Man United yarudi sokoni kusaka straika
Muktasari:
- Miamba hiyo ya Old Trafford, tayari imeshatumia Pauni 125 milioni kwenye usajili wa dirisha hili baada ya kumnasa Matheus Cunha kutoka Wolves na Bryan Mbeumo kutoka Brentford. Wawili hao kwa pamoja walifunga mabao 35 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita.
LONDON, ENGLAND: MANCHESTER United inapambana kwa nguvu zote kunasa straika mpya kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Miamba hiyo ya Old Trafford, tayari imeshatumia Pauni 125 milioni kwenye usajili wa dirisha hili baada ya kumnasa Matheus Cunha kutoka Wolves na Bryan Mbeumo kutoka Brentford. Wawili hao kwa pamoja walifunga mabao 35 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita.
Wakati mastraika wa Man Unted, Rasmus Hojlund na Joshua Zirkzee walikuwa butu mbele ya goli na kupambana na hali zao kwa msimu uliopita.
Kutokana na hilo, kocha Ruben Amorim atalazimika kuingia sokoni kunasa straika mpya kabla ya dirisha kufungwa mapema Septemba.
Na kwenye hilo la kusaka huduma ya straika mpya, Man United imeweka ubaoni majira ya washambuliaji saba wa kati, ikimsaka mmoja atue Old Trafford.
Mtaalamu wa masuala ya usajili, Ben Jacobs alisema kipaumbele cha Man United kwa sasa kipo kwenye kuboresha safu ya ushambuliaji kwa maana ya kutafuta straika baada ya usajili wa Mbeumo.
“Imesajili watu walionyesha ubora kwenye Ligi Kuu England na sasa wanahitaji Namba 9 kwenda kuongoza mashambulizi. Kunasa straika ndio kipaumbele chao,” alisema Jacobs.
Mastraika gani kwenye rada? Man United imeshafahamu mastraika inaowasaka ili waje kwenye kikosi chao baada ya kuwakosa Hugo Ekitike na Viktor Gyokeres, ambao wa kwanza ameshatua Liverpool na mwingine atakwenda Arsenal.
Wakali wote hao wawili, awali walikuwa kwenye rada za Man United. Lakini, sasa Man United imelekeza nguvu kwa mastraika Benjamin Sesko, Nicolas Jackson, Ollie Watkins, Dominic Calvert-Lewin na Aleksandar Mitrovic, ikijadili namna ya kunasa huduma ya mmoja wao. Na kwenye hilo, Jacobs aliongeza: “Kuna majina machache yanajadiliwa huko ndani Man United. Benjamin Sesko ni mmoja wa anayewavutia, lakini pia bei yake itashuka mwishoni mwa Julai au mwanzoni mwa Agosti. Kwenye mkataba wake kuna kipengele kinachodaiwa kutaja bei ya Pauni 69 milioni na hakika kama Sesko atatua Man United, basi watakuwa wamepata kitu cha maana.”
Hojlund na Zirkzee itakuwaje? Kitendo cha Man United kutaka straika mpya hilo linaibua utata wa kuhusu hatima za wakali Hojlund na Zirkzee. Wawili hao bado wana mikataba mirefu kwenye kikosi hicho, miaka mitatu na minne mtawalia.
Hata hivyo, kitendo cha kufunga mabao 17 tu wote wawili kwenye michuano yote ya msimu uliopita, ndicho kitu kinachowafanya waletewe straika mpya.
Jacobs alisema: “Wanataka kusajili Namba 9 ili aje kushindania namba na Hojlund na Zirkzee au ambadili mmoja wao. Hicho ndicho kinachovutia zaidi. Nadhani Zirkzee ana nafasi kubwa ya kubaki na Hojlund itabidi apambane sana kupiga hatua kubwa zaidi.”