Mbappé aumia goti, kuikosa mechi ya Ubelgiji
Muktasari:
- Huo utakuwa ni mwendelezo wa Mbappe kukosa mechi kutokana na majeraha, kwani hata msimu uliopita alitumia miezi miwili akijiuguza kutokana na jeraha la mguu na siku chache kabla ya fainali za Kombe la Dunia 2026 aliumia pia na kukosa mechi kibao.
ISTANBUL, UTURUKI: TIMU ya taifa ya Ufaransa itamkosa straika Kylian Mbappe aliyetoka uwanjani akichechemea baada ya kuonekana kupata jeraha la goti, muda mfupi baada ya kuifungia bao la ushindi dhidi ya Uturuki katika Ligi ya Mataifa ya Ulaya.
Huo utakuwa ni mwendelezo wa Mbappe kukosa mechi kutokana na majeraha, kwani hata msimu uliopita alitumia miezi miwili akijiuguza kutokana na jeraha la mguu na siku chache kabla ya fainali za Kombe la Dunia 2026 aliumia pia na kukosa mechi kibao.
Mshambuliaji huyo wa Real Madrid alifunga kwa shuti la chini chini katika dakika ya 55 baada ya kupewa pasi na Michael Olise, na muda mfupi baada ya kufikisha bao lake la 67 kwa Ufaransa na kuvunja rekodi, alikaa chini na kukunja uso kwa maumivu huku akisugua eneo linalozunguka goti lake la kushoto.
Jeraha hilo litamfanya nyota huyo kukosa mchezo ujao wa mashindano hayo dhidi ya Ubelgiji ugenini kesho, Jumatatu, ambapo litakuwa pengo kwa Ufaransa kukosa huduma ya mtu ambaye amekuwa na uwiano mzuri wa muda na kufunga.
Baada ya kuumia kocha mpya wa Ufaransa, Zinedine Zidane alimpumzisha na kumuingiza Desire Doue, inagwa katika hali iliyotia moyo Mbappe alitoka mwenyewe uwanjani bila kusaidiwa na baadaye ilielezwa kwamba nahodha huyo atarejea Real Madrid kwa ajili ya matibabu.
“Siyo jambo zuri. Kwa bahati mbaya nadhani atalazimika kurudi nyumbani. Hatutaki kumbakisha ili kuongeza balaa zaidio, ” Zidane alikiambia kituo cha televisheni cha Ufaransa, TF1.
“Alinyosha goti lake kupita kiasi wakati akipiga shuti. Hali hiyo inaumiza moyo sana.”