Fenerbahce, Lewandowski kuna mchongo unasikiliziwa
Muktasari:
- Inaelezwa vigogo hao wamempa ofa ya mkataba wa miezi 18 lakini Lewandoski amekataa na kusisitiza anahitaji walau mkataba wa miaka mitatu.
FENERBAHCE ya Uturuki inataka kumsajili mshambuliaji mkongwe wa Barcelona na timu ya taifa ya Poland, Robert Lewandowski, mwenye umri wa miaka 37, ambaye ameripotiwa ataondoka katika viunga vya Nou Camp mwisho wa msimu huu.
Inaelezwa vigogo hao wamempa ofa ya mkataba wa miezi 18 lakini Lewandoski amekataa na kusisitiza anahitaji walau mkataba wa miaka mitatu.
Barca inataka kuachana na mshambuliaji huyu kutokana na umri wake pia mshahara wake mkubwa na wanaamini akiondoka utawawezesha kusajili wachezaji wengi na kuwaingiza katika mfumo bila ya kuwa na shida ya kanuni za masuala ya kifedha zilizowekwa na La Liga.
Fenerbahce inataka kumpa Lewandoski mshahara unaokadiriwa kufikia Pauni 200,000 na mchezaji mwenywe anaonekana kukubali lakini changamoto ambayo bado haijatatuliwa ni masuala ya muda wa mkataba.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Lewandowski amecheza mechi 13 za michuano yote na kufunga mabao nane. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
Karim Adeyemi
Mshambuliaji wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Ujerumani, Karim Adeyemi, anataka kujiunga na Arsenal badala ya Manchester United, licha ya klabu zote mbili kuonyesha nia ya kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22. Mabosi wa Dortmund wanadaiwa kuwa tayari kumwachia fundi huyu lakini kwa dau litakaloanzia Pauni 60 milioni. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Jadon Sancho
WINGA wa Manchester United, Jadon Sancho, mwenye umri wa miaka 25, ameambiwa atalazimika kupunguza mshahara wake hadi kufikia Pauni 150,000 kwa wiki ikiwa anataka kutua Borussia Dortmund katika dirisha lijalo la majira ya baridi.
Sancho ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, anatamani sana kuondoka Man United kwa sababu hapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha wababe hao.
Christos Mandas
WOLVES inamtaka kipa wa Lazio, Christos Mandas, ambaye ifikapo Januari anaweza kununuliwa kwa Pauni 12 milioni.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24, amekuwa katika kiwango bora kwenye kikosi cha Lazio tangu alipoanza kupewa nafasi baada ya majeraha ya aliyekuwa kipa namba moja Ivan Provedel. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Vitaly Janelt
Eintracht Frankfurt inafanya juhudi kuhakikisha inamsajili kiungo wa Brentford, Vitaly Janelt lakini mambo yanaonekana kuwa magumu.
Taarifa zinaeleza Brentford haipo tayari kumwachia mchezaji huyu na sasa ipo katika mazungumzo ya kumsainisha mkataba mpya wakati ule wa sasa ukiatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Janelt mwenye umri wa miaka 27, tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 10 za michuano yote.
Ahmed Abdullahi
SUNDERLAND ipo tayari kumruhusu mshambuliaji wao wa kimataifa wa Nigeria Ahmed Abdullahi, 21, kuondoka kwa mkopo Januari mwakani.
Abdullahi alijiunga na Sunderland mwaka 2023 akitokea TikiTaka Academy Nigeria na anatolewa kwa mkopo ili kupata muda mwingi zaidi wa kucheza tofauti na ilivyo sasa.
Timu kadhaa za Ligi Kuu Ufaransa na Ubelgiji zimeonyesha nia ya kumsainisha mkataba wa mkopo wa nusu msimu.
Jorthy Mokio
HADI sasa Manchester United ndiyo inayoonekana kuwa kinara katika mbio za kuiwania saini ya beki chipukizi wa Ajax, Jorthy Mokio, mwenye umri wa 17, ambaye pia anahitajika na Tottenham na Newcastle United. Mokio ni miongoni mwa mabeki vijana wanaofanya vizuri kwa sasa katika Ligi Kuu Uholanzi. Man United inamwona kama mrithi sahihi wa Lisandro Martinez.
Antoine Semenyo
MABOSI wa Arsenal hawana mpango wa kumsajili mshambuliaji wa Bournemouth, Antoine Semenyo, 25, dirisha lijalo la usajili la Januari.
Semenyo anatajwa kuhitajika sana na Liverpool ili kwenda kuziba pengo la Mohamed Salah ambaye amekuwa katika kiwango bora tangu msimu uliopita. Liverpool ipo tayari kutoa zaidi ya Pauni 70 milioni.