Mastaa hawa Man United wanauzwa
Muktasari:
- Man United inashindwa kupiga hatua kubwa tangu ilipochukuliwa na bilionea Sir Jim Ratcliffe, ambaye amenunua hisa chache mwaka jana na kushughulikia masuala ya kisoka kwenye timu hiyo ya Old Trafford.
MANCHESTER, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Manchester United imeripotiwa sasa imefungua milango ya kupokea ofa zote za kumhusu mchezaji yeyote kwenye kikosi chao – ikiwamo wale watatu ambao awali walitajwa kwamba hawaguswi katika kipindi cha kocha Erik ten Hag.
Man United inashindwa kupiga hatua kubwa tangu ilipochukuliwa na bilionea Sir Jim Ratcliffe, ambaye amenunua hisa chache mwaka jana na kushughulikia masuala ya kisoka kwenye timu hiyo ya Old Trafford.
Man United ilimaliza msimu vibaya ikiwa chini ya kocha Ten Hag, lakini kocha huyo Mdachi alipewa Pauni 200 milioni za kufanya usajili wa mastaa wapya kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi. Na sasa timu hiyo ipo chini ya kocha Ruben Amorim na bado mambo si matamu sana.
Wachezaji wengi kwenye kikosi hicho hawafiti vyema kwenye mfumo mpya wa kiuchezaji wa 3-4-3. Na ripoti zinafichua, tajiri Ratcliffe yupo tayari kumpa sapoti kocha mpya ili kusajili na kuwaweka sokoni mchezaji yeyote kwenye kikosi hicho.
Wakati Man United ikiwa haina mpango wa kuachana bure na wachezaji wake, lakini imefungua milango ya kupokea ofa ya kila mchezaji. Hiyo ina maana inawahusu pia wachezaji Amad Diallo na Bruno Fernandes wote wapo sokoni na watapigwa bei endapo kama kutakuwa na ofa nzuri mezani.
Wakati huo mastaa wapya waliosajiliwa mwaka jana akiwamo Leny Yoro, Matthijs de Ligt na Manuel Ugarte nao wapo sokoni licha ya kuwa na miezi sita tu kwenye klabu hiyo, hata wale mastaa watatu waliodaiwa kwamba hawaguswi katika kipindi cha Ten Hag ambao ni Rasmus Hojlund, Alejandro Garnacho na Kobbie Mainoo, ambao pia Man United haitasimama njiani kuwazuia kama kutakuwa ofa nzuri.
Kinachoelezwa ni kwamba Mainoo kwa sasa yupo kwenye rada za Chelsea, ambao pia wapo tayari kumchukua jumla winga Jadon Sancho kwa ada ya Pauni 20 milioni kwenye dirisha la mwisho wa msimu huu baada ya sasa kuwa kwenye kikosi hicho cha Stamford Bridge kwa mkopo.
Man United inakabiliwa na ishu ya mapato ya matumizi baada ya kutumia pesa nyingi kwenye usajili kwa miaka kadhaa. Kutokana na hilo, itahitaji kuwafungulia mlango wa kutokea baadhi ya mastaa wake wenye majina makubwa ili kumruhusu kocha mpya Amorim kusajili wachezaji watakaoingia kwenye mfumo na mbinu zake za kiuchezaji. Kuuzwa kwa Mainoo, Garnacho na Rashford, ambao waliibukia kwenye akademia ya klabu hiyo kutaipa Man United faida ya asilimia 100.
Fowadi Rashford ni mmoja wa wachezaji wanaotazamiwa kwamba wanaweza kuondoka kwenye timu hiyo Januari hii.
AC Milan na Borussia Dortmund zimeonyesha dhamira ya kunasa saini ya Rashford, huku Joshua Zirkzee akiwa kwenye rada za Juventus, wakati kiungo Casemiro akiendelea kufuatiliwa na klabu za Saudi Arabia.