Mbappe kaweka shilingi yake kwa Morocco
Muktasari:
- Staa huyo ametumia siku zake za mapumziko huko Real Madrid kwenda Morocco kutazama mechi kadhaa za Afcon 2025 inayoendelea kwa sasa na kuamini Simba wa Atlas, ambayo nahodha wake ni Hakimi ndiyo watakaobeba ubingwa.
RABAT, MOROCCO: SUPASTAA wa soka, Kylian Mbappe anaamini chama analochezea swahiba wake, Achraf Hakimi ambako ni Morocco ndilo litakalonyakua ubingwa wa AFCON.
Staa huyo ametumia siku zake za mapumziko huko Real Madrid kwenda Morocco kutazama mechi kadhaa za Afcon 2025 inayoendelea kwa sasa na kuamini Simba wa Atlas, ambayo nahodha wake ni Hakimi ndiyo watakaobeba ubingwa.
Mfaransa huyo alikuwa gumzo Ijumaa alipotokea jukwaani kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah huko Rabat akiwa amevaa jezi ya Morocco yenye jina la Hakimi mgongoni kushuhudia mechi ya pili ya Kundi A, ambapo Simba wa Atlas ilitoka 1-1 na Mali.
Mbappe alisafiri hadi Morocco kwenda kumpa sapoti mchezaji mwenzake wa zamani wa PSSG, Hakimi, ambaye hata hivyo kwenye mechi hiyo aliishia kukaa benchini.
Jumapili. Mbappe alikuwa Marrakech kutazama mechi ya Cameroon, nchi anayotokea baba yake, ambayo iliwa kwenye kibarua cha kukabiliana na mabingwa watetezi, Ivory Coast na kutoka sare ya bao 1-1.
Baada ya kuhudhuria mechi hizo mbili, staa huyo wa Real Madrid alipata picha ya ubingwa wa Afcon 2025 na kutoa utabiri wake, huku Hakimi akisema: “Nimefurahi kwanza kumwona rafiki yangu kwenye nchi yangu. Anaipenda Morocco. Amekuja na familia yake, amefurahia kuwa hapa.”