza wa Argentina dhidi ya Algeria, Messi aliulizwa na waandishi wa habari kuhusu hali yake ya kihisia.
“Hapana, kwa kweli hili halihusiani kabisa na michezo. Imekuwa siku chache ngumu na zenye changamoto,” amesema Messi.
Baadaye, mwandishi wa habari Eduardo Feinmann alidai kuwa hali hiyo ilihusiana na afya ya Jorge.
“Ni kuhusu baba yake. Baba yake hana afya njema. Hali hii imekuwepo kwa muda, kwa miezi kadhaa, tangu mwaka jana,” amesema Feinmann kupitia Radio Mitre.
Amesema hali ya Jorge ilikuwa imezidi kuwa mbaya katika kipindi hicho na kwamba Lionel alikuwa akipitia wakati mgumu kihisia kama binadamu mwingine yeyote.
Taarifa zilizofuata zilieleza kuwa Jorge aliwahi kupata tatizo la kiafya nyumbani kwake Januari mwaka huu na kulazwa hospitalini.
Sasa, baada ya kifo chake, Lionel Messi amepoteza mtu ambaye alikuwa si tu baba yake, bali pia mshauri, wakala na mshirika wake mkuu katika safari yake ya kuwa mmoja wa wanasoka waliotengeneza historia.
Jorge ameacha Lionel, Rodrigo, Matias na Maria Sol pamoja na mke wake Celia na familia nyingine katika kipindi cha maombolezo.
Kwa Messi, huu ni msiba mkubwa wa kifamilia katika maisha yake, huku dunia ya soka ikiungana naye kumpa pole baada ya kumpoteza mtu aliyekuwa sehemu muhimu ya mafanikio yake tangu akiwa mtoto.