Man United hapajatulia, Amorim ana kazi nyingine
Muktasari:
- Wakati Sir Jim Ratcliffe na wenzake walipofanya uamuzi wa kumfuta kazi Erik ten Hag mwishoni mwa Oktoba 2024, mashabiki wa United walitarajia matokeo bora na mabadiliko makubwa.
MANCHESTER, ENGLAND: KLABU ya Manchester United sasa ina alama nne pungufu ikilinganishwa na ilivyokuwa msimu uliopita baada ya kucheza mechi zilezile saba za mwanzo, kwa mujibu wa jedwali la kulinganisha lililotolewa na Opta Sport.
Wakati Sir Jim Ratcliffe na wenzake walipofanya uamuzi wa kumfuta kazi Erik ten Hag mwishoni mwa Oktoba 2024, mashabiki wa United walitarajia matokeo bora na mabadiliko makubwa.
Kocha huyo wa Kiholanzi alikuwa amepitia kipindi kigumu mwanzoni mwa msimu, ambapo timu yake ilipoteza mechi tatu nyumbani ikiwemo vichapo vya 0–3 dhidi ya Tottenham Hotspur na Liverpool, kisha kufungwa 2–1 na West Ham, hali iliyomfanya apoteze kazi.
Hata hivyo, karibu mwaka mmoja baadaye, hali haijaonyesha mabadiliko yoyote makubwa.
Uteuzi wa Ruben Amorim ulipokewa kwa shangwe kubwa. Mashabiki walimwona kama meneja kijana, mwenye falsafa ya kisasa, aliyekuwa ameiwezesha Sporting Lisbon kushinda Ligi Kuu ya Ureno (Primeira Liga) kwa mara ya kwanza baada ya miaka takriban 20.
Lakini kocha huyo mwenye umri wa miaka 40 ameshinda mechi 10 tu kati ya 34 za Ligi Kuu England akiwa kocha wa Manchester United — na nusu ya ushindi huo umekuja dhidi ya timu mpya zilizopandishwa daraja. Kwa takribani mwaka mzima, hajawahi kushinda mechi mbili mfululizo za ligi.
Mashabiki walitarajia ujio wa wachezaji kama Benjamin Sesko, Matheus Cunha, Bryan Mbeumo na Senne Lammens, pamoja na maandalizi ya msimu mapya, ungeleta mafanikio katika mfumo wake wa 3-4-3.
Lakini kwa mujibu wa takwimu za Opta Sport, United sasa iko alama nne nyuma ya walipokuwa msimu uliopita baada ya mechi hizo hizo.
Msimu wa 2024–25, katika mechi zao dhidi ya timu kama Man City, Arsenal, na Chelsea, walipata alama 14, ilhali msimu huu wameshinda alama 10 pekee.
Kinyume chake, timu kama Bournemouth ya Andoni Iraola na Tottenham Hotspur chini ya Thomas Frank zimeonyesha maendeleo makubwa. Wakati huo huo, Manchester City ya Pep Guardiola imekuwa alama sita mbele ikilinganishwa na msimu uliopita.
Timu kama Aston Villa, Brighton, na Wolves zinashika mkia kwenye jedwali hilo la kulinganisha kutokana na mwanzo mbaya. Timu ya Brighton chini ya Fabian Hurzeler iko alama tisa nyuma ya walipokuwa msimu uliopita.
Hali hii inatia wasiwasi kwa mashabiki na bila shaka kwa wamiliki wa klabu, hasa tunapoingia kwenye kipindi hatari cha Oktoba na Novemba ambacho mara nyingi hujulikana kama “msimu wa kufukuzana makocha.”
Kumekuwa na uvumi kwamba Sir Jim Ratcliffe, mtu aliyemteua Amorim, anaweza kumfukuza kazi kabla hajamaliza mwaka mmoja tangu aingie Old Trafford.
Shinikizo dhidi ya Amorim liliongezeka baada ya timu yake kupoteza 3–1 dhidi ya Brentford wiki iliyopita, na mechi ya nyumbani dhidi ya Sunderland ikatajwa kuwa “ya kuokoa kazi.”
Mabao kutoka kwa Mason Mount na Benjamin Sesko yaliihakikishia United ushindi muhimu dhidi ya Black Cats, ushindi ulioweza kuokoa nafasi ya Amorim kwa muda.
Baada ya mechi, Mount alisema wachezaji wako “asilimia 100 nyuma ya kocha wao,” lakini Amorim aliwataka waonyeshe uaminifu huo kwa vitendo uwanjani.
Alisema: “Tunapaswa kuonyesha kwa matendo. Najua wanataka kufanya vizuri, najua hawataki kubadilisha makocha kila wakati. Lakini kama nilivyosema wiki hii, kuwa upande wa kocha ni kujitolea kikamilifu kila dakika.”
Akaongeza: “Mara nyingine tunaangalia timu yetu na tunajua tunaweza kufanya vizuri zaidi. Tunapaswa kuonyesha hayo uwanjani si tu nyumbani bali pia ugenini.”
“Hakuna mwendelezo kwenye timu yetu, iwe kabla au baada ya mapumziko. Inakatisha tamaa kuona hatuwezi kurudia kiwango tunachokionesha nyumbani tukiwa ugenini,” alisema.
Ushindi huo ulikuwa wa tatu mfululizo Old Trafford, ingawa mechi mbili zilizopita za nyumbani zilifuatwa na vipigo dhidi ya Manchester City na Brentford.
Baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa, Manchester United itasafiri kwenda Anfield kuvaana na Liverpool, mechi kubwa itakayothibitisha kama Amorim anaweza hatimaye kuanza kujenga mwendelezo wa mafanikio akiwa kocha wa klabu hiyo.