Man United yachapika Premier
Muktasari:
- Man United imepoteza mechi ya tatu kati ya sita za kwanza za ligi msimu huu baada ya kichapo kutoka kwa Brentford, na imani ambayo mabosi wa timu hiyo walikuwa nayo kwa Amorim imepungua ambapo sasa lolote linaweza kutokea.
MANCHESTER, ENGLAND: BAADA ya kupokea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Brentford ugenini katika mchezo wa mapema uliopigwa leo Jumamosi, kocha wa Manchester United anadaiwa kuwa katika hali mbaya na mabosi wa timu hiyo wanatarajiwa kukutana kujadili hali ya timu.
Man United imepoteza mechi ya tatu kati ya sita za kwanza za ligi msimu huu baada ya kichapo kutoka kwa Brentford, na imani ambayo mabosi wa timu hiyo walikuwa nayo kwa Amorim imepungua ambapo sasa lolote linaweza kutokea.
Brentford ilipata bao la kwanza kupitia kwa Igor Thiago dakika ya nane ambaye pia alifunga la pili dakika ya 20.
Man United ilipata bao la kufuatia machozi dakika ya 26 kupitia kwa Benjamin Sesko ambaye lilikuwa ni bao lake la kwanza katika Ligi Kuu England tangu ajiunge na timu hiyo dirisha lililopita.
Mashetani Wekundu walikuwa na nafasi ya kusawazisha baada ya mshambuliaji Bryan Mbeumo kuangushwa katika eneo la hatari na mwamuzi kuizawadia penalti. Hata hivyo, nahodha Bruno Fernandez alipiga mpira ulioishia mikononi mwa kipa wa Brentford, Caoimhín Kelleher na kuokolewa.
Dakika ya 90+5, Mathias Jensen aliimaliza kazi kwa kufunga bao la tatu lililowavunja nguvu Manchester United.
Wiki iliyopita, bosi Sir Jim Ratcliffe aliwasili kwa helikopta kwenye uwanja wa mazoezi wa Man United ambako alionekana akizungumza na Amorim kwa muda, kisha baadaye akawa na kikao na kocha huyo pamoja na viongozi wengine wa klabu.
Amorim alipoulizwa kuhusu kilichojadiliwa alisema kilikuwa ni kikao cha kawaida kuhusu maendeleo ya timu, ingawa taarifa za ndani zilidai tajiri alimwambia kuwa ana imani naye, lakini anataka kuona timu ikiwa na mabadiliko.
Lejendari wa Manchester United, Rio Ferdinand amempa ushauri Amorim akimwambia ili atoboe anahitaji nguvu ya kinda Kobbie Mainoo katika eneo la kiungo kwani kuna upungufu.
Beki huyo wa zamani wa kimataifa wa England anaamini Mainoo (20), anaweza kulifanya eneo la kati kuwa na uwiano na kuifanya timu hiyo itembee tofauti na ilivyo sasa, akionya pia kama staa huyo hatapewa nafasi kuna uwezekano mkubwa Januari, 2026 akaomba kuondoka na hawatakuwa na haki ya kumzuia kama alivyofanya dirisha lililopita.
Mashabiki wengi wamekuwa wakilalamika mbinu za Amorim wakieleza wachezaji wamekuwa wakicheza kwa uwezo binafsi na kwamba mipango ya kocha haionekani.
REKODI
Kichapo hicho kimeifanya Man United kubaki na pointi saba ilizopata baada ya kushinda mechi mbili na sare moja, huku ikipoteza tatu kati ya sita za msimu huu, huku Brentford ikifikisha pointi saba ikishinda mechi mbili, sare moja na kufungwa tatu katika mechi hizo.
Hiyo ilikuwa ni mechi ya 200 kwa Amorim kusimama katika benchi kama kocha na amekuwa na rekodi mbaya zaidi akiwa na Man United kuliko ilivyokuwa akiwa na Sporting Lisbon, ambapo ameiongoza Man United katika mechi 33 za Ligi Kuu England akifungwa 17 wakati katika Ligi Kuu Ureno kwenye mechi 167 alipoteza mechi 14.
Thiago ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili kufunga mabao mawili ya mapema zaidi dhidi ya Man United katika mechi moja baada ya Alexis Sanchez ambaye alifanya hivyo akiwa na Arsenal Oktoba 2015 ndani ya dakika 19.
Katika penalti saba ambazo kipa wa Brentford, Caoimhín Kelleher, amepigiwa akiwa na Liverpool pamoja na timu yake ya sasa amefanikiwa kuokoa nne ambazo ni sawa na asilimia 57.