Mbappe amkaribisha Zidane kwa ujumbe mzito
Muktasari:
- Uteuzi wa Zidane umepokelewa kwa shangwe kubwa, lakini aliyeonyesha hisia zaidi ni nahodha wa Ufaransa, Kylian Mbappe, ambaye hakusubiri muda mrefu kumkaribisha kocha huyo kupitia mitandao ya kijamii.
PARIS, UFARANSA: ENZI mpya zimeanza ndani ya timu ya taifa ya Ufaransa baada ya Shirikisho la Soka la nchi hiyo (FFF) kumtangaza rasmi nguli Zinedine Zidane kuwa kocha mkuu wa Les Bleus, akichukua nafasi ya Didier Deschamps aliyefunga pazia la miaka 14 ya mafanikio.
Uteuzi wa Zidane umepokelewa kwa shangwe kubwa, lakini aliyeonyesha hisia zaidi ni nahodha wa Ufaransa, Kylian Mbappe, ambaye hakusubiri muda mrefu kumkaribisha kocha huyo kupitia mitandao ya kijamii.
Mshambuliaji huyo wa Real Madrid aliweka picha ya Zidane kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuandika maneno mawili tu yaliyozungumzwa sana na mashabiki wa soka duniani: "Bienvenue chez toi" yaani, "Karibu nyumbani."
Ujumbe huo umeonyesha heshima kubwa ambayo Mbappe amekuwa nayo kwa Zidane, ambaye kwa miaka mingi amekuwa mmoja wa watu anaowatazama kama mfano katika soka la Ufaransa. Sasa kwa mara ya kwanza, wawili hao wataunganishwa ndani ya timu ya taifa, mmoja akiwa kocha na mwingine nahodha.
Zidane anarithi kikosi chenye vipaji vingi kinachoongozwa na Mbappe, huku jukumu lake kubwa likiwa kuirejesha Ufaransa kileleni mwa soka la dunia kwa kulisaka taji la Euro 2028 na Kombe la Dunia 2030.
Nguli huyo wa miaka 54 si mgeni kwa Les Bleus. Ndiye shujaa aliyeiongoza Ufaransa kutwaa Kombe la Dunia la mwaka 1998 akiwa mchezaji, mafanikio yaliyomweka kwenye orodha ya magwiji wakubwa zaidi katika historia ya nchi hiyo.
Anachukua nafasi ya Deschamps, ambaye ameiacha timu ikiwa na rekodi ya kuvutia baada ya kuiongoza tangu mwaka 2012. Katika kipindi chake, aliipa Ufaransa ubingwa wa Kombe la Dunia 2018, taji la UEFA Nations League mwaka 2021, huku pia akifika fainali za Euro 2016 na Kombe la Dunia 2022.
Kwa Zidane, huu ni mwanzo wa safari mpya baada ya kukaa nje ya ukocha kwa miaka mitano tangu aondoke Real Madrid mwaka 2021.
Akiwa Santiago Bernabeu aliweka rekodi ya kipekee kwa kuiongoza Real Madrid kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, pamoja na mataji mawili ya LaLiga, mafanikio yaliyomfanya kuwa mmoja wa makocha wenye heshima kubwa duniani.
Sasa macho ya Wafaransa yataelekezwa kwa Zidane kuona kama ataweza kuhamishia mafanikio yake ya ngazi ya klabu kwenye timu ya taifa, huku ushirikiano wake na Mbappe ukitajwa kuwa silaha muhimu katika ndoto za Les Bleus kurejea kileleni mwa soka la dunia.