Messi afikisha mabao 922, asogelea rekodi ya 1,000
Muktasari:
- Messi alifikia idadi hiyo baada ya kufunga bao katika dakika ya 26 kwa mguu wake wa kushoto, wakati Inter Miami ikitoka sare ya 2-2 dhidi ya Philadelphia Union katika mchezo wa Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
MIAMI, MAREKANI; Lionel Messi ameendelea kuweka historia katika soka baada ya kufikisha rasmi mabao 922 katika maisha yake soka la kulipwa.
Messi alifikia idadi hiyo baada ya kufunga bao katika dakika ya 26 kwa mguu wake wa kushoto, wakati Inter Miami ikitoka sare ya 2-2 dhidi ya Philadelphia Union katika mchezo wa Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
Bao hilo lilikuwa na uzito wa kipekee kwa Messi, kwa kuwa lilikuwa bao lake la kwanza tangu kufariki kwa baba yake mzazi, Jorge Messi, mapema mwezi huu.
Baada ya kufunga, Messi alisherehekea kwa kunyoosha mikono yake kuelekea angani, ishara iliyotafsiriwa kama kumbukumbu na heshima kwa baba yake.
MABAO 922 YA MESSI YAMEGAWANYIKAJE?
Katika jumla ya mabao yake 922, Messi amefunga katika klabu na timu ya taifa kama ifuatavyo
Barcelona: Mabao 672
Argentina: Mabao 125
Inter Miami: Mabao 93
Paris Saint-Germain (PSG): Mabao 32
Kwa kufikisha mabao 922, Messi sasa amebakiza mabao 78 pekee ili kufikisha hatua kubwa ya mabao 1,000 katika soka la kulipwa.
Mbali na rekodi hiyo ya mabao, Messi pia anaendelea kushikilia rekodi ya kuwa miongoni mwa wachezaji wenye idadi kubwa zaidi ya pasi za mabao (asisiti) katika historia ya soka, akiwa na takribani 420.
Hatua hiyo inaendelea kuongeza mvuto katika mjadala wa rekodi za muda wote, huku Messi akiendelea kusaka historia nyingine kubwa kabla ya kufikisha idadi ya mabao 1,000.