Man United yamtaka Son wa Spurs Old Trafford
Muktasari:
- Son hayupo kwenye kiwango kizuri sana huko Spurs msimu huu, lakini bado ameonyesha ubora mbele ya lango, akiwa amefunga mabao 10 na kuasisti mara 10 katika mechi 35 alizocheza kwenye michuano yote, ikiwamo mabao sita na asisti nane kwenye mechi 23 alizocheza Ligi Kuu England.
MANCHESTER United imeripotiwa kujiandaa kupeleka ofa ya maana kabisa huko Tottenham Hotspur kwa ajili ya kunasa huduma ya mshambuliaji wa Korea Kusini, Son Heung-min ili akakipige Old Trafford.
Son hayupo kwenye kiwango kizuri sana huko Spurs msimu huu, lakini bado ameonyesha ubora mbele ya lango, akiwa amefunga mabao 10 na kuasisti mara 10 katika mechi 35 alizocheza kwenye michuano yote, ikiwamo mabao sita na asisti nane kwenye mechi 23 alizocheza Ligi Kuu England.
Son, 32, alisaini mkataba wa mwaka mmoja Januari mwaka huu na sasa atakuwa katika kikosi cha Spurs hadi Juni 2026, lakini ripoti kwa mujibu wa Fichajes, Man United inaamini itafanikiwa kunasa saini yake kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Man United inaamini Son atakwenda kuwafungia mabao ya kutosha baada ya mkali huyo aliyedumu kwenye Ligi Kuu England kwa miaka 10, ametumikia Spurs kwenye mechi 443 za michuano yote, amefunga mabao 172 na asisti 94.
Christopher Nkunku
MSHAMBULIAJI wa Chelsea, Christopher Nkunku ameripotiwa kuwa kwenye rada za Bayern Munich wakipiga hesabu za kunasa saini yake kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Kinachoripotiwa ni Bayern imepanga kupiga bei mastaa kibao ili kupata pesa za kusajili washambuliaji wawili kwenye dirisha hili huku Nkunku akitajwa kuwa mmoja wao. Fowadi mwingine anayefikiriwa ni winga wa Borussia Dortmund, Jamie Gittens.
Andrea Cambiaso
MANCHESTER City imeripotiwa kuweka nguvu kwenye mchakato wa kusajili beki wa pembeni kwenye dirisha lijalo na kwenye hilo mambo yanaweza kuangukia kwa mkali wa Juventus, Andrea Cambiaso. Man City ilimtoa beki wa kulia, Kyle Walker kwenda kwa mkopo AC Milan kwenye dirisha la Januari na mpango wao ulikuwa kumbadili na Cambiaso, lakini ilishindwa kukamilisha dili hilo na sasa inasubiri mwishoni mwa msimu ipambane kupata saini yake.
Adam Wharton
MANCHESTER United imeripotiwa kuwa kwenye mchakato wa kunasa huduma ya kiungo wa kati wa Crystal Palace, Adam Wharton dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Wharton, 21, alijiunga na Palace akitokea Blackburn Rovers mwanzoni mwa 2024 na amekuwa na kiwango bora sana jambo linalofanya timu kibao kuanza kufukuzia huduma yake, ikiwamo Man United ambao wamelenga kujiimarisha eneo la kati ya uwanja.
Johan Bakayoko
PSV Eindhoven imefichua itahitaji pesa nyingi sana ili ishawishike kumpiga bei staa wao, Johan Bakayoko dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Mshambuliaji huyo wa Ubelgiji anajiandaa kuachana na PSV mwishoni mwa msimu huu. Uhamisho wa kwenda England ni kitu kinachotarajia kutokea kutokana na Newcastle, Liverpool na Tottenham zinakuhitaji huduma yake na klabu yake ikifichua itamuuza kwa Euro 40 milioni.
Frenkie de Jong
ARSENAL imeripotiwa kumfuatilia kwa karibu kiungo wa Barcelona, Frenkie de Jong ikihitaji huduma yake kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Kinachoelezwa ni Arsenal itahitaji kiungo mpya wa kuongezeka kwenye kikosi chao na sasa wanamtazama Mdachi De Jong, licha ya kubainishwa kiungo wa Real Sociedad, Martin Zubimendi kuwa kwenye mipango yao.
Jack Grealish
NEWCASTLE United imeripotiwa kuwa na mpango wa kwenda kuvamia Manchester City kunasa huduma ya kiungo mshambuliaji, Jack Grealish. Grealish amekuwa na wakati mgumu Etihad na sasa Newcastle wanahitaji saini yake ili akakipige huko St James’ Park mwishoni mwa msimu huu. Man City ipo tayari kupokea ofa zinazomhusu.
Angel Gomes
NEWCASTLE United na Tottenham Hotspur zinatarajia kuingia vitani kumuwania mshambuliaji wa Lille, Angel Gomes, ambaye atakuwa huru mwishoni mwa msimu huu. Mkataba wa kiungo huyo mshambuliaji utafika tamati Juni na jambo hilo limezifanya Newcastle na Spurs kupambana kumrudisha Ligi Kuu England.