Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mabao mawili hayatoshi kwa Cherki, Maresca aingilia kati

Muktasari:

  • Cherki aling'ara katika Uwanja wa Selhurst Park baada ya kufunga mabao mawili kipindi cha pili, huku Erling Haaland naye akifunga mabao mawili na kuisaidia City kupata ushindi mnono wa 4-1.

LONDON, England; RAYAN Cherki juzi aliwaacha mashabiki wa soka wakiwa wamechanganyikiwa na wengine wakicheka baada ya kuelezea kiwango chake katika ushindi wa Manchester City dhidi ya Crystal Palace kuwa hakikuwa kizuri licha ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-1.

Cherki aling'ara katika Uwanja wa Selhurst Park baada ya kufunga mabao mawili kipindi cha pili, huku Erling Haaland naye akifunga mabao mawili na kuisaidia City kupata ushindi mnono wa 4-1.

Ushindi huo unamaanisha kuwa kocha Enzo Maresca sasa ameshinda mechi mbili za Ligi Kuu England kati ya mbili tangu kuchukua nafasi ya Pep Guardiola, baada ya timu yake kuvuka nyakati ngumu katika kipindi cha kwanza dhidi ya Crystal Palace.

Cherki alipewa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi, lakini mahojiano yake baada ya mchezo na kituo cha Sky Sports yaliwafanya mashabiki kuzungumza zaidi, huku kituo hicho kikilazimika kuomba radhi baada ya mchezaji huyo kutumia lugha chafu hewani.

Cherki alisema:

“Kiwango changu kilikuwa cha kawaida tu. Kipindi cha kwanza hatukupata nafasi, na nilicheza vibaya sana.

“Nilipoona Enzo anataka kunibadilisha, sikupenda hilo. Nilihitaji kuwaonyesha kwamba nataka kucheza, nataka kufunga, nataka kumpa Erling pasi ya kufunga.

“Kwa sababu leo sikumpa mipira mingi, hivyo wakati mwingine nataka kumpa mipira mingi.”

Bao la kwanza la Cherki lilikuja baada ya kuonyesha umahiri mkubwa na kasi ya miguu, alipofanikiwa kuupitisha mpira mbele ya mabeki kadhaa wa Palace kabla ya kuupenyeza wavuni.

Bao lake la pili lilikuwa shuti kali la mbali ambalo liligusa mchezaji mmoja na kubadili mwelekeo kidogo kabla ya kuingia wavuni.

Na alipoulizwa kuhusu bao lake la kwanza, Cherki alionyesha unyenyekevu badala ya kujisifu, akieleza zaidi hamu yake ya kufanya msimu wa City kuwa wa kukumbukwa.

Alisema:

“Ninafuraha sana kwa ushindi. Tutaonana wiki ijayo. Pep alikuwa sehemu kubwa ya historia, sasa tutaanza historia nyingine. Tunataka kuthibitisha hilo na tuko hapa kwa ajili hiyo.”

MARESCA AMPINGA

Kocha wa Manchester City, Enzo Maresca, hakukubaliana na tathmini ya Cherki kuhusu kiwango chake, ingawa alikiri kuwa huenda mchezaji huyo hakuwa katika kiwango chake cha juu katika kipindi cha kwanza.

“Anayo furaha,” Maresca alisema kuhusu Cherki baada ya mchezo. “Kiwango chake kilikuwa kizuri sana, si kwa sababu tu ya mabao mawili, bali pia namna alivyofanya kazi bila mpira.

“Anapaswa kuwa na presha. Alikuwa anawajibika kumfuatilia Wharton wakati Palace ilikuwa na mpira. Mchezo wake ulikuwa kamili akiwa na mpira na hata bila mpira.

“Anapenda mpira. Hivyo ni rahisi zaidi kufanya kazi naye. Halafu huyo ni Rayan. Tunajua jinsi alivyo mzuri na ubora alionao. Kwa sasa anaisaidia timu kwa pasi za mwisho na mabao, na hakuna shaka kwamba ataendelea kuisaidia timu siku zijazo.

“Huenda hakuwa akicheza katika kiwango chake katika kipindi cha kwanza, lakini kwa ujumla nilifurahishwa na namna alivyofanya kazi bila mpira. Kipindi cha pili alifunga mabao mawili na akawa na furaha zaidi.”

HAALAND AMTANIA

Haaland, ambaye alionekana kutabasamu baada ya Cherki kutumia lugha chafu kwenye televisheni, pia alimsifu kiungo huyo mshambuliaji.

“Tumekuwa na maandalizi mafupi ya msimu. Rayan (Cherki), wiki tano zilizopita alikuwa kwenye Kombe la Dunia. Mechi baada ya mechi tutarudi kwenye kiwango chetu, tunahitaji mechi chache tu.

“Tulicheza vizuri. Ni kocha mpya, lakini tumekuwa tukicheza pamoja, pamoja na kuongezwa kwa wachezaji wachache wapya, kwa muda mrefu.

Tunajua tunachopaswa kufanya na tunahitaji tu kumwamini Enzo. Hii ni hatua sahihi kuelekea upande sahihi kwa kila mmoja.”

REDKNAPP AMWITA“GENIUS”

Mchambuzi wa Sky Sports, Jamie Redknapp, pia alijaza sifa kwa Cherki baada ya mchezo huo, akimtaja Mfaransa huyo kuwa ni “genius” kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza na mpira.

“Baada ya Rayan Cherki kufunga bao la kushangaza, City ilianza kucheza na kupata udhibiti mkubwa wa mchezo,” alisema Redknapp.

“Cherki alionekana kuwa tofauti kwa sababu mabao yake mawili yalikuja katika muda muhimu sana.

“Alikuwa na athari kubwa sana kwenye mchezo na ilikuwa jambo zuri kabisa kumuona akifanya hivyo. Yeye ni genius. Mambo anayoweza kufanya akiwa na mpira ni ya kiwango cha juu kabisa.”

Manchester City, ambayo bado inatarajia kusajili wachezaji zaidi kabla ya dirisha la usajili kufungwa Jumanne, itarejea uwanjani Jumamosi ijayo ambapo itakuwa mwenyeji wa Coventry City.