Mabosi PSG wanamtaka Lamine Yamal
Muktasari:
- Hilo ni kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa Ufaransa, Romain Molina, ambaye amekuwa akiandika pia habari zake kwenye The Guardian, New York Times na BBC.
PARIS, UFARANSA: MABOSI wa Paris Saint-Germain wameripotiwa kuwa na imani kwamba watamng'oa Lamine Yamal kutoka Barcelona.
Wakati staa huyo mwenye umri wa miaka 18 akizungumzia uwezekano wa kuwa mchezaji wa klabu moja katika maisha yake yote ya soka, wakurugenzi wa PSG wenyewe bado wana matumaini makubwa kwamba watanasa saini ya winga huyo wa Kihispaniola ili akacheze kwenye ligi ya Ufaransa.
Hilo ni kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa Ufaransa, Romain Molina, ambaye amekuwa akiandika pia habari zake kwenye The Guardian, New York Times na BBC.
Kampuni ya Qatar Sports Investments, inayomiliki klabu ya PSG, imebainisha dhamira yake ya kumsajili Yamal ili akacheze kwenye Ligue 1.
"Wanasema, 'Tunamtaka.' Imeamriwa huko Doha. Siku moja watamchukua bila ya kujali atagharimu," amesema Molina.
Yamal alisaini mkataba mpya huko Barcelona ambao utafika tamati 2031, huku kiwango kilichowekwa kwenye mkataba huo kwa timu itakayotaka kuvunja ni Euro 1 bilioni.