Mastaa wanaokimbiza NBA
Muktasari:
- Hata hivyo, moja kati ya mambo yanayoibuka kila wakati ligi hii inaposimama ni msimamo wa mchezaji bora wa msimu.
NEW YORK, MAREKANI: LIGI Kuu NBA kwa sasa imesimama kupisha michezo ya NBA Emirate Cup, ambayo imeanza kuchezwa tangu Novemba 13.
Hata hivyo, moja kati ya mambo yanayoibuka kila wakati ligi hii inaposimama ni msimamo wa mchezaji bora wa msimu.
Tovuti ya NBA News imeweka orodha ya wachezaji ambao kwa sasa wanaonekana wanaweza kuchukua tuzo hiyo kwa kuzingatia takwimu zao na vitu walivyofanya tangu kuanza kwa ligi msimu huu ambayo ndiyo kwanza imechezwa kwa mwezi mmoja.
5.Nikola Jokic - Denver Nuggets
Si tu amekuwa chanzo cha ushindi kwa Nuggets katika miaka sita iliyopita, pia ni mchezaji ambaye ni ngumu sana kukosekana uwanjani.
Ndiye anayeshikilia tuzo ya kuwa mchezaji mwenye thamani zaidi (MVP) aliyoipata msimu uliopita na bado anapewa nafasi kubwa ya kufanya hivyo msimu huu.
Jokic ambaye jana aliisaidia Nuggets kushinda mchezo wao dhidi ya Dallas Mavericks kwa kufunga pointi 33, amekuwa na wastani mzuri kwa kila mechi anayocheza na hutupia zaidi ya pointi 25 na kuendelea.
4. Jayson Tatum - Boston Celtics
Wiki iliyopita alikosa tu ribaundi moja kufikisha triple-double, alipoisaidia Celtic kushinda dhidi ya Cavaliers ambayo haikuwa imepoteza mechi tangu kuanza kwa ligi msimu huu.
Tatum ni mmoja wa wachezaji bora msimu huu ambao wameifanya Celtic kushangaza watu wengi kutokana na kiwango ilichoonyesha.
Staa huyu amewaka sana na ana takwimu bora zaidi msimu huu ambazo hakuwahi kuwa nazo katika maisha yake ya NBA kuanzia katika pointi alizo nazo, ribaundi, asisti na kupokonya mipira.
3.Anthony Davis - Los Angeles Lakers
Alifunga pointi 40 dhidi ya Spurs, kisha akapiga pointi 31 dhidi ya Pelicias kabla ya kutupia pointi 26 mbele ya Utah Jaz.
Moja kati ya mambo yanayomfanya staa huyu kuwa katika nafasi hii ni kucheza katika mechi zilizopita akiwa na maumivu na kwa mujibu wa tovuti ya NBA News siku chache zilizopita amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya unyayo.
Pia staa huyu alikuwa msaada mkubwa kwa Lakers mwanzoni mwa msimu wakati LeBron James na Dalton Knecht hawajaanza kufunguka.
2. Giannis Antetokounmpo - Milwaukee Bucks
Licha ya timu yake kutofanya vizuri msimu huu, Antetokounmpo ameendelea kuwa mmoja wa mastaa wanaofanya vizuri katika ligi ya NBA msimu huu.
Staa huyu ana rekodi ya kufunga pointi 30 kila mechi na ufanisi wa asilimia 60 kwenye mitupo yake. Pia anashikilia nafasi ya tano katika mastaa wenye ribaundi nyingi zidi msimu huu.
Anaongoza pia kufunga pointi nyingi katika kipindi robo ya mchezo.
Antetokounmpo pia anasifika kwa kulinda na kusumbua mabeki wa timu pinzani jambo linalowapa nafasi wenzake kufunga pointi.
1.Shai Gilgeous-Alexander - Oklahoma City Thunder
Amecheza vizuri wiki iliyopita licha ya Thunder kupoteza dhidi ya Spurs na Mavericks na alifunga jumla ya pointi 68 na asisti 15 katika michezo hiyo.
Licha ya kufanya vibata wiki iliyoppita, Thunder imeendelea kuwa ya pili katika msimamo wa Ukanda wa Mashariki.