Mashabiki Man United walalamikia tiketi

Muktasari:
- Timu hiyo imeanzisha mfumo mpya wa kupanga tiketi kulingana na aina ya mechi na baadhi ya wanachama watalazimika kulipa hadi Pauni 97 kwa mechi kubwa, kuanzia mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal Agosti, 17.
MANCHESTER, ENGLAND: MASHABIKI wa Manchester United wamelaani ongezeko jipya la bei za tiketi, wakilielezea ni pigo lingine kali kwao.
Timu hiyo imeanzisha mfumo mpya wa kupanga tiketi kulingana na aina ya mechi na baadhi ya wanachama watalazimika kulipa hadi Pauni 97 kwa mechi kubwa, kuanzia mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal Agosti, 17.
Takriban mashabiki 20,000 wanaonunua tiketi za mechi za nyumbani kupitia mfumo wa uanachama wataathirika kwa namna moja au nyingine.
Umoja wa Mashabiki wa Manchester United (MUST) umedai timu hiyo “haikushirikisha mashirika yoyote yanayowakilisha mashabiki” katika maamuzi hayo.
Hata hivyo, Afisa Mtendaji Mkuu, Omar Berrada amesisitiza walifanya mazungumzo na baadhi ya vyama vya mashabiki kabla ya kuamua.
Taarifa ya moja ya kundi la umoja wa mashabiki liitwalo MUST ilisomeka: “Baada ya msimu uliopita kuwa mgumu, tulitarajia timu ingefikiria upya mpango huu mpya wa upangaji wa tiketi.”
“Mpango huu utaongeza bei kwa kiasi kikubwa kwa mashabiki 20,000 kwa kila mechi wanayonunua tiketi moja moja.”
“Hili ni pigo lingine kali kwa mashabiki wa Manchester United.”
Mashabiki tayari walikuwa kwenye mvutano na timu hiyo baada ya Sir Jim Ratcliffe na wenzake kuanzisha kiwango cha Pauni 66 kwa wale wasio na tiketi za msimu, bila punguzo lolote, katikati ya msimu uliopita.
Mechi ya ufunguzi dhidi ya Arsenal ni moja ya mechi sita za Ligi Kuu zilizowekwa kwenye Kategoria A, zikiwa na bei ya kati ya Pauni 59 hadi 97 kwa wanachama.
Mechi nyingine katika Kategoria A ni dhidi ya Manchester City, Liverpool, Chelsea, Tottenham, na Newcastle.
Kategoria B inajumuisha mechi 11 za ligi, huku mechi dhidi ya Wolves na Sunderland zikiwa kwenye Kategoria C.
Mechi za Carabao na FA zimewekwa kwenye Kategoria D, ambayo ni ya bei ya chini zaidi.
Mabadiliko haya yatasababisha ongezeko la hadi asilimia 50 kwa mashabiki wanaonunua tiketi kwa mechi moja moja.
MUST waliongeza: “Kwa mara nyingine tena, hawakushirikiana na mwakilishi yeyote wa mashabiki katika maamuzi haya.”
“Na kama kawaida, wanafanya maamuzi yanayokwenda kinyume na masilahi ya mashabiki na timu kwa jumla.”
“Mfumo huu wa upangaji tiketi kwa aina ya mechi utaleta madhara makubwa.”
Hata hivyo, Man United ilisisitiza kuwa vikundi vya mashabiki vilihusishwa na inadai bei za sasa ni za chini ikilinganishwa na zile zilizopendekezwa awali kwa Bodi ya Ushauri wa Mashabiki ambao Berrada amesema wamekuwa na mazungumzo nao tangu uamuzi wa Pauni 66.
Hata hivyo, kundi jingine la mashabiki liitwalo The 1958, lilisema:”Hii ni dharau nyingine kwa mashabiki waaminifu.
Majadiliano na timu hakuna. Mashabiki wanapotoa malalamiko halali, timu hujibu kwa maneno ya kisiasa. Faida inawekwa mbele. Mashabiki ambao ndio roho ya timu hii wanawekwa mwisho.”