Msimu huu EPL ni wa mabao kipindi cha pili?
Muktasari:
- Licha ya Chelsea kuwa na ufanisi mkubwa katika dakika 15 za mwanzo wa mechi, imefunga na kufungwa mabao mengi zaidi katika kipindi cha pili kuliko kipindi cha kwanza. Huo ni mwenendo uliojitokeza katika timu mbalimbali za Ligi Kuu England baada ya raundi 10 za msimu huu.
LONDON, ENGLAND: MSIMU huu kumekuwa na rekodi ya uwiano mkubwa wa mabao yanayofungwa katika kipindi cha pili cha mechi za Ligi Kuu England (EPL). Hata hivyo, baadhi ya timu zimeenda kinyume na mwenendo huo. Je, timu zimekuwa zikifunga na kufungwa mabao katika vipindi gani vya mechi?
Kabla ya kalenda ya michuano ya Fifa inayoendelea Manchester United walijikuta wakifungwa mabao 2-0 ndani ya dakika tatu na sekunde 40 dhidi ya Aston Villa. Huo ulikuwa mwanzo wa kushangaza katika mchezo uliojaa matukio mengi, na ndiyo mara ya mapema zaidi kwa United kujikuta wakifungwa mabao mawili katika mchezo wowote wa Ligi Kuu England.
Kumekuwa na sababu nyingi za kuikosoa Man United kutokana na ubora wa uchezaji msimu huu, lakini kufungwa mabao ya mapema halikuwa mojawapo ya matatizo yao makubwa.
Kabla ya kukutana na Villa, mara ya mapema zaidi kwa United kuruhusu bao katika mchezo wa Ligi Kuu England msimu huu ilikuwa katika mechi ya ufunguzi wakati Semi Ajayi alipoiweka Hull City mbele kwa bao 1-0 dakika ya 17. Kabla ya mechi za Fifa kulikuwa na matukio 31 ambayo timu za EPL zilifungwa mabao ya kwanza mapema zaidi ya muda ambao United wamefungwa msimu huu.
Hata baada ya sare ya mabao 4-4 iliyopatikana Old Trafford, bado kuna timu tano zilizofungwa mabao mengi zaidi ya Man United ndani ya dakika 15 za mwanzo wa mechi. Ipswich Town (6) na Crystal Palace (5), ndizo timu zilizoathirika zaidi, huku Manchester City ikiwa imefungwa mabao manne na kufunga moja katika dakika 15 za mwanzo wa michezo ya Ligi Kuu England msimu huu.
Chelsea ndiyo timu hatari zaidi ndani ya dakika 15 za mwanzo wa mechi msimu huu ikiwa imefunga mabao saba na haijaruhusu bao lolote katika kipindi hicho kwenye michezo 10 ya kwanza.
Tayari imefikia zaidi ya theluthi moja ya rekodi ya mabao mengi zaidi yaliyofungwa na timu ndani ya dakika 15 za mwanzo wa mechi katika msimu mmoja wa ligi hiyo ambayo ni 19 yaliyofungwa na Man City 2018/19. Hata hivyo, ni muhimu kutambua kuwa Chelsea haijafunga bao ndani ya dakika 15 za mwanzo tangu ilipocheza na Bournemouth katika raundi ya sita.
Licha ya Chelsea kuwa na ufanisi mkubwa katika dakika 15 za mwanzo wa mechi, imefunga na kufungwa mabao mengi zaidi katika kipindi cha pili kuliko kipindi cha kwanza. Huo ni mwenendo uliojitokeza katika timu mbalimbali za Ligi Kuu England baada ya raundi 10 za msimu huu.
TWENDE SAWA
Kwa jumla, mabao 112 pekee kati ya 273 yaliyofungwa msimu huu yamepatikana kabla ya mapumziko. Uwiano huo wa asilimia 41 ndio mdogo zaidi kuwahi kushuhudiwa katika msimu wowote wa Ligi Kuu England. Kuna timu tatu ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kushusha wastani huo kufikia kiwango cha chini zaidi kuwahi kurekodiwa; Everton, Tottenham Hotspur na Coventry City.
Michezo inayohusisha Everton imeshuhudia idadi ndogo zaidi ya mabao yaliyofungwa kabla ya mapumziko (4), ikiwa na uwiano wa asilimia 18.2.
Rekodi ya uwiano mdogo zaidi wa mabao ya kipindi cha kwanza katika michezo inayohusisha timu fulani kwa msimu mzima wa Ligi Kuu England inashikiliwa na Man City ambayo ilikuwa na asilimia 29.5 msimu wa 2011/12.
Everton imefungwa asilimia 80 ya mabao na kufunga asilimia 83 ya mabao yake yote katika kipindi cha pili. Kama ilivyo kwa Everton, Tottenham Hotspur pia imefunga mabao mawili pekee katika kipindi cha kwanza msimu huu, ikiwa imetupia mengi zaidi dakika 15 za mwisho za michezo (6) kuliko ilivyofunga kabla ya dakika ya 75 msimu wa 2026/27.
Nayo Coventry imekuwa miongoni mwa timu hatari zaidi katika dakika 15 za mwanzo wa kipindi cha pili. Ni Man City pekee (6), ndiyo iliyofunga mabao mengi zaidi kuliko Coventry City (5) kati ya dakika ya 46 na 60. Hata hivyo, Coventry City wamekuwa na changamoto katika safu ya ulinzi kipindi cha pili, wakiruhusu mabao 14 baada ya mapumziko, idadi kubwa zaidi katika ligi.
Upande mwingine wa mwenendo huo ni Brighton ambao wamekuwa na kiwango bora msimu huu wakifunga mabao 14 katika kipindi cha kwanza cha mechi za ligi hiyo, idadi kubwa zaidi kuliko timu nyingine yoyote.
Wakiwa wamefungwa mabao sita zaidi kabla ya mapumziko, Brighton ndiyo pekee msimu huu ambao wana mabao mengi zaidi kipindi cha kwanza kuliko kile cha pili (asilimia 60.6 -mabao 20 kati ya 33).
Pia, Brighton ndiyo timu pekee iliyofunga mabao mengi zaidi kipindi cha kwanza msimu huu kuliko Bournemouth (10).
Bournemouth imefunga asilimia kubwa zaidi ya mabao yake katika kipindi cha kwanza, ikiwa na asilimia 63 na kama mechi zingekuwa zinaishia wakati wa mapumziko msimu huu ingekuwa inaongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi nne ikiwa na alama 23, baada ya kushinda michezo saba, sare mbili na kupoteza mmoja.
Bahati mbaya kwa Bournemouth, Brentford pekee (11) ndiyo iliyopoteza pointi nyingi baada ya kuongoza kuliko wao (8) msimu huu. Hali hiyo imewafanya washindwe kudumisha kiwango cha uongozi wa msimamo katika dakika 90 za michezo yao.
UNAISHIJE KIBINGWA?
Bila shaka, katika soka mara nyingi siyo namna unavyoanza mchezo inayokuwa na athari kubwa katika nafasi unayomalizia kwenye msimamo wa ligi, bali ni namna unavyouhitimisha. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Arsenal, wameanza vizuri safari ya kutafuta kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa misimu miwili mfululizo, jambo ambalo halijafanywa tangu 1935.
Arsenal wanaoongoza msimamo kwa tofauti ya pointi tano wamefungwa mabao matano msimu huu, idadi ndogo zaidi katika ligi, na wanaonekana kuwa katika nafasi ya kuwania kuvunja rekodi ya muda wote ya kufungwa machache zaidi katika msimu mmoja wa ligi hiyo.
Rekodi ya sasa inashikiliwa na Chelsea iliyofungwa mabao 15 msimu wa 2004/05 ilipokuwa ikiruhusu wastani wa bao 0.39 kwa kila mchezo. Kwa sasa Arsenal ina wastani wa mabao 0.50 kwa kila mchezo, ikimaanisha kwamba inahitaji kuruhusu mabao yasiyozidi 11 katika michezo 28 iliyobaki ili kuvunja rekodi hiyo.
The Gunners bado hawajafungwa bao lolote baada ya dakika ya 57 katika mchezo wowote wa Ligi Kuu England msimu huu. Kwa kuzingatia hali hiyo, wanaweza pia kuwania kuvunja rekodi ya kufungwa mabao machache zaidi katika dakika 30 za mwisho za michezo katika msimu mmoja, inayoshikiliwa na Chelsea, iliyofungwa mabao manne katika misimu ya 2004/05 na 2005/06.
Rekodi ya Brighton katika safu ya ulinzi kipindi cha pili pia inastahili kuangaziwa, kwani kikosi hicho cha Fabian Hurzeler kimefungwa bao moja pekee baada ya mapumziko msimu wa 2026/27.
Rekodi ya Ligi Kuu England ya kufungwa mabao machache zaidi katika kipindi cha pili kwa msimu mmoja pia inashikiliwa na Chelsea, ambayo iliruhusu mabao saba pekee katika misimu yake ya ubingwa ya 2004/05 na 2005/06 chini ya kocha Jose Mourinho.
Kwa hali ilivyo baada ya mechi 10 za msimu huu, Brighton wanaonekana kuwa wapinzani wakubwa zaidi wa Arsenal katika mbio za ubingwa wa ligi hiyo, jambo ambalo pia ni la kushangaza zaidi. Ikiwa mwenendo wa jumla wa ligi wa kufungwa mabao mengi zaidi katika kipindi cha pili utaendelea, huenda hatimaye ubingwa ukaamuliwa na timu zitakazoweza kudumisha kiwango chao katika dakika za mwisho za michezo.