Man City yaituliza Arsenal, yatwaa ubingwa wa 9 Carabao Cup
Muktasari:
- Katika mchezo huo wa fainali uliopigwa kwenye dimba la kihistoria la Wembley, City wamethibitisha kwanini wao ni wafalme wa michuano hiyi kwa kutangazwa mabingwa rasmi wa msimu wa 2025/26.
WEMBLEY, LONDON: Manchester City imeendeleza ubabe wake katika michuano ya Carabao Cup (EFL) baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 2-0 dhidi ya Arsenal.
Katika mchezo huo wa fainali uliopigwa kwenye dimba la kihistoria la Wembley, City wamethibitisha kwanini wao ni wafalme wa michuano hiyi kwa kutangazwa mabingwa rasmi wa msimu wa 2025/26.
Ushindi huo unaufanya Manchester City sasa kuweka kabatini taji lake la 9 la Carabao Cup, rekodi inayozidi kuimarisha hadhi ya klabu hiyo katika ramani ya soka la Uingereza.
Dakika nne za maangamizi, Nico O’Reilly ang’ara
Licha ya mchezo kuanza kwa kasi na upinzani mkali kutoka kwa vijana wa Arsenal, kipindi cha pili kilikuwa cha neema kwa "The Citizens". Shujaa wa mchezo huo alikuwa kinda mwenye kipaji kikubwa, Nico O’Reilly, aliyewazidi ujanja mabeki wa Arsenal na kumpiku kipa Kepa Arrizabalaga.
O’Reilly alifungua milango ya furaha katika dakika ya 60. Kabla Arsenal hawajajipanga sawasawa, alirejea tena dakika ya 64 na kupachika bao la pili, akihitimisha karamu ya mabao ndani ya dakika nne pekee na kuwanyong’onyesha mashabiki wa "The Gunners".
Rekodi ya Dhahabu kwa Pep Guardiola
Ubingwa huu kwa kocha mkuu, Pep Guardiola unakuwa wa tano kwenye mashindano hayo akiwa na Manchester City tangu alipojiunga na klabu hiyo.
Mafanikio haya yanakuja baada ya mfululizo wa mataji aliyotwaa katika miaka ya: 2018, 2019, 2020, 2021, na 2026 (Leo)
Guardiola ameweza kujenga utamaduni wa ushindi ambao umekuwa mgumu kuvunjwa, huku akionyesha uwezo wa kuibua vipaji vipya kama O’Reilly vinavyoamua mechi kubwa.
Kwa upande wa Arsenal, kichapo hiki kinawaacha na maswali mengi kuhusu safu yao ya ulinzi iliyoshindwa kuhimili presha ndani ya kipindi kifupi cha kipindi cha pili.
Wakati jua likizama jijini London, rangi ya samawati (Sky Blue) ilitanda kote Wembley, huku mashabiki wa City wakishangilia mwanzo mzuri wa kuvuna mataji msimu huu licha ya kupoteza mashindano ya UEFACL 2025/26.