Man United yatoa msimamo kwa Rasmus Hojlund
Muktasari:
- Fundi huyu anawindwa sana na Napoli na RB Leipzig ambazo zote zipo katika mazungumzo na Man United juu ya usajili wa staa huyo.
MANCHESTER United imeiambia Napoli na timu zote zinazomhitaji mshambuliaji wao wa kimataifa wa Denmark, Rasmus Hojlund, 22, zinatakiwa kutoa pesa au kumchukua kwa mkopo wenye kipengele cha kumnunua jumla staa huyo.
Fundi huyu anawindwa sana na Napoli na RB Leipzig ambazo zote zipo katika mazungumzo na Man United juu ya usajili wa staa huyo.
Hojlund, aliyesajiliwa kutoka Atalanta kwa takribani Pauni 72 milioni mwaka 2023, mkataba wake na Man Uniyed unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Msimu uliopita Rasmus alikuwa mmoja kati ya wachezaji waliocheza mechi nyingi za Man United na jumla alicheza 52, akafunga mabao 10 na kutoa asisti nne.
Hata hivyo, nafasi yake katika kikosi cha kwanza haionekani kuwepo kutokana na usajili ambao mashetani hao wekundu wameufanya katika dirisha hili.
Staa huyu amepewa ruhusa ya kuondoka katika dirisha hili ikiwa atapata timu itayotoa pesa sahihi inayohitajika.
Mbali ya Napoli, Rasmus pia anahusishwa na AC Milan na huenda akaondoka dirisha hili kabla halijafungwa.
Morgan Rogers
ARSENAL inaangalia uwezekano wa kuwasilisha ofa kwenda Aston Villa kumsajili kiungo wa klabu hiyo na timu ya taifa ya England, Morgan Rogers,23, katika dirisha hili la majira ya kiangazi, lakini Villa wamesisitiza watazingatia tu ofa zitakazoanzia Pauni 80 milioni. Rogers ambaye alijiunga na Villa kutoka Middlesbrough Januari 2024 kwa ada ya karibu Euro 8.5 milioni, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
Harvey Elliott
RB Leipzig imefikia makubaliano binafsi na kiungo wa Liverpool, Harvey Elliott. Hata hivyo, uhamisho huu unategemea hatma ya kiungo wa Uholanzi, Xavi Simons, 22, ambaye yupo karibu kukamilisha dili lake la kwenda Chelsea. Simons, ambaye alikuwa kwa mkopo Leipzig msimu uliopita akitokea PSG kabla hajasaini mkataba wa kudumu, anatarajiwa kujiunga na Chelsea kwa ada ya Pauni 60 milioni.
Kostas Tsimikas
MARSEILLE inataka kumsajili beki wa kushoto wa Liverpool, Kostas Tsimikas 29, ambaye ameomba kuondoka dirisha hili la majira haya ya kiangazi. Tsimikas alijiunga na Liverpool mwaka 2020 akitokea Olympiacos, lakini amekuwa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu uliopita alicheza mechi 29 za michuano yote.
Matty Cash
NOTTINGHAM Forest inataka kumsajili beki wa kimataifa wa Poland ambaye kwa sasa anaichezea Aston Villa, Matty Cash, 28, dirisha hili. Cash aliwahi kuichezea Forest kati ya mwaka 2016 hadi 2020 kabla ya kuhamia Villa kwa Pauni16 milioni. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu uliopita alicheza mechi 38 za michuano yote. Villa haionekani kuwa tayari kumuuza kwa sasa.
Tyler Dibling
EVERTOM bado inataka kusajili mchezaji mmoja kabla dirisha hili kufungwa na ripoti zinadai macho na masikio yao yote yapo kwa kwa mshambuliaji chipukizi wa Southampton, Tyler Dibling, 19, ambaye iliwasilisha ofa hapo awali lakini ilikataliwa. Staa huyu anayeichezea timu ya vijana ya England chini ya miaka 20, alionyesha kiwango bora msimu uliopita akwa na Soton kuanzia timu ya vijana.
Nathan Collins
MABOSI wa Tottenham Hotspur wameongeza jitihada zao katika mchakato wa kumsajili beki wa kati wa Brentford, Nathan Collins, 24, ambaye pia anahitajika na Liverpool katika dirisha hili. Collins alisajiliwa na Brentford kutoka Wolves kwa rekodi ya uhamisho ya klabu hiyo ya Pauni 23 milioni mwaka 2023, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Axel Disasi
BOURNEMOUTH imefungua mazungumzo na Chelsea ili kuipata huduma ya beki wa kati wa timu hiyo na Ufaransa, Axel Disasi, 27, dirisha hili. Disasi aliyejiunga na Chelsea akitokea AS Monaco kwa Pauni 38.5 milioni anataka kuondoka kwa sababu ya kujiunga na timu itakayompa nafasi kubwa zaidi ya kucheza. Mkataba wa Disasi unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.