Manchester City kuzijaza noti klabu EPL
Muktasari:
- Takwimu zilizotolewa na wataalamu wa data wa OLBG zinaonyesha kuwa jumla ya pauni 527,935,464 zinaweza kudaiwa kutoka kwa City, kwa kuzingatia misimu kuanzia 2011/12 hadi msimu uliopita.
LONDON, ENGLAND: MANCHESTER City inaweza kulazimika kulipa zaidi ya pauni500 milioni kwa klabu 38 za Ligi Kuu England kutokana na mapato ya zawadi za ligi ambayo zingepoteza kwa miaka iliyopita, iwapo adhabu hiyo itatekelezwa kufuatia hukumu ya kukiuka kanuni za fedha.
Takwimu zilizotolewa na wataalamu wa data wa OLBG zinaonyesha kuwa jumla ya pauni 527,935,464 zinaweza kudaiwa kutoka kwa City, kwa kuzingatia misimu kuanzia 2011/12 hadi msimu uliopita.
Hata hivyo, kiasi hicho ni makadirio ya kinadharia, si fidia iliyoamriwa kulipwa na Ligi Kuu England. Hakuna uamuzi wa mwisho kuhusu adhabu ya klabu hiyo ambao umetangazwa.
City ilitajwa kukutwa na hatia katika mashtaka 114 kati ya 115 yaliyokuwa yakikabiliwa tangu mwaka 2023, baada ya uchunguzi wa miaka minne uliofanywa na kamati huru.
Licha ya hukumu hiyo, adhabu bado haijakamilishwa huku City ikiendelea kupinga tuhuma hizo na kupanga kukata rufaa.
Mashtaka hayo yalihusisha ukiukaji wa kanuni za Udhibiti wa Fedha za UEFA (FFP) pamoja na kanuni za Ligi Kuu England za faida na uendelevu wa kifedha (PSR).
City inakabiliwa na adhabu mbalimbali zinazoweza kujumuisha kupokonywa pointi, faini kubwa na hata kushushwa daraja.
Kwa mujibu wa OLBG, makadirio hayo yamekokotolewa kwa kuangalia kiasi cha fedha ambacho kila klabu ingepata iwapo City ingeondolewa kwenye msimamo wa ligi katika kila msimu husika.
Hali hiyo ingesababisha klabu nyingine kupanda nafasi moja kwenye msimamo na hivyo kupata mgao mkubwa zaidi wa fedha za zawadi, ambazo huongezeka kadiri timu inavyomaliza katika nafasi ya juu.
Takwimu za msimu uliopita ni makadirio kwa sababu Ligi Kuu England bado haijachapisha malipo rasmi ya msimu wa 2025/26.
Everton inatajwa kuwa mnufaika mkubwa zaidi, ikikadiriwa kupata pauni 28,944,186, huku wapinzani wao wakubwa, Manchester United, wakitajwa kuwa wa pili kwa uwezekano wa kulipwa pauni 28,118,305.
Arsenal, Chelsea na Liverpool kila moja inaweza kupata zaidi ya pauni milioni 20 kutokana na hesabu hizo.
Mwenyekiti wa Man City, Khaldoon Al-Mubarak, anaendelea kusisitiza kuwa klabu hiyo haina hatia na anaamini itafutiwa mashtaka yote kupitia rufaa.
Hata hivyo, baadhi ya wanasheria wanaamini kuwa hata rufaa ikikataliwa, City inaweza kupeleka suala hilo katika Mahakama Kuu ya England.
Iwapo hatua hiyo itachukuliwa, kesi hiyo isiyo ya kawaida inaweza kuendelea hadi mwaka 2028.