Martinez ni yeye tu
Muktasari:
- Kipa Altay Bayindir alipangwa kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England kuchukua nafasi ya Andre Onana ambaye bado hajawa fiti kutokana na kuumia na kufanya makosa kwenye kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Arsenal.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA Ruben Amorim wa Manchester United ameshindwa kuwashawishi mabosi kumsajili kipa Emiliano Martinez, imeelezwa.
Kipa Altay Bayindir alipangwa kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England kuchukua nafasi ya Andre Onana ambaye bado hajawa fiti kutokana na kuumia na kufanya makosa kwenye kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Arsenal.
Amorim alipaswa kuonyesha kwa dhati anahitaji huduma ya kipa mpya kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Lakini, taarifa za kutoka Argentina zinazofichuliwa na mwandishi Gaston Edul akidai kocha Amorim alishindwa kuwashawishi mabosi kwamba anahitaji Namba 1 kwenye kikosi chake msimu huu. Kwa muda sasa, Man United imehusishwa na kipa wa Aston Villa, Martinez.
Ofa ya Pauni 40 milioni ingefaa kumvuta kipa huyo mwenye umri wa miaka 32 kwenda kukipiga Old Trafford. Lakini, badala yake Man United iliamua kupeleka ofa ya kumpata kipa huyo kwa mkopo, ikakataliwa. Edul alisema kwenye chaneli ya YouTube 412: “Dili lilikaribia kabisa. Benchi la ufundi, hasa Amorim, walimhitaji na Martinez alitambua Amorim anamtaka. Amorim hakuishawishi bodi umuhimu wa kutumia pesa kusajili kipa mzuri.
“Mabosi walimwambia Onana yupo na aliwapojibu ndiyo, basi walichofanya mabosi ni kujaribu kumchukua kwa mkopo. Aston Villa iliweka wazi masharti yao yanayoweza kuwasukuma kumuuza kipa huyo.”
Ilifichuka tangu Juni mwaka huu kwamba Amorim alikuwa shabiki mkubwa wa kipa Martinez, ambaye alisajili mkataba wa miaka mitano huko Villa Park wakati wa dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, lakini ilibainishwa kwamba angehama kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya kutoa ishara ya kuaga mashabiki wakati wa mechi ya mwisho ya msimu. Ukimweka kando Martinez, Man United inaisaka huduma ya Gianluigi Donnarumma, ambaye hahitajiki Paris Saint-Germain baada ya kusajiliwa Lucas Chevalier.