Bukayo Saka afunguka, atupia hat-trick
Muktasari:
- Winga huyo wa Arsenal mwenye umri wa miaka 24 aling’ara kwa kufunga mabao mawili kipindi cha kwanza kabla ya kukamilisha hat-trick yake kwa mkwaju wa penalti katika dakika za mwisho za mchezo, uliokuwa miongoni mwa mechi zenye mabao mengi zaidi kwenye mashindano hayo.
DALLAS, MAREKANI: MSHAMBULIAJI Bukayo Saka ameibuka shujaa wa England baada ya kufunga mabao matatu na kuiongoza timu hiyo kutwaa medali ya shaba ya Kombe la Dunia kwa ushindi wa kusisimua wa mabao 6-4 dhidi ya Ufaransa katika mchezo wa kusaka nafasi ya tatu.
Winga huyo wa Arsenal mwenye umri wa miaka 24 aling’ara kwa kufunga mabao mawili kipindi cha kwanza kabla ya kukamilisha hat-trick yake kwa mkwaju wa penalti katika dakika za mwisho za mchezo, uliokuwa miongoni mwa mechi zenye mabao mengi zaidi kwenye mashindano hayo.
Licha ya kiwango chake bora, Saka alianza michezo miwili pekee katika Kombe la Dunia kabla ya kuonyesha ubora wake dhidi ya Ufaransa.
Kilichowashangaza wengi ni kwamba kocha Thomas Tuchel hakumpa hata dakika moja ya kucheza katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Argentina, uliomalizika kwa England kuondolewa baada ya kupoteza nafasi ya kutinga fainali.
Baada ya mchezo huo, wengi walidhani Saka alikuwa akisumbuliwa na majeraha, lakini nyota huyo amefichua kuwa alikuwa mzima kabisa na alikuwa tayari kucheza.
“Bila shaka ningependa kucheza zaidi, lakini sasa nimechelewa kuzungumzia hilo,” .
“Napenda kuzungumza kupitia kiwango changu uwanjani, na nimefanya hivyo. Sasa tuendelee mbele. Nilikuwa fiti,” amesema Saka.
Kauli hiyo imeongeza mjadala kuhusu uamuzi ya Tuchel, ambaye amekuwa akikosolewa vikali tangu England ilipoondolewa na Argentina. Mashabiki na wachambuzi wengi wamehoji mbinu zake za kuchezesha timu pamoja na mabadiliko aliyofanya, wakiamini yalichangia kufifisha ndoto za England kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia.