Man United yamkodishia Pochettino ndege binafsi
Muktasari:
- Kocha huyo mwenye umri wa miaka 54, atazungumza na waandishi wa habari na kuwaaga wachezaji wake kabla ya kupanda ndege binafsi iliyoandaliwa na mabosi wa United.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imepeleka ndege binafsi kwa ajili ya kumchukua kocha mpya Mauricio Pochettino moja kwa moja kutoka Marekani kwenda England, ili aanze majukumu yake mapya ndani ya klabu hiyo kabla ya mchezo mkubwa dhidi ya Liverpool.
Pochettino anatarajiwa kuwasili Manchester Jumatano asubuhi baada ya kumaliza mchezo wake wa mwisho akiwa kocha wa timu ya taifa ya Marekani dhidi ya Haiti, utakaochezwa Cincinnati saa sita usiku kwa saa za Uingereza.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 54, atazungumza na waandishi wa habari na kuwaaga wachezaji wake kabla ya kupanda ndege binafsi iliyoandaliwa na mabosi wa United.
Mpango huo unalenga kuhakikisha anapata muda wa kupumzika ndani ya ndege kabla ya kuanza kazi mara moja katika kituo cha mazoezi cha klabu hiyo, Carrington.
Pochettino hatakuwa peke yake katika safari hiyo, kwani ataambatana na kocha wa kikosi cha kwanza Miguel D'Agostino, mkufunzi wa nguvu na mazoezi Silvia Tuya pamoja na mchambuzi Alec Scott.
Wakati huohuo, wasaidizi wengine watatu wa benchi lake la ufundi tayari wamewasili Manchester tangu mwishoni mwa wiki, baada ya Marekani kuichapa Haiti mabao 6-0 katika mchezo wa kwanza wa hatua hiyo mjini Miami.
Wasaidizi hao ni Jesus Perez, kocha wa makipa Toni Jimenez pamoja na mwanawe Pochettino, Sebastiano Pochettino, ambaye pia ni mkufunzi wa viungo na mazoezi ya mwili.
Kuwasili kwa sehemu kubwa ya benchi la ufundi mapema kunatajwa kuwa hatua muhimu katika maandalizi ya mchezo wake wa kwanza dhidi ya Liverpool utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Anfield.
Huo ni mchezo mkubwa kwa United, hasa ikizingatiwa kuwa timu hiyo imekuwa ikipitia kipindi kigumu na kujikuta katika eneo la kushuka daraja.
Pochettino anatarajiwa kuanza kukutana na wachezaji kadiri wanavyorejea kutoka kwenye majukumu ya timu zao za taifa, huku akitarajiwa pia kuzungumza na vyombo vya habari vya klabu kabla ya mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari Ijumaa mchana.
Akizungumzia maandalizi hayo kabla ya mchezo wa marudiano dhidi ya Haiti, Pochettino amesema baadhi ya wasaidizi wake wataambatana naye baada ya kumaliza majukumu ya Marekani.
"Nitakuwa na Miguel, Silvia na Alec, ambao baadaye wataungana nami Manchester," amesema.
Aliendelea kueleza kuwa wasaidizi wengine tayari walikuwa wamewasili England.
"Swali linalofuata ni Jesus, Toni na Sebastiano wako wapi? Wao wametutangulia. Baada ya mchezo wa Miami, walisafiri kwenda Manchester na tayari wapo huko. Huo ndio ulikuwa mpango tulipokubaliana na Manchester United pamoja na timu ya taifa ya Marekani," amesema.
Pochettino ameongeza kuwa maandalizi hayo ni muhimu kwa sababu mara tu watakapowasili, kazi itaanza bila kupoteza muda.
"Jumatano tutakapowasili, hakutakuwa na nafasi ya kusimama. Tutaanza kazi na kisha michezo itafuata," amesema.
Kwa sasa macho yote ya mashabiki wa Manchester United yanaelekezwa kwa Pochettino, wakisubiri kuona kama ataweza kuifufua timu hiyo na kuiondoa kwenye wakati mgumu kabla ya kukutana na mahasimu wao Liverpool.