Kumuona mama yake Yamal Sh1 milioni
Muktasari:
- Sheila ambaye alizaliwa Guinea ya Ikweta kabla ya kuhamia Barcelona akiwa na mama yake, alihudhuria hafla ya Ballon d’Or jijini Paris, Ufaransa wiki iliyopita akiwa na Yamal (18).
LONDON, ENGLAND: KAMPUNI moja ya uandaaji wa matukio ya michezo inawatoza mashabiki wa soka takriban Sh1 milioni ili kuwapa nafasi ya kukutana na Sheila Ebana ambaye ni mama mzazi wa Lamine Yamal katika hafla ya kuelekea Krismasi, mwaka huu.
Sheila ambaye alizaliwa Guinea ya Ikweta kabla ya kuhamia Barcelona akiwa na mama yake, alihudhuria hafla ya Ballon d’Or jijini Paris, Ufaransa wiki iliyopita akiwa na Yamal (18).
Akaunti ya mama huyo ya Instagram ina zaidi ya wafuasi 350,000 na mara kwa mara huchapisha picha zake akiwa kwenye mechi za mtoto wake, Yamal.
Mrembo huyo amekuwa akifuatiliwa na alipata umaarufu tangu Yamal alipoanza kucheza kikosi cha wakubwa cha Barcelona msimu wa 2023/24, na kuwa mmoja kati ya washambuliaji tegemeo.
Kutokana na umaarufu huo kampuni ya Jen C Events imeona sehemu ya kupata pesa kwa kuandaa hafla maalumu ya chakula cha jioni kuelekea Krismasi itakayofanyika mwezi ujao.
Katika hafla hiyo, mama wa Yamal ndiye atakuwa mgeni rasmi na watu ambao watataka kumuona au kupiga naye picha wanaweza kushiriki. “Jiandae kukutana na Sheila Ebana, mama yake Lamine Yamal mmoja wa wanasoka bora duniani katika sherehe kubwa ya Krismasi ya JEN C,” tangazo linasomeka.
Hafla hiyo imepangwa kufanyika Novemba 7 kuanzia saa 1:30 usiku hadi saa 5:30 usiku jijini London na inaruhusiwa kuhudhuriwa na watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea pekee.
Bei za tiketi zinaanzia Pauni 130.72 ambayp mtu atakayenunua atapewa chakula cha aina tatu, shampeni wakati wa kuingia pamoja na vinywaji vichache.
Vilevile kuna tiketi za Pauni 150 maarufu kama ‘iilver’ ambazo mnunuaji atapewa nyongeza ya vinywaji na zile za mwisho za VIP zinazouzwa kwa Pauni 313.82, ambazo zinatoa fursa ya kupiga picha na mama huyo pamoja na kutokuwa na ukomo wa chakula na vinywaji.
Akimzungumzia mama yake mwezi uliopita, Yamal amesema: “Mama yangu hakuweza kuwa nami sana wakati nacheza mpira kwa sababu alikuwa anafanya kazi muda mwingi. Lakini kila aliporudi nyumbani usiku alikuwa akinipikia chakula. Nilipopata pesa nilimnunulia nyumba mahali alipochagua. Yeye ni malkia wangu anastahili kila kitu.”