Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Petit amkata Kane mbio za Ballon d'Or 2026

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Petit, tatizo la Kane siyo idadi ya mabao aliyofunga, bali ni kushindwa kuwa na ushawishi katika mechi kubwa na za uamuzi.

PARIS, UFARANSA: NGULI wa zamani wa soka wa Ufaransa, Emmanuel Petit, anaamini kuwa mshambuliaji wa Bayern Munich na timu ya taifa ya England, Harry Kane, hana tena nafasi ya kutwaa tuzo ya Ballon d'Or 2026, licha ya kuwa na msimu wa kipekee wa kufunga mabao.

Kwa mujibu wa Petit, tatizo la Kane siyo idadi ya mabao aliyofunga, bali ni kushindwa kuwa na ushawishi katika mechi kubwa na za uamuzi.

Kane alikuwa na msimu bora katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo alifunga mabao 14 katika mechi 13 akiwa na Bayern Munich. Hata timu yake ilipotolewa na PSG kwa jumla ya mabao 6-5 katika hatua ya nusu fainali, nyota huyo alikuwa amefunga mabao mawili na kutoa asisti moja.

Katika Kombe la Dunia 2026, nahodha huyo wa England alimaliza akiwa na mabao sita na asisti moja katika mechi saba. Hata hivyo, hakufunga wala kutoa asisti katika ushindi wa robo fainali dhidi ya Norway, wala katika mchezo wa nusu fainali ambao England ilipoteza dhidi ya Argentina.

Petit, ambaye alitwaa Kombe la Dunia na Ufaransa 1998, alisema: "Nafasi za Harry Kane kushinda Ballon d'Or zimekwisha. Kama ungeangalia Bundesliga pekee, basi asingekuwa na tatizo. Lakini katika Ligi ya Mabingwa na akiwa na timu ya taifa wakati ilipohitaji kushinda mechi ngumu zaidi, nafikiri alipotea."

Aliendelea kusema: "Siwezi kumnyooshea kidole kwa sababu alijitahidi na alifunga mabao mengi. Lakini hakuwa na athari katika mechi kubwa, kama ilivyokuwa pia kwenye Ligi ya Mabingwa. Kwa hiyo naamini kuna wachezaji kadhaa walio mbele yake."

Licha ya ukosoaji huo, Kane alikuwa na msimu wa kuvutia binafsi ambapo alifunga mabao 61 katika mechi 51 alizoichezea Bayern Munich na timu ya taifa ya England. Hata hivyo, Petit anaamini kuwa katika mbio za Ballon d'Or, kiwango cha mchezaji katika mechi za uamuzi na mafanikio ya timu huwa na uzito mkubwa kuliko takwimu za mabao pekee.

Petit aliwataja Lamine Yamal, Rodri na Lionel Messi kuwa miongoni mwa wachezaji wenye hoja imara zaidi ya kushinda Ballon d'Or kutokana na viwango walivyoonyesha katika klabu zao na Kombe la Dunia.

Akiwazungumzia mastaa hao, alisema: "Yamal alikuwa na Kombe la Dunia bora sana. Unajua sheria za Ballon d'Or zimebadilika sana, kama zilivyobadilika sheria za mchezo. Rodri amekuwa tena mchezaji bora katika mashindano haya. Messi pia alikuwa na mashindano mazuri, ingawa anacheza Inter Miami."

Hata hivyo, Petit hakumtaja mchezaji mmoja anayemuona ndiye mwenye nafasi kubwa zaidi ya kushinda tuzo hiyo. Hata hivyo alihitimisha kwa kusema anatarajia mshindi wa Ballon d'Or achaguliwe kwa kuzingatia soka aliloonyesha uwanjani, badala ya umaarufu au maslahi ya kibiashara.

"Najua Kombe la Dunia lina uzito kuliko taji lolote la klabu. Lakini bado unahitaji kushinda mataji. Sijui kama atakuwa mchezaji wa Hispania au la, lakini ushindani utakuwa mkubwa. Mwishowe, natumaini hautakuwa uamuzi wa kibiashara."

Kauli ya Petit imeongeza mjadala kuhusu nani anastahili kutwaa Ballon d'Or 2026. Ingawa Harry Kane ana rekodi ya kuvutia ya mabao, gwiji huyo wa Ufaransa anaamini kuwa kushindwa kung'ara katika mechi muhimu kumepunguza kwa kiasi kikubwa nafasi yake ya kutwaa tuzo hiyo ya heshima kubwa zaidi kwa mchezaji binafsi duniani.