Sowah katika mtego wa rekodi Singida Black Stars
Muktasari:
- Sowah alijiunga na Singida Januari 17, 2025 akitokea Al-Nasr ya Libya, alionyesha kiwango cha juu msimu wa 2024-2025 kwa kufunga mabao 13 kwenye ligi, kisha 2025-2026 akatua Simba alipomaliza na mabao matatu.
BAADA ya mshambuliaji wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah kufikia mabao matatu katika ligi aliyomaliza nayo msimu wa 2025-2026 akiwa na Simba, ana mtihani wa kuvunja rekodi yake mwenyewe aliyoiandika kwa mara ya kwanza akicheza timu hiyo.
Mabao anayomiliki Sowah kwa sasa kafunga dhidi ya Fountain Gate, Kagera Sugar na Polisi Tanzania ambapo timu hiyo imecheza mechi 10, imebakiza 20 anazoweza kuzitumia kuyafikia mabao 13 au kuvunja rekodi hiyo aliyoiweka 2024-2025.
Sowah alijiunga na Singida Januari 17, 2025 akitokea Al-Nasr ya Libya, alionyesha kiwango cha juu msimu wa 2024-2025 kwa kufunga mabao 13 kwenye ligi, kisha 2025-2026 akatua Simba alipomaliza na mabao matatu.
Staa wa zamani wa Yanga na Singida United, Kipanya Malapa, alimzungumzia Sowah kuwa ni fundi wa kufunga, hivyo kazi imebaki kwake kuwa na muendelezo na alichokianza.
“Ni mshambuliaji mzuri, kwani alilionyesha hilo katika msimu wake wa kwanza akijiunga na Singida usajili wa dirisha dogo na aliweza kufunga mabao 13, ndiyo maana nasema ni maamuzi yake mwenyewe kufunga zaidi ya hayo au kumaliza msimu akiwa na mabao machache,” amesema Kipanya.
Mwingine aliyemzungumzia ni staa wa zamani wa Azam FC na Taifa Stars, Said Morad, amesema: “Sowah ni mshambuliaji mzuri, kama hatakuwa na changamoto yoyote anaweza akawa anatajwa kwenye tano bora ya wafungaji wa mabao mengi.”
Kwa upande wa kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni amesema: “Muendelezo wa anachofanya mchezaji ni nidhamu na kujituma, mfano mzuri Mbwana Samatta muda mwingi amecheza nje, kutokana na nidhamu na kujua anahitaji nini katika soka, hivyo kwenye mpira wa miguu lolote linawezekana.”