Prime
EXCLUSIVE: MO ashusha presha, aahidi kuvunja utawala wa Yanga
RAIS wa Heshima Simba, Mohammed Dewji (MO), amesema klabu hiyo imejipanga kurejesha heshima yake msimu huu 2026-2027 baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu mitano mfululizo.
Kauli ya Mo inakuja wakati watani zao wa jadi, Yanga SC chini ya Rais wake, Injinia Hersi Said imefanikiwa kutawala soka la Tanzania kwa kutwaa mataji 16, kati yake matano ya Ligi Kuu.
Mbali ya kutwaa ubingwa, pia Yanga iliweka rekodi ya kuifunga Simba mara sita mfululizo katika misimu ya hivi karibuni.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, MO Dewji alisema presha ya kuona Simba ikikosa mafanikio ndiyo iliyomshawishi kurejea kuiongoza klabu hiyo ili kuhakikisha mambo yanarudi kwenye mstari.
"Mimi niliingia rasmi Simba mwaka 2017 wakati mfumo wa bodi ulipoanza. Nilikuwa mwenyekiti wa bodi na katika kipindi hicho tulishinda ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo," alisema MO.
Alieleza kuwa, baadaye aliamua kuachia nafasi hiyo kwa sababu ya majukumu yake mengine, akiamini Simba ilihitaji kiongozi ambaye angekuwa karibu zaidi na shughuli za kila siku za klabu.
"Baada ya mimi kuondoka, kulikuwa na viongozi wengine walioiongoza klabu kwa takribani miaka mitatu, lakini mambo hayakwenda kama tulivyotarajia. Nilipata presha kubwa kutoka kwa wanachama na mashabiki waliotaka mabadiliko ya uongozi, nikaona ni lazima nirejee kusaidia kuweka mambo sawa," alisema tajiri huyo.
MO alisema Simba imekaribia mafanikio katika misimu miwili iliyopita, lakini dakika za mwisho wanapotea.
"Msimu wa 2024/25 tulifika fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini hatukufanikiwa kutwaa ubingwa. Vilevile tulipigania taji la Ligi Kuu hadi mchezo wa mwisho dhidi ya Yanga, lakini tukalikosa. Hiyo inaonyesha tupo karibu na mafanikio."
Kuhusu malalamiko ya kutotendewa haki kwenye mashindano ya ndani, MO alisema hilo ni jambo ambalo klabu imekuwa ikilizungumza mara kwa mara, lakini hakutaka kulipa uzito katika mahojiano hayo.
"Kuna mambo mengi ambayo tunaamini hayajawa ya haki kwetu kwenye mashindano ya ndani, lakini sitaki kuyazungumzia sana kwa sasa. Kilicho muhimu ni kwamba sisi kama Simba tumejipanga vizuri na lengo letu ni kurejesha heshima ya klabu kwa kufanya vizuri zaidi na kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu."
Akizungumzia maendeleo ya soka la Tanzania, MO alisema kiwango cha mchezo huo kinaendelea kupanda na kuwapongeza Watanzania kwa namna wanavyozipenda na kuzisimamia klabu zao.
"Ukiniuliza timu ninayoishabikia England, sina. Sijawahi kuishi Manchester wala sina uhusiano na mji huo, hivyo ushindi au kushindwa kwa timu za huko haunigusi. Ninayoihusudu na kuipenda ni Simba kwa sababu ni timu ya nyumbani, ya Dar es Salaam, na ndiyo timu yangu."
MO pia alizungumzia suala la mabadiliko ya makocha, akisema wakati mwingine uamuzi wa kuachana na kocha huwa hauepukiki pale matokeo yanapokuwa hayaridhishi, lakini si kila wakati kufanya hivyo huwa suluhisho.
"Kuna makocha ambao mazingira yanawashinda na ni lazima uamue kuachana nao. Lakini wapo pia wanaostahili kupewa muda wa kujenga timu."
Alitolea mfano benchi la sasa la ufundi la Simba chini ya kocha Steve Barker, akieleza kuwa klabu ina imani kubwa na uwezo wake.
"Steve Barker ameonyesha uthabiti mkubwa. Alikaa Stellenbosch kwa miaka minane, jambo linaloonyesha uwezo wake wa kujenga timu kwa muda mrefu. Nasi tunatarajia kufanya kazi naye kwa kipindi kirefu na kufikia malengo yetu."
Tangu kuanza kwa uwekezaji wa MO mwaka 2017, Simba imejenga heshima yake kimataifa baada ya kuweka rekodi ya kuwa klabu ya Tanzania iliyofuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara tano, na kucheza fainali moja ya Kombe la Shirikisho Afrika.