Michael Olise avunja rekodi ya Pele
Muktasari:
- Nyota huyo wa Bayern Munich ameonyesha kiwango cha juu kilichowavutia mashabiki duniani kote na kufanikiwa kuvunja rekodi iliyodumu kwa zaidi ya nusu karne.
MIAMI, MAREKANI: KOMBE hili la Dunia limekuwa la kipekee kwa kiungo mshambuliaji wa Ufaransa, Michael Olise.
Nyota huyo wa Bayern Munich ameonyesha kiwango cha juu kilichowavutia mashabiki duniani kote na kufanikiwa kuvunja rekodi iliyodumu kwa zaidi ya nusu karne.
Baada ya kutoa pasi mbili za mabao kwa Kylian Mbappe, Olise sasa amefikisha jumla ya pasi saba za mabao (asisti) katika Kombe la Dunia la 2026, na hivyo kumpiku gwiji wa Brazil, Pele, aliyetoa pasi sita za mabao kwenye Kombe la Dunia la mwaka 1970 nchini Mexico.
Rekodi hiyo inamfanya Olise kuwa mchezaji mwenye pasi nyingi zaidi za mabao katika shindano mmoja wa Kombe la Dunia katika historia ya mashindano hayo.
Bado ana nafasi ya kuvunja rekodi nyingine
Licha ya mafanikio hayo, Olise bado yuko nyuma kwa pasi tano za mabao kufikia rekodi ya muda wote inayoshikiliwa na Lionel Messi. Endapo atacheza Kombe la Dunia la 2030, akiwa na umri wa miaka 28 pekee, atakuwa na nafasi nzuri ya kuifikia au hata kuivunja rekodi hiyo.
Katika mashindano haya, Olise amekuwa mhimili wa ubunifu wa Ufaransa, akitengeneza nafasi nyingi za mabao na kuonyesha ushirikiano wa hali ya juu na Mbappe, hasa kwa uwezo wake wa kumtafuta mshambuliaji huyo ndani ya eneo la hatari.
Kutokana na mustakabali wa Olise kuendelea kuzua gumzo kwenye soko la usajili, kiwango chake kimewafanya mashabiki wa Real Madrid kuanza kuota siku ambayo angeweza kucheza sambamba na Mbappe wakiwa wamevaa jezi nyeupe ya miamba hiyo ya Hispania.