Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Cedric Kaze kazi ipo Kagera Sugar

KAZE Pict

Muktasari:

  • Kocha huyo raia wa Burundi, amekabidhiwa Kagera baada ya Juma Kaseja kusitishiwa mkataba wake kutokana na mechi sita za mwanzo za Ligi Kuu Bara msimu huu kucheza bila ushindi. Kagera imevuna pointi mbili pekee, sare mbili na vipigo vinne, ikikaa nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi.

KOCHA Cedric Kaze ametua Kagera Sugar akiwa amebeba kazi nzito kuliko kutafuta ushindi wa mechi. Ameingia kwenye timu inayohitaji kubadilisha mwelekeo haraka huku ikiwa na changamoto kadhaa za majeruhi, wachezaji ambao bado hawajapata vibali vya kucheza na kumbukumbu ya mwanzo mbaya wa msimu.

Kocha huyo raia wa Burundi, amekabidhiwa Kagera baada ya Juma Kaseja kusitishiwa mkataba wake kutokana na mechi sita za mwanzo za Ligi Kuu Bara msimu huu kucheza bila ushindi. Kagera imevuna pointi mbili pekee, sare mbili na vipigo vinne, ikikaa nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi.

Kaze sasa anaingia katika mazingira ambayo muda wa kufanya majaribio ni mdogo. Kagera inahitaji pointi, lakini wakati huo huo kocha huyo anapaswa kuijenga timu upya, kuitengeneza kiufundi na kurejesha kujiamini kwa wachezaji ambao tayari wameanza msimu kwa presha kubwa.


KAZ 06

MAJERUHI

Changamoto ya kwanza anayokutana nayo Kaze ni hali ya kikosi. Kagera ina wachezaji sita waliokumbwa na majeraha, huku mshambuliaji Kassim Fekha akiwa amefanyiwa upasuaji wa goti na anatarajiwa kukaa nje kwa miezi saba hadi tisa.

Kiungo Freddy Tangalo naye anatarajiwa kukaa nje zaidi ya miezi miwili baada ya kuvunjika mfupa wa paja, wakati Deus Malilo akiendelea kuuguza goti. Said Kipao, Abdul Mohamed na Ally Salum nao wamekuwa wakisumbuliwa na majeraha ya vifundo vya miguu, ingawa wanatarajiwa kurejea baada ya mapumziko ya kalenda ya FIFA.

Hii ina maana Kaze hajapokea kikosi kamili na kuanza kazi akiwa na uhuru wa kuchagua wachezaji anaowataka. Badala yake, atalazimika kufanya kazi na kile alichonacho, huku akisubiri baadhi ya majeruhi kurejea.


KAZ 05

ISHU YA VIBALI

Wakati ishu ya majeraha ikiwa inaikabili Kagera Sugar, kuna suala lingine la wachezaji wa kimataifa.

Kagera imekuwa ikisubiri vibali vya wachezaji watatu ambao hadi sasa hawajaonekana uwanjani. Wachezaji hao ni beki Boniface Onyango, kiungo mshambuliaji Emmanuel Mvuyekule na mshambuliaji Collins Maina.

Hivyo Kaze atalazimika kupanga timu wakati baadhi ya silaha alizotarajiwa kuzitumia bado hazijawa sehemu ya ushindani.


KAZ 01

LIGI HAINA SUBIRA

Changamoto nyingine ni ushindani wa Ligi Kuu Bara yenyewe. Kagera haijapewa muda wa kujenga kikosi taratibu. Baada ya mechi sita, tayari imepoteza nne na imekuwa miongoni mwa timu zinazopambana katika eneo la chini la msimamo.

Zaidi ya hilo, baadhi ya vipigo vimekuwa vizito.

Kipigo cha 6-2 dhidi ya Geita Gold ni ishara ya tatizo ambalo Kaze atalazimika kulifanyia kazi hasa kwenye ulinzi, huku timu ikiwa imeshindwa kupata ushindi katika michezo yake yote sita ya mwanzo.


KAZ 04

REKODI INAMPA KAZI

Kaze anaingia Kagera akiwa na uzoefu wa soka la Tanzania, lakini rekodi yake katika mazingira ya timu ndogo pia ni sehemu ya jambo litakaloangaliwa.

Ameshafanya kazi Yanga na Namungo, lakini mazingira aliyokutana nayo katika timu hizo yalikuwa tofauti. Yanga alikuwa katika klabu yenye matarajio makubwa na wachezaji wengi wenye uwezo, huku Namungo ikiwa katika mazingira ya kupambana na timu zenye bajeti na kina tofauti vya vikosi.

Kwa Kagera, sasa anahitaji kuonyesha uwezo wa kujenga matokeo akiwa na kikosi kinachopambana kujinasua chini ya msimamo.


KAZ 03

MATOKEO

Kagera ipo nafasi ya 15 ikiwa na pointi mbili baada ya mechi sita, ikiwa imetoka sare mbili na kupoteza nne. Katika mechi hizo, ilianza kwa kufungwa 2-0 na Simba, ikatoka sare ya 1-1 na Singida Black Stars, ikachapwa 6-2 na Geita Gold, ikapoteza 2-1 dhidi ya Mashujaa, ikafungwa 2-0 na Azam kabla ya kutoka sare ya 1-1 na Fountain Gate.


KAZ 02

MSIKIE KAZE

Akizungumza na Mwanaspoti Kaze hakutaka kuzungumza mengi, alichoweka wazi ni lengo lake ni kuiondoa timu kwenye nafasi za chini na kuipandisha juu ya msimamo.

Kocha huyo alisema: “Siwezi kuzungumza mengi lakini nachoweza kuahidi kwa wadau na mashabiki wa Kagera Sugar ni kuona timu inaondoka nafasi za chini na kupanda juu.

"Ninaamini kama tukishirikiana sote, kuanzia uongozi wa timu, benchi la ufundi hadi wachezaji na tukipata sapoti ya mashabiki wetu tunaweza kufanya vitu vizuri na kuwafurahisha."