Madonna, Shakira, Bieber kutikisa mapumziko Kombe la Dunia
Muktasari:
- Mabilioni ya mashabiki duniani watakuwa wakishuhudia pambano hilo litakalochezwa Uwanja wa MetLife, huku nahodha wa timu itakayoshinda akilazimika kusubiri kwa muda mrefu zaidi kabla ya kuinua kombe kutokana na ratiba hiyo mpya ya burudani.
FAINALI ya Kombe la Dunia kati ya Argentina na Hispania itakuwa ya kipekee leo baada ya FIFA kuamua kwa mara ya kwanza katika historia kuanzisha burudani ya muziki wakati wa mapumziko ya kipindi cha kwanza (halftime show).
Mabilioni ya mashabiki duniani watakuwa wakishuhudia pambano hilo litakalochezwa Uwanja wa MetLife, huku nahodha wa timu itakayoshinda akilazimika kusubiri kwa muda mrefu zaidi kabla ya kuinua kombe kutokana na ratiba hiyo mpya ya burudani.
Nani watatumbuiza?
FIFA imempa jukumu mwimbaji wa Coldplay, Chris Martin, kusimamia maandalizi ya tamasha hilo. Miongoni mwa mastaa watakaopanda jukwaani ni Madonna, Shakira, Justin Bieber, Burna Boy, pamoja na kondakta maarufu kutoka Venezuela, Gustavo Dudamel.
Bendi ya Coldplay pia itatoa burudani ikishirikiana na PS22 Chorus, kundi la wanafunzi kutoka New York. Aidha, wahusika maarufu wa Sesame Street na The Muppets nao watakuwa sehemu ya onyesho hilo.
FIFA imesema tamasha hilo litakuwa la kwanza kuunganisha soka, muziki na ujumbe wa kijamii katika fainali ya Kombe la Dunia, huku likisaidia kampeni ya FIFA Global Citizen Education Fund inayolenga kukusanya dola 100 milioni kwa ajili ya kuboresha elimu na kutoa fursa za soka kwa watoto duniani.
Sherehe za kufunga pia zipo
Mbali na halftime show, kutakuwa pia na sherehe za kufunga mashindano zitakazowakutanisha mastaa mbalimbali akiwemo Post Malone, Tom Cruise, Nicole Scherzinger, Jennifer Hudson, Robbie Williams, Laura Pausini pamoja na mwanamitandao IShowSpeed.
FIFA imesema hafla hiyo itatoa heshima kwa mataifa yote 48 yaliyoshiriki mashindano hayo, huku jukumu maalumu la Tom Cruise likibaki kuwa siri.
Mapumziko yatachukua muda gani?
Ingawa onyesho lenyewe linatarajiwa kudumu dakika 11, taarifa mbalimbali zinaeleza kuwa mapumziko yote yanaweza kufikia dakika 20 au zaidi.
Sheria za soka zinataka mapumziko yasizidi dakika 15 isipokuwa kwa ruhusa ya mwamuzi, lakini FIFA inaonekana tayari imeandaa mpango maalumu kwa ajili ya fainali hiyo.
Katika fainali ya Kombe la Dunia la Klabu mwaka uliopita, mapumziko yalidumu karibu dakika 25 licha ya burudani kuchukua dakika 10 pekee.
Hali hiyo imezua wasiwasi kuhusu uwezekano wa wachezaji kupata majeraha kutokana na kukaa muda mrefu vyumbani pamoja na changamoto ya kujenga na kuvunja jukwaa ndani ya uwanja kabla ya mchezo kuendelea.
Maoni yamegawanyika
Rais wa FIFA, Gianni Infantino, amesema tamasha hilo litapeleka ujumbe wa umoja na matumaini kwa mabilioni ya watazamaji duniani.
"Tunataka kuunganisha soka, muziki na maadili ya pamoja katika tukio ambalo litakumbukwa hata baada ya filimbi ya mwisho," amesema Infantino.
Kwa upande wake, mtayarishaji mkuu wa tamasha hilo, Guy Carrington, amesema maandalizi yamechukua miezi kadhaa na kuahidi onyesho la kiwango cha juu.
Hata hivyo, si kila mtu ameridhishwa na uamuzi huo. Mwanamuziki Robert Smith wa bendi ya The Cure ameonyesha kupinga wazi wazo la halftime show, akitoa kauli kali dhidi ya mpango huo.
Kwa sasa macho ya dunia yataelekezwa MetLife Stadium, si tu kushuhudia bingwa mpya wa Kombe la Dunia, bali pia kuona kama jaribio la kwanza la FIFA kuleta burudani ya aina ya Super Bowl kwenye fainali ya soka litafanikiwa.