Baada ya kumkosa Leão, Villa yamvizia kinda wa PSG
Muktasari:
- Villa imefanya haraka kukamilisha dili hilo na mabingwa hao wa Ulaya, huku Leao akiwa karibu kujiunga na Galatasaray ya Uturuki.
LONDON, ENGLAND: KLABU ya Aston Villa iko mbioni kukamilisha usajili wa kinda wa Paris Saint-Germain (PSG), Ibrahim Mbaye, kwa dau linalozidi pauni 47 milioni, baada ya kushindwa kumpata winga wa AC Milan, Rafael Leao.
Villa imefanya haraka kukamilisha dili hilo na mabingwa hao wa Ulaya, huku Leao akiwa karibu kujiunga na Galatasaray ya Uturuki.
Kwa mujibu wa taarifa, Villa ilianza kumfuatilia Mbaye kwa karibu baada ya kuonekana kuwa hana nafasi kubwa kwenye mipango ya PSG, huku klabu hiyo ikiwa tayari kumruhusu kuondoka.
Mbaye, mwenye umri wa miaka 18, alikuwa pia akiwindwa na Liverpool, ambayo ilifanya mazungumzo ya awali kuhusu uwezekano wa kumsajili, lakini ikaamua kutosonga mbele. Bayer Leverkusen pia iliwahi kuwasilisha ofa kwa ajili ya nyota huyo.
Aston Villa imekuwa ikimfuatilia Mbaye kwa muda mrefu, hivyo kukamilisha usajili wake kunatajwa kuwa ushindi mkubwa kwa klabu hiyo kutokana na ushindani uliokuwapo kutoka kwa timu nyingine.
Mbaye alizaliwa nchini Ufaransa, lakini alichagua kuwakilisha Senegal katika ngazi ya kimataifa. Kinda huyo aliwahi kuichezea Senegal kwenye Kombe la Dunia na hata kufunga bao dhidi ya Ufaransa akiwa na jezi ya ‘Lions of Teranga’.
Kwa upande wa klabu, Mbaye ana bao moja na asisti mbili akiwa na PSG, lakini msimu uliopita alianza katika michezo 10 pekee kutokana na ushindani mkubwa wa nafasi ndani ya kikosi hicho.
Ingawa nafasi yake anayopendelea ni upande wa kulia wa safu ya ushambuliaji, Mbaye ana uwezo wa kucheza pia upande wa kushoto, jambo linalomfanya kuwa chaguo lenye uwezo wa kuongeza nguvu na ubunifu kwenye safu ya mbele ya Aston Villa.
Awali, Villa ilikuwa imetuma ujumbe wa viongozi wake mjini Milan kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kumsajili Leao kwa mkopo. Hata hivyo, baada ya nyota huyo kusogea zaidi kuelekea Galatasaray, Villa ilibadili mwelekeo na kuamua kumalizana na Mbaye.
Aston Villa sasa inatarajiwa kumpa Mbaye jukumu kubwa katika mipango yake ya muda mrefu, huku kinda huyo akitarajiwa kuwa miongoni mwa sura mpya zinazong'arisha safu ya ushambuliaji ya klabu hiyo ambayo imeondokewa na mastaa wengi.