Biashara ya Vinicius Jr inavyozua utata wa usajili
Muktasari:
- Real Madrid kwa sasa inanufaika kwa kiwango kikubwa kutokana na mikataba mingi ya udhamini aliyonayo nyota huyo wa Brazil, ambaye katika misimu ya karibuni amejidhihirisha kuwa moja ya sura zinazouza zaidi katika soka la dunia.
MADRID, HISPANIA: WINGA wa Real Madrid, Vinicius Junior, ameendelea kujijengea hadhi kubwa si tu ndani ya uwanja wa soka, bali pia kwenye ulimwengu wa biashara, huku akiwa miongoni mwa wachezaji wenye mvuto mkubwa zaidi kwa kampuni mbalimbali duniani jambo ambalo ni hofu kubwa kwa dili lake la kwenda Arsenal.
Real Madrid kwa sasa inanufaika kwa kiwango kikubwa kutokana na mikataba mingi ya udhamini aliyonayo nyota huyo wa Brazil, ambaye katika misimu ya karibuni amejidhihirisha kuwa moja ya sura zinazouza zaidi katika soka la dunia.
Hali hiyo inakuja wakati taarifa za Daily Mail Sport zikieleza kuwa Arsenal imeanza kuchunguza uwezekano wa kufanya usajili wa kushtukiza wa Vinicius katika dirisha hili la usajili iwapo atashindwa kufikia makubaliano ya kuongeza mkataba mpya na Real Madrid.
Kwa sasa Vinicius ana mkataba unaotarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu wa 2027-28, lakini Jumatatu hakuripoti mazoezini kabla ya msimu mpya kuanza, huku wawakilishi wake wakiendelea na mazungumzo muhimu na viongozi wa Real Madrid kuhusu mkataba mpya.
Ingawa Real Madrid haionekani kuwa tayari kumpa mshahara unaolingana na ule wa nyota mwenzake Kylian Mbappe, viongozi wa klabu hiyo wana kila sababu ya kupambana kumbakiza kutokana na hadhi yake ya kimataifa na uwezo wake mkubwa wa kuzalisha mapato kupitia haki za kibiashara.
Vinicius kwa sasa ana ushirikiano wa kibiashara na makampuni 16 tofauti, jambo linalomfanya kuwa mmoja wa wachezaji wenye thamani kubwa zaidi nje ya uwanja wa soka.
Miongoni mwa wachezaji walioshiriki Kombe la Dunia la majira ya kiangazi yaliyopita, Vinicius alikuwa wa pili kwa kuwa na mikataba mingi ya udhamini, akitanguliwa na Neymar pekee ambaye ana mikataba 20 ya kibiashara.
Machapisho anayoweka kwenye mitandao yake ya kijamii kutangaza bidhaa na huduma za kampuni hizo yamekusanya zaidi ya watazamaji milioni 100 tangu alipoteuliwa kwenye kikosi cha Brazil cha Kombe la Dunia, jambo linaloonyesha ukubwa wa ushawishi wake akiwa sura muhimu ya Brazil na Real Madrid.
Tangu aliposajiliwa Real Madrid mwaka 2018, Vinicius amesaini mikataba yenye thamani kubwa na kampuni maarufu duniani zikiwemo Gatorade, Pepsi, Prada, PlayStation, UNESCO, Visa na Nike.
Mbali na hizo, pia anadhaminiwa na Boss, Clear, Omo, Rexona, Betnacional, Dubai Tourism, Havaianas, Vivo pamoja na Marriott Bonvoy, na kufanya jumla ya washirika wake wa kibiashara kufikia kampuni 16.
Kwa mujibu wa gazeti la Hispania la AS, wakati Vinicius alipoongeza mkataba wake mwaka 2022 ambao unamalizika kiangazi cha mwaka 2027, alikubali kuipa Real Madrid takribani asilimia 50 ya haki za matumizi ya picha na taswira yake.
Makubaliano hayo yanamaanisha kuwa kila fedha anazopata kupitia shughuli zake za kibiashara hugawanywa nusu kwa nusu kati yake na Real Madrid, hali inayomfanya kuwa moja ya migodi mikubwa ya mapato katika soka la dunia.
Gazeti hilo la Hispania lilieleza kwa utani kwamba, kutokana na mfumo huo, Vinicius ni kama anajilipa mwenyewe mshahara wake akiwa Real Madrid, angalau hadi pale makubaliano mapya yatakapofikiwa kati yake na klabu hiyo.
Nguvu hiyo ya kibiashara inaweza pia kuwa moja ya changamoto katika mazungumzo ya kuongeza mkataba, huku taarifa za kuvutiwa na Arsenal zikimpa nyota huyo nguvu zaidi mezani wakati wa majadiliano.
Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Roc Nation Sports Brazil, Frederico Pena, inayomsimamia Vinicius, amesema mchezaji huyo sasa amefikia kiwango ambacho hakutazamwi tena kama mwanasoka pekee bali kama biashara kamili.
"Japokuwa bado ni kijana, Vinicius tayari ni mchezaji muhimu katika klabu kubwa zaidi duniani na pia katika timu ya taifa ya Brazil.
"Amekuwa bingwa na nyota katika kampeni mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku akiwa mfano wa uvumilivu, mafanikio ya michezo na msukumo kwa mamilioni ya Wabrazil.
"Mbali na hilo, haogopi kusimamia masuala muhimu ya kijamii, iwe kupitia misimamo yake au mchango wake kwa jamii. Hilo ndilo linalofanya idadi ya kampuni zinazotaka kushirikiana naye kuendelea kuongezeka."
Pena ameongeza kuwa biashara ya Vinicius sasa inaendeshwa kama kampuni kubwa yenye idara mbalimbali.
"Kuna muundo kamili wenye Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), Ofisa Mkuu wa Fedha (CFO), pamoja na idara za utawala, sheria, biashara, masoko na mawasiliano ambazo zinasimamia kila kitu.
"Kuna miradi mingi inayohusisha wadhamini wake mbalimbali, sambamba na shughuli za kijamii kupitia taasisi yake ambayo sasa ni kinara duniani katika mbinu bunifu za kufundisha watoto na vijana, pamoja na mafunzo kwa walimu kuhusu mbinu za elimu zinazopinga ubaguzi wa rangi."
Ingawa uwezo wake mkubwa uwanjani unaendelea kuisogeza Real Madrid karibu na mataji na mafanikio, ukweli ni kwamba thamani halisi ya Vinicius Junior kwa sasa haipo ndani ya dakika 90 pekee, bali pia katika himaya kubwa ya biashara aliyojenga nje ya uwanja