Manchester United yamwinda nyota Barcelona
Muktasari:
- Kiungo huyo amekuwa na mchango mkubwa ndani ya Barcelona msimu huu, akifunga mabao matano na kuvutia macho ya klabu mbalimbali zinazotaka kuimarisha safu zao za ushambuliaji.
MANCHESTER, ENGLAND: Manchester United imeonyesha nia ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa Barcelona, Fermin Lopez, katika dirisha lijalo la usajili, ikiwa sehemu ya mkakati wa kuongeza makali ya safu yake ya ushambuliaji.
Lopez, mwenye umri wa miaka 23, anatajwa kuwa na thamani ya takribani Pauni 70 milioni (zaidi ya Sh140 bilioni), huku vigogo wengine wa soka barani Ulaya, Paris Saint-Germain (PSG) na Chelsea, nao wakitajwa kumwania nyota huyo wa kimataifa wa Hispania.
Kiungo huyo amekuwa na mchango mkubwa ndani ya Barcelona msimu huu, akifunga mabao matano na kuvutia macho ya klabu mbalimbali zinazotaka kuimarisha safu zao za ushambuliaji.
Taarifa zinaeleza kuwa Manchester United imekuwa ikimfuatilia Lopez kwa muda mrefu, ingawa changamoto ya kifedha inaweza kuwa kikwazo katika kufanikisha dili hilo.
Hata hivyo, mahitaji ya United kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji yameongezeka baada ya mshambuliaji wake kutoka Slovenia, Benjamin Sesko, kupata majeraha ya mfupa wa muundi (shin), yanayohofiwa kumuweka nje ya uwanja hadi Januari.
Hali hiyo imeiacha timu hiyo ikiwa na upungufu wa mshambuliaji wa kati, huku kocha Michael Carrick akihitaji haraka suluhisho la kuziba pengo hilo.
Katika hatua nyingine, United pia imehusishwa na mshambuliaji wa Leeds United, Dominic Calvert-Lewin, ambaye iliwahi kumuangalia wakati akiwa Everton lakini haikufanikisha usajili wake.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa za Daily Mail Sport, uwezekano wa United kumsajili Calvert-Lewin unaonekana kuwa mgumu kutokana na upinzani mkubwa wa kihistoria kati ya klabu hizo mbili.
Calvert-Lewin, 29, ameimarisha kiwango chake tangu ajiunge na Leeds kwa uhamisho wa bure katika majira ya joto ya mwaka 2025, baada ya kukumbwa na majeraha yaliyodhoofisha kipindi chake cha mwisho akiwa Everton. Mshambuliaji huyo wa England amefunga mabao 20 katika mechi 49 alizoichezea Leeds, yakiwemo matano katika mechi 10 za mwanzo wa msimu huu.
Kutokana na mchango wake, Leeds inatajwa kuwa kwenye mazungumzo ya kumpa mkataba mpya mshambuliaji huyo ili kuendelea kunufaika na huduma yake.
Mbali na safu ya ushambuliaji, Manchester United pia inatarajiwa kuangalia uwezekano wa kuongeza mabeki katika dirisha la Januari, iwapo itakuwa na fedha za ziada za kufanya usajili.
Kwa sasa, macho ya mashabiki wa United yataelekezwa katika mipango ya klabu hiyo ya usajili, huku Lopez akiwa miongoni mwa majina yanayovutia zaidi katika orodha ya wachezaji wanaowindwa na vigogo hao wa England.