Man United wanyimwa penalti, VAR yatoa ufafanuzi
Muktasari:
- Tukio hilo lilitokea dakika ya 86 baada ya Lisandro Martinez kuugusa mpira na kuuelekeza kwa Bassey, ambapo marudio ya video yalionyesha mpira ukigusa mkono wa beki huyo wa Fulham.
LONDON, England: Manchester United ilinyimwa penalti katika dakika za mwisho za mchezo dhidi ya Fulham, licha ya mpira kugonga mkono wa beki Calvin Bassey, huku waamuzi wakiamua kuendelea na mchezo katika sare ya mabao 1-1 iliyopatikana Jumapili.
Tukio hilo lilitokea dakika ya 86 baada ya Lisandro Martinez kuugusa mpira na kuuelekeza kwa Bassey, ambapo marudio ya video yalionyesha mpira ukigusa mkono wa beki huyo wa Fulham.
Wakati huo, United ilikuwa nyuma kwa bao moja na ikijitahidi kusaka bao la kusawazisha. Hata hivyo, mwamuzi Peter Bankes aliamuru mchezo uendelee, uamuzi ambao uliungwa mkono na waamuzi wenzake.
Baadaye, Ligi Kuu England ilitoa ufafanuzi kupitia kituo chake rasmi cha Match Centre kwenye mtandao wa X, ikiweka wazi mazungumzo kati ya Bankes, mwamuzi msaidizi Dan Cook na mwamuzi wa VAR, Nick Hopton.
Taarifa hiyo ilisomeka: “Uamuzi wa mwamuzi kutotoa penalti kwa Manchester United kutokana na uwezekano wa kosa la kucheza mpira kwa mkono na Bassey ulikaguliwa na kuthibitishwa na VAR.”
Baada ya mpira kugonga mkono wa Bassey, Cook alisema: “Uko karibu na mwili wake na umegonga, lakini mkono wake uko karibu na mwili.”
Bankes akajibu: “Uamuzi wa uwanjani ni kuendelea na mchezo.”
Hopton naye akaongeza: “Mikono iko karibu na mwili wake. Kama ilivyoonekana, tunathibitisha uamuzi wa uwanjani wa kuendelea na mchezo, kama ulivyoelezwa.”
United ilikuwa ikikabiliwa na siku ngumu baada ya Martinez kujifunga bao la kuchekesha muda mfupi baada ya saa moja ya mchezo, huku kipa Senne Lammens, pia akionekana kuchangia tukio hilo.
Mashabiki wa United walizidi kukasirika baada ya ombi la penalti kufutwa, lakini timu hiyo iliweza kuondoka na pointi moja baada ya shuti la Matheus Cunha dakika ya 89 kugonga mchezaji David Affengruber na kuingia wavuni.
Kocha Michael Carrick anakabiliwa na ukosoaji mkali kuhusu kiwango cha timu yake, akiwamo aliyekuwa mwenzake wa zamani, Gary Neville, kutokana na ukosefu wa kasi na haraka katika mchezo huo.
Hata hivyo, Carrick alisisitiza kuwa ameridhishwa na juhudi za wachezaji wake kabla ya mapumziko ya kimataifa, ambayo yatampa nafasi muhimu ya kufanya marekebisho ndani ya kikosi.
“Sikufikiri tulionekana wazembe. Soka ni mchezo mgumu. Tulidhibiti sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza na tukacheza soka zuri leo. Kuna vipindi ambavyo mambo hayaendi kwa upande wako,” alisema Carrick.