Marc Guehi azisubirisha Real Madrid, Liverpool na Barcelona
Muktasari:
- Awali beki huyu ambaye anawindwa na wababe wengi Ulaya, alihusishwa na Liverpool katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, lakini dili lilifeli dakika za mwisho licha ya yeye mwenyewe kukubali kujiunga na majogoo hao.
INAELEZWA beki kisiki wa Crystal Palace, Marc Guehi mwenye umri wa miaka, 25, yupo tayari kusubiri hadi mwisho wa msimu huu ili kufanya uamuzi wa wapi atakwenda baada ya kumalizika kwa mkataba wake.
Awali beki huyu ambaye anawindwa na wababe wengi Ulaya, alihusishwa na Liverpool katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, lakini dili lilifeli dakika za mwisho licha ya yeye mwenyewe kukubali kujiunga na majogoo hao.
Kwa sasa Real Madrid na Barcelona ni miongoni mwa timu ambazo zinahitaji saini yake katika dirisha lijalo, lakini sasa zitabidi zisubiri hadi mwisho wa msimu kujua hatma ya nyota huyo wa kimataifa wa England.
Liverpool pia bado inamwona kama chaguo sahihi la kuongeza nguvu kwenye safu yao ya ulinzi ambayo Virgil van Dijk umri umeanza unamtupa mkono, huku Ibrahim Konate mkataba wake ukimalizika mwisho wa msimu.
Ibrahima Konate
Liverpool imempa ofa ya mkataba mpya kwa beki wao wa kimataifa wa Ufaransa, Ibrahima Konate, 26, ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika mwisho wa msimu huu.
Hata hivyo, hadi sasa Konate bado hajakubali ofa hiyo kwa sababu anasikilizia kwanza kujua kama Madrid bado inahitaji saini yake dirisha la majira ya kiangazi mwakani.
Madrid inatamani sana huduma ya fundi huyu ili akawe mbadala wa Eder Militao na David Alaba ambao ni majeruhi wa mara kwa mara.
Dayot Upamecano
BEKI wa Bayern Munich, Dayot Upamecano, 27, ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, ameziingiza vitani Real Madrid, Inter Milan na Liverpool zinazotaka kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Licha ya kupata ofa kutoka kwa timu zinazohitaji saini yake Januari mwaka huu, Upamecano, ambaye amecheza zaidi ya mechi 40 akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa, anataka kumaliza msimu akiwa na Bayern kisha afanye uamuzi wa wapi atatua.
Federico Chiesa
WINGA wa Liverpool, Federico Chiesa, 28, anaripotiwa kufikiria kuondoka timu hiyo Januari mwakani kutokana na ukosefu wa muda mwingi wa kucheza. Klabu nne za Serie A ambazo ni Inter Milan, Napoli, AS Roma na AC Milan zimetajwa kutaka kumsajili. Tangu kuanza kwa msimu huu Chiesa amecheza mechi 13 za michuano yote. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Murillo
KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca amemweka beki wa Nottingham Forest, Murillo Pires, 23, kama chaguo lake la kwanza katika orodha ya mabeki anaohitaji wasajiliwe dirisha lijalo. Hata hivyo, kumekuwa na ushindani kutoka kwa Arsenal na Barcelona, ambazo zote zinafuatilia kwa karibu beki huyo wa kimataifa wa Brazil ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Casemiro
Manchester United inataka kumbakisha kiungo wake mkongwe, Casemiro, 33, kwa kumpa mkataba mpya, lakini kwa sharti moja muhimu la kukubali apunguze mshahara wake wa sasa. Casemiro kwa sasa analipwa zaidi ya Pauni 350,000 kwa wiki na Man United inataka kulipa chini ya hapo ili kubana matumizi na kuendana na kanuni za usawa wa matumizi ya fedha. Staa huyu amekuwa akiminika sana na kocha Ruben Amorim.
Joao Neves
LIVERPOOL inaandaa dau nono la Pauni 40 milioni kumnasa kiungo wa kimataifa wa Ureno anayekipiga PSG, Joao Neves, 21. Nyota huyo ambaye amekuwa na kiwango bora tangu msimu uliopita, alitua PSG akitokea Benfika na Liverpool inaona atakwenda kumaliza shida kwenye nafasi ya kiungo inayoonekana kudorora. Msimu huu amefunga mabao matano katika mechi saba za League 1.
Pedro Neto
WINGA wa kimataifa wa Ureno anayekipiga Chelsea, Pedro Neto, 25, amekuwa chaguo muhimu la Barcelona inayotaka kumsajili mwisho wa msimu huu, dirisha la majira ya kiangazi. Mkurugenzi wa michezo wa miamba hiyo ya La Liga, Deco ni shabiki wake na hivyo kuongeza uwezekano wa nyota huyo ambaye amekuwa na kiwango bora Darajani, kutua La Liga.