Mashabiki Chelsea wamzomea Enzo
Muktasari:
- Fernandez aliingia dakika ya 61 kuchukua nafasi ya nahodha Reece James, lakini mara tu alipoingia uwanjani sehemu ya mashabiki ilianza kumzomea huku wengine wakimshangilia na kuimba jina lake.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO wa Chelsea, Enzo Fernandez amejikuta katikati ya mjadala mkubwa baada ya mashabiki wa klabu hiyo kuonyesha hisia tofauti aliporejea uwanjani katika mchezo wa mwisho wa kirafiki wa kujiandaa na msimu mpya dhidi ya Real Sociedad.
Fernandez aliingia dakika ya 61 kuchukua nafasi ya nahodha Reece James, lakini mara tu alipoingia uwanjani sehemu ya mashabiki ilianza kumzomea huku wengine wakimshangilia na kuimba jina lake.
Mwitikio huo uliendelea kila mara alipokuwa akigusa mpira, jambo lililoonyesha jinsi mashabiki wa Chelsea walivyogawanyika kuhusu mustakabali wake ndani ya klabu hiyo.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Argentina pia alikabidhiwa kitambaa cha unahodha kutoka kwa James baada ya kuingia uwanjani.
Fernandez, mwenye umri wa miaka 25, amekuwa akihusishwa na nia ya kuondoka Stamford Bridge katika dirisha hili la usajili, huku akitajwa kutaka kutafuta changamoto mpya.
Mabingwa wa zamani wa England, Manchester City, wanaonolewa na kocha wa zamani wa Chelsea, Enzo Maresca, wamekuwa wakitajwa kuvutiwa na huduma zake, lakini Chelsea imeweka wazi kuwa klabu yoyote inayomhitaji lazima ilipe pauni milioni 120 (zaidi ya Sh300 bilioni).
Hata hivyo, hadi sasa hakuna ofa rasmi iliyowasilishwa kwa Chelsea, hali inayofanya viongozi wa klabu hiyo kuamini Fernandez atasalia Stamford Bridge msimu huu.
Ripoti zinaeleza kuwa Chelsea iliweka masharti ya mauzo kwa mchezaji huyo na wakala wake, Javier Pastore, tangu Mei mwaka huu, lakini hakuna klabu iliyofikia mahitaji hayo.
Mwezi Machi, Fernandez alizua mjadala baada ya kutoa kauli za kuikosoa Chelsea akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Argentina, huku pia akihusishwa na uwezekano wa kuhamia Real Madrid.
Hata hivyo, miamba hiyo ya Hispania ilikuja kutoa taarifa rasmi ikikanusha kuwa ilikuwa ikifuatilia usajili wake.
Pastore, ambaye aliwahi kucheza Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya Argentina, naye amekuwa akizungumza hadharani kuhusu uwezekano wa mchezaji huyo kuondoka Chelsea.
Fernandez alirejea mazoezini wiki hii baada ya kupewa mapumziko marefu kufuatia majukumu ya Kombe la Dunia, huku kocha mpya wa Chelsea, Xabi Alonso, akisisitiza kuwa anamtaka kiungo huyo kubaki klabuni.
Inaelezwa kuwa mara baada ya kutua Stamford Bridge, Alonso alimtafuta Fernandez moja kwa moja na kufanya mazungumzo maalumu kuhusu nafasi yake ndani ya kikosi hicho, ishara inayoonyesha kuwa bado ni sehemu muhimu ya mipango yake kuelekea msimu mpya.