Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mariga awakumbuka Ngassa, Kaseja

Mariga akiwa na mke wa wakala wake.

Muktasari:

  • Namweleza Mariga jinsi ambavyo Ngassa alikwama kucheza West Ham, kisha akakwama kucheza Marekani. Mwishowe namuuliza Mariga kama ingekuwa vizuri kwa Ngassa kuanza kucheza soka katika nchi za Scandinavia kama ilivyokuwa kwake kisha aibukie katika ligi kubwa za Ulaya.

TUNAENDELEA na simulizi ya mahojiano ya Mwanaspoti na mwanasoka wa kimataifa wa Kenya, McDonald Mariga, anayechezea klabu ya Parma ya Italia. Katika toleo lililopita alianza kuwazungumzia wanasoka wa Tanzania anaowafahamu, endelea...

“Kuna yule mchezaji wenu mfupi, ana kasi sana. Huwa anategemea mbio katika mchezo wake, anaitwa nani yule? Kuna wakati alienda West Ham kufanya trial (majaribio), iliishaje ile deal (mpango)?” anahoji Mariga.

Moja kwa moja natambua kwamba Mariga anamzungumzia Mrisho Ngassa, staa wa Simba na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars. Namtajia jina la Ngassa na moja kwa moja anamkumbuka vizuri zaidi.

“Yeah Ngassa. Anajua sana yule dogo. Mechi zetu za Harambee Stars ndiye ambaye alikuwa anatusumbua sana na muda wote makocha walikuwa wanatuambia tumwangalie zaidi yeye. Bado anacheza Tanzania yule?” anahoji Mariga.

“Mwingine ni yule kipa wenu anaitwa Juma (Kaseja), bado yupo yule? Kipa mzuri hivi mfupi mfupi. Anadaka vizuri sana, bado yupo?” anahoji Mariga kwa shauku kubwa.

Namweleza Mariga jinsi ambavyo Ngassa alikwama kucheza West Ham, kisha akakwama kucheza Marekani. Mwishowe namuuliza Mariga kama ingekuwa vizuri kwa Ngassa kuanza kucheza soka katika nchi za Scandinavia kama ilivyokuwa kwake kisha aibukie katika ligi kubwa za Ulaya.

“Hapana. Si lazima. Katika soka nafasi ikitokea itumie hapo hapo. Kama hakuitumia vizuri nafasi yake ya kwenda West Ham basi hilo ni tatizo. Mimi nilianzia soka Ulaya nikicheza daraja la tatu Sweden. Nafasi huwa haiji mara mbili,” anasema Mariga.

Ghafla Mariga anaikumbuka zaidi Tanzania. Anakumbuka watu wake na kuwasifia kuwa ni watu wazuri. Anakumbuka klabu za usiku kama Club Billicanas na nyinginezo.

Anaikumbuka mechi ya mwisho ya Kirafiki kati ya Harambee Stars na Taifa Stars iliyochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Cha kushangaza anamkumbuka hadi Mwandishi wa Mwanaspoti, Doris Mallyaga.

“Doris yupo yule? Mwambie namsalimia sana,” anasema huku akitabasamu.

Pamoja na kuwa yuko mbali na Afrika Mashariki kwa sasa, Mariga anafuatilia kwa karibu soka la ukanda huu huku akiamini kuwa linakua na hasa Tanzania.

“Najua kwamba Tanzania kuna pesa nyingi katika soka kuliko Kenya na Uganda. Nasikia kuna wachezaji wengi wa Kenya wanacheza Tanzania. Mimi namjua zaidi Jerry Santo kwa sababu niko naye katika timu ya taifa,” anaongeza.

Hapo hapo namuuliza Mariga, ni wachezaji gani kutoka Kenya aliowaacha nyumbani ambao anaamini kuwa walikuwa na vipaji vikubwa kuliko yeye, lakini wameshindwa kufikia hatua aliyofikia. Mariga anakuwa makini kujibu swali hili.

“Unajua wakati mwingine kucheza na kupata mafanikio makubwa kama mimi inakuwa ni bahati vile vile, Mungu naye anapanga. Nilipokuwa Sweden kulikuwa na wachezaji wengine kama Mambo (Robert Mambo), Titus Mulama. Ni wachezaji wazuri sana, lakini ndio hivyo tena,” anasema Mariga.

Mariga anakiri kwamba huenda yeye na mdogo wake watafungua njia kwa wanasoka wa Afrika Mashariki na Kati kucheza soka la kulipwa katika ligi kubwa za Ulaya.

“Sasa hivi watatuamini kwa sababu mimi na Mugabe tunafanya vizuri. Wachezaji wa Afrika Mashariki wanaweza kufanya vizuri huku. Sioni tatizo lolote, kama mimi nimeweza kwanini wengine washindwe?” Anahoji Mariga.

Wakati tunaendelea kuongea na Mariga, ghafla kengele ya mlangoni kwake inalia. Ananyanyuka kwenda kuwafungulia wageni wake. Anarudi na wazungu watatu.

“Huyu hapa ni wakala wangu anaitwa Lorenzo Marchesi. Ndiye anayeshughulikia masuala yangu yote ya uhamisho. Lakini pia yeye na ndugu zake ndio rafiki zangu wa karibu hapa Parma. Mara nyingi tunatoka usiku pamoja,” anasema akitoa utambulisho huo.

“Unajua hapa nawajua Wakenya watatu tu na wote wako bize na mambo yao kwa hiyo mimi na Lorenzo pamoja na wadogo zake ndio tunazunguka pamoja.”

Katika kuonyesha kuwa Mariga bado anatamani kuona Ngassa anafanikiwa, anamgusia Marchesi kuhusu uwezo wa Ngassa huku wakitumia lugha ya Kiitaliano.

“Nilikuwa namwambia hapa Marchesi jinsi ambavyo Afrika Mashariki kuna wachezaji wazuri na kwamba kuna mchezaji wa Tanzania ambaye amewahi kufanya trial West Ham.” Anasema Mariga.

Kiitaliano baina ya Mariga na Marchesi kinanikosha zaidi. Mariga ananiarifu kuwa anaongea Kiitaliano kwa ufasaha sana, hiyo ni baada ya kumuuliza anaongea lugha ngapi kwa ufasaha.

Wakati beki wa Fulham, Philippe Senderos na Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger wakiwa wanasifika kwa kuongea lugha nyingi, Mariga naye ni miongoni mwa wanasoka wanaoongea lugha nyingi.

Je Mariga anaongea lugha ngapi? Fuatilia simulizi hii Jumamosi ijayo ambapo pia utapata kujua ni timu gani kubwa kati ya Manchester United, Arsenal na Liverpool ambayo mdogo wake, Victor Mugabe Wanyama anaweza kucheza msimu ujao.