Arteta vs Maresca vita ya kwanza ya taji Cardiff
Muktasari:
- Tofauti na miaka ya nyuma, mchezo huo mwaka huu utachezwa kwenye Uwanja wa Principality jijini Cardiff, badala ya Wembley.
CARDIFF, WALES: LEO Jumapili, Arsenal na Manchester City zitashuka dimbani kuwania Ngao ya Jamii (Community Shield) ya msimu wa 2026/27, mchezo ambao kwa kawaida huwa pazia la ufunguzi wa msimu mpya wa soka nchini England.
Tofauti na miaka ya nyuma, mchezo huo mwaka huu utachezwa kwenye Uwanja wa Principality jijini Cardiff, badala ya Wembley.
Arsenal wana kumbukumbu nzuri katika uwanja huo, hasa kutokana na kipindi ambacho Wembley mpya ulikuwa ukijengwa.
WANA REKODI BORA
Arsenal walicheza mechi nyingi zaidi kwenye uwanja huo kuliko timu nyingine yoyote kati ya mwaka 2001 na 2007, ikicheza 10 na kushinda mataji manne ya Ngao ya Jamii katika kipindi hicho.
Kwa upande wa Man City, imewahi kucheza kwenye uwanja huo mara moja pekee. Ilikuwa Agosti 2003, walipokutana na TNS katika mchezo wa kufuzu Kombe la UEFA na kushinda kwa mabao 2-0 hivyo kila mmoja anakwenda akiwa hana ugeni kwenye uwanja huo, lakini waliocheza kipindi hicho hawapo leo.
Pamoja na kwamba Community Shield mara nyingi huonekana kama taji lisilo na uzito mkubwa ukilinganisha na mataji mengine, timu zote mbili zitataka kuondoka Cardiff zikiwa na kombe hilo.
Kikosi cha Mikel Arteta kinaweza kujiamini zaidi kinapokabiliana na City ambayo imefanyiwa mabadiliko makubwa tangu Pep Guardiola alipoondoka mwishoni mwa msimu wa 2025/26 msimu ambao Arsenal ilifanya mambo makubwa kwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu baada ya kupita miaka 22 na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
FAIDA ARSENAL
Arsenal imekuwa ikifanya vizuri katika mechi za Ngao ya Jamii iliyochezahivi karibuni, baada ya kushinda tano za mwisho kwenye mashindano hayo.
Pia, walifanikiwa kushinda kila waliposhiriki Ngao wakiwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, katika miaka ya 1998, 2002 na 2004.
Zaidi ya hapo, Arsenal wameifunga Manchester City kila walipokutana nayo katika mechi hii.
Walishinda 4-0 mwaka 1934, 3-0 mwaka 2014 na baadaye wakashinda kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 1-1 mwaka 2023.
Arsenal ina jumla ya ushindi mara 17 katika historia ya Ngao hiyo, idadi inayowafanya kuwa timu ya pili nyuma ya Manchester United yenye ushindi 21.
Kwa upande mwingine, Man City imepoteza mechi hii mara tisa katika historia yake, ingawa ilishinda mara ya mwisho ilipokutana na Man United mwaka 2024 na ina mataji saba.
ARTETA NA REKODI NZURI
Alishinda mara mbili akiwa mchezaji mwaka 2014 na 2015, kabla ya kushinda mara nyingine mbili akiwa kocha mwaka 2020 na 2023.
Kwa Enzo Maresca, hii itakuwa mara yake ya kwanza kabisa kucheza au kuiongoza timu katika mechi hii mkubwa wa Ngao tangu ameanza kuwa kocha.
MARESCA NA HISTORIA
Maresca anaweza kuandika historia ya kipekee endapo atashinda Jumapili, kwani tayari amekuwa kocha wa kwanza wa Manchester City kushiriki ngao katika mchezo wake wa kwanza wa ushindani akiwa kwenye benchi la timu hiyo. Hata hivyo, Arsenal wana sababu kadhaa za kuwa waangalifu wanapojiandaa kwa mchezo huo.
Kwanza, katika miaka 10 iliyopita, mabingwa wa FA Cup ndio walioshinda Ngao mara nyingi zaidi, wakifanya hivyo mara nane kati ya 10.
Pia, katika mikutano yao ya hivi karibuni, Man City ndiyo imekuwa na rekodi nzuri zaidi dhidi ya Arsenal.
City imepoteza mchezo mmoja pekee kati ya sita za mwisho dhidi ya Arsenal, huku michezo miwili ikiisha kwa sare na mingine mitatu ikishindwa na Arsenal.
Kikosi cha Maresca pia kinaweza kuwa kigumu kufunguka kutokana na rekodi yake ya kujilinda. City imeweka ‘clean sheet’ katika michezo saba kati ya tisa ya mwisho ya ushindani.
Kwa sababu hiyo, haitakuwa jambo la kushangaza iwapo mchezo huu utaishia kwenye mikwaju ya penalti.
Hilo limekuwa jambo la kawaida katika mchezo wa ngao hivi karibuni, kwani michezo mitano kati ya saba iliyopita ya mashindano hayo imeamuliwa kwa mikwaju ya penalti.
MABADILIKO CITY
Kuhusu wachezaji watakaoanza kwa ajili ya dakika 90, Manchester City inatarajiwa kumkosa Rodri, ambaye inaonekana yuko njiani kuhamia Barcelona.
Barcelona bila shaka haitafurahishwa kuona nahodha huyo wa timu ya taifa ya Hispania akipata majeraha wakati mazungumzo ya uhamisho huo yakiaminika kuwa katika hatua muhimu.
Pia, kutokuwepo kwa Bernardo Silva na John Stones kutafanya kikosi cha kwanza cha City kionekane tofauti kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na kile kilichomaliza msimu uliopita.
Hata hivyo, hilo halimaanishi kwamba City haina ubora wa kutosha kushinda mchezo huo.
Kinyume chake, maandalizi yao ya msimu mpya hadi sasa yanaweza kusemwa kuwa yamekuwa bora kuliko ya Arsenal, huku Maresca akiwa bado hajapoteza mchezo tangu alipochukua jukumu la kuinoa City.
Manchester City inaweza kuwa na kazi kubwa mbele yake dhidi ya Arsenal ambayo tayari imejiongezea nguvu kwa kuwasajili Bruno Guimaraes na Christos Tzolis, huku ikitarajiwa kufanya usajili zaidi kabla ya dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi kufungwa.
Arsenal itaanza msimu wake wa Ligi Kuu dhidi ya Coventry, wakati Manchester City itaanza kampeni yake dhidi ya Bournemouth.