Bellingham, Ashlyn mapenzi motomoto
Muktasari:
- Mrembo huyo raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 28 amekuwa kwenye uhusiano na kiungo huyo wa Real Madrid tangu mwaka 2024 na sasa ameonekana mara kwa mara akimshangilia katika mechi za England.
MIAMI, MAREKANI: KWA miaka mingi, imekuwa ikijulikana kuwa mama wa Jude Bellingham, Denise, ndiye shabiki wake mkubwa na mtu aliyekuwa karibu naye tangu alipoanza safari yake ya soka.
Lakini katika Kombe la Dunia 2026, sura nyingine imekuwa ikivuta macho ya mashabiki majukwaani naye ni mpenzi wake, Ashlyn Castro.
Mrembo huyo raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 28 amekuwa kwenye uhusiano na kiungo huyo wa Real Madrid tangu mwaka 2024 na sasa ameonekana mara kwa mara akimshangilia katika mechi za England.
Ingawa wawili hao hawajazungumzia sana hadharani kuhusu mahusiano yao, Bellingham aliwahi kumuita Ashlyn “my love”, huku mwanadada huyo akimwelezea staa huyo wa England kama:”Mtu mwenye kujali, mwenye moyo mwema, anayefanya kazi kwa bidii na mtu wa kipekee zaidi kuwahi kumfahamu.”
MREMBO MWENYE MASHABIKI ZAIDI YA MILIONI MOJA
Ashlyn ni mwanamitindo na mshawishi wa mitandao ya kijamii (influencer) mwenye zaidi ya wafuasi milioni moja kupitia Instagram na TikTok.
Amefanya kazi na kampuni mbalimbali kubwa za mitindo na urembo, ikiwemo Clarins, lakini licha ya umaarufu huo hupendelea kuweka maisha yake binafsi mbali na macho ya umma.
Kurasa zake za mitandao zimejaa maudhui ya mitindo, urembo na safari mbalimbali.
MAPENZI YAO HAYAFICHIKI
Mwaka jana wawili hao walinaswa wakifurahia mapumziko ndani ya boti ya kifahari huko Sardinia, Italia, wakionekana wenye furaha kubwa.
Hata hivyo, Ashlyn huendelea kutoa ishara ndogo zinazoonyesha mapenzi yake kwa Bellingham.
Akiwa Miami kwa ajili ya Kombe la Dunia, aliposti picha na kuandika:
“Sunshine state.”
Bellingham hakusita kujibu kwa kuweka emoji za macho ya mapenzi, huku staa wa Love Island, Uma Jammeh, aliyekuwa rafiki wa Ashlyn, akimuita “Princess.”
AMEJENGA UKARIBU NA WAZAZI WA BELLINGHAM
Ashlyn pia ameonekana kujizolea nafasi maalumu ndani ya familia ya Bellingham.
Mwaka 2025 alipigwa picha akiwa ameketi pamoja na wazazi wa Jude katika Uwanja wa Santiago Bernabeu wakimtazama nyota huyo akiitumikia Real Madrid.
Tangu wakati huo amekuwa mgeni wa kawaida kwenye mechi za Real Madrid na England, huku mapema mwaka huu akionekana tena akiwa amekaa karibu na mama yake Jude katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia.
WALIVYOANZA MAPENZI
Tetesi za wawili hao zilianza kushika kasi mwishoni mwa mwaka 2024 baada ya mashabiki kuwaona wakipeana maoni kwenye machapisho yao ya Instagram.
Mwezi Januari 2025 walipigwa picha wakila chakula cha mchana pamoja jijini Madrid baada ya Real Madrid kuifunga RB Salzburg katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wiki chache baadaye Ashlyn alionekana katika eneo maalumu la wageni wa heshima akiwa na familia ya Bellingham wakati wa mchezo dhidi ya Girona.