Marc Guehi aitosa Liverpoll ataka kutimkia Real Madrid
Muktasari:
- Guehi, ambaye ni kiungo tegemeo wa Palace na timu ya taifa ya England, amebadilisha mawazo yake baada ya Madrid kuonyesha nia ya kutaka kumsajili licha ya kwamba alifanya makubaliano binafsi na vigogo wa Liverpool.
BEKI kisiki wa Crystal Palace, Marc Guehi, mwenye umri wa miaka 25, amewaambia washauri wake anapendelea kujiunga na Real Madrid baada ya mpango wake wa kutua Liverpool kufeli dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Guehi, ambaye ni kiungo tegemeo wa Palace na timu ya taifa ya England, amebadilisha mawazo yake baada ya Madrid kuonyesha nia ya kutaka kumsajili licha ya kwamba alifanya makubaliano binafsi na vigogo wa Liverpool.
Katika msimu uliopita Guehi aliisaidia Palace kushika nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu Engkand ambapo alicheza mechi 32 za ligi hiyo na kufunga bao moja.
Mkataba wa fundi huyu unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na anadaiwa kuwa amekataa kusaini mkataba mpya licha kuwekewa ofa mezani na timu yake.
Palace inapambana kumsainisha mkataba mpya ili asiondoke bure mwisho wa msimu lakini haionekani hilo likifanikiwa na mwenyewe amekuwa na hamu ya kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine.
Erling Haaland
BARCELONA imepanga kufanya kila linalowekana kwa kubana matumizi na kuongeza mapato zaidi ili kufanikisha kumsajili straika wa Manchester City, Erling Haaland dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Hivi karibuni Barca imeripotiwa kutaka kumsajili fundi huyu lakini hali yao ya kiuchumi kwa sasa haiwaruhusu kufanya usajili mkubwa kiasi hicho. Barca inamwona Haaland kama mbadala sahihi wa Robert Lewandowski, 37 ambaye huenda akaondoka.
Carlos Baleba
MABINGWA watetezi wa taji la Ligi Kuu England, Liverpool, wanamfuatilia kiungo wa Brighton, Carlos Baleba, 21, ambaye pia yupo kwenye rada ya Manchester United. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Cameroon anadaiwa kuuzwa kwa takribani Pauni 50 milioni. Mwenyewe amewasiliana na mabosi wa Brighton na kuwaeleza dhamira yake ya kutaka kuondoka. Kuna uwezekano bei tajwa hapo juu ikapanda kutokana na ongozeko la timu zinazohitaji.
Oihan Sancet
TOTTENHAM Hotspur na Arsenal ni miongoni mwa klabu za Ligi Kuu England zinazomfuatilia kiungo wa Athletic Bilbao, Oihan Sancet, 25, raia wa Hispania. Sancet ameonyesha ubora mkubwa hususani katika suala la kutengeneza mashambulizi jambo ambalo limezishawishi timu hizo kutoka London. Msimu uliopita alifunga mabao 10 katika mechi 34 pamona na kutoa asisti nane.
Federico Valverde
MANCHESTER United ipo tayari kumtoa kiungo wao wa kimataifa wa England, Kobbie Mainoo, 20, pamoja na kiasi cha fedha ili kuipata huduma ya kiungo Federico Valverde wa Real Madrid katika dirisha lijalo. Hata hivyo, Real Madrid hainokani kuwa tayari kumuuza Valverde, 27, kwa sasa kutokana na umuhimu wake. Msimu uliopita alicheza mechi 38 za michuano yote.
Senne Lammens
INAELEZWA kipa wa Manchester United, Senne Lammens, 23, alikataa kujiunga na Aston Villa dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana na badala yake akajiunga na Man United. Villa ilikuwa inamwona Lammens kama mbadala sahihi wa Emiliano Martinez aliyekuwa anahisishwa kuondoka mwisho wa msimu uliopita. Hata hivyo, kipa huyo bado hajaanza kucheza na amekuwa akiishia benchi kumpisha Altay Bayındır.
Frenkie de Jong
BAYERN Munich na Manchester United zimeonyesha nia ya kumsajili kiungo wa Barcelona, Frenkie de Jong, 28, ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu. Staa huyu kuna uwezekano akauzwa Januari mwakani kwa sababu vigogo wa Barca hawataki kuona akiondoka bure mwisho wa msimu. Msimu uliopita, alicheza mechi 36 za La Liga akaoa asisti tisa na mabao matatu.
Manor Solomon
CRYSTAL Palace inafikiria kuanza tena mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Israeli, Manor Solomon, 26, kutoka Tottenham, dirisha lijalo baada ya kufeli lililopita la majira ya baridi. Dili hilo lilifeli kwa sababu Spurs ilikuwa inataka Palace ilipe mshahara wote wa staa huyo pia itoe ada ya uhamisho wa mkopo jambo ambalo Palace haikuwa imelikubali.