Maajabu ya Korea Kusini Kombe la Dunia
Muktasari:
- Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Guadalajara huko Mexico, Korea Kusini ilitanguliwa kufungwa bao na Ladislav Krejcí dakika ya 59 kisha kusawazisha kupitia Hwang In-beom kwenye dakika ya 67 na Oh Hyeon-Gyu dakika ya 80.
TIMU ya taifa ya Korea Kusini imeendeleza maajabu katika michuano ya Kombe la Dunia, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Jamhuri ya Czech kwenye mechi ya kwanza ya kundi A.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Guadalajara huko Mexico, Korea Kusini ilitanguliwa kufungwa bao na Ladislav Krejcí dakika ya 59 kisha kusawazisha kupitia Hwang In-beom kwenye dakika ya 67 na Oh Hyeon-Gyu dakika ya 80.
Ushindi huo wa Korea Kusini dhidi ya Jamhuri ya Czech unakuwa wa kwanza katika mechi ya ufunguzi wa Kombe la Dunia tangu mwaka 2010.
Kabla ya mechi ya leo, mara ya mwisho kwa timu hiyo kushinda mechi ya kwanza ya ufunguzi ya Kombe la Dunia ilikuwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ugiriki katika fainali za michuano hiyo zilizofanyika Afrika ya Kusini mwaka 2010.
Ushindi huo wa Korea Kusini wa 2-1 dhidi ya Jamhuri ya Czech unakuwa ni wa tatu mfululizo kwa kuzifunga timu za Ulaya katika michuano ya Kombe la Dunia, baada ya kuifunga Ujerumani mabao 2-0 mwaka 2018, kisha ikaichapa Ureno 2-1 mwaka 2022.
Mbali na hilo ila katika mara nne kati ya nane ambayo timu hiyo ya Korea Kusini imeshiriki michuano ya Kombe la Dunia imeibuka na ushindi baada ya kuruhusu bao la utangulizi.
Katika fainali za Kombe la Dunia la mwaka 1994 lililofanyika Marekani kama ilivyo sasa, Korea ilitanguliwa kufungwa bao na Hispania kisha kugeuza kibao na kushinda mabao 2-1.
Katika fainali za mwaka 2002, ikiwa mwenyeji kwa kushirikiana na Japan, kwenye hatua ya 16 bora, Korea Kusini ilitanguliwa pia kuruhusu bao dhidi ya Italia, japo hadi mwisho wa mechi hiyo kikosi hicho kiliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Katika fainali za mwaka 2006, huko Ujerumani, Korea Kusini ikaendeleza rekodi yake baada ya kutanguliwa kufungwa bao dhidi ya Togo na mwisho wa mechi hiyo ikashinda tena mabao 2-1.
Mwaka huu wa 2026 katika fainali za Kombe la Dunia linalofanyika nchi tatu za Marekani, Mexico na Canada, Korea imeendeleza ubabe wake wa kutoka nyuma na kushinda, baada ya Jamhuri ya Czech kuongoza 1-0 kisha kuichapa 2-1.
Korea Kusini ilifuzu Michuano hii ya Kombe la Dunia baada ya kufanya vizuri katika hatua za kufuzu Bara la Asia.
Timu hiyo iliongoza kundi C lililokuwa na China, Thailand na Singapore, ambapo kikosi hicho kilikusanya pointi 16, kati ya 18, ambapo ilifuzu rasmi kufuatia kuifunga Iraq mabao 2-0, mjini Basra, yaliyofungwa na Kim Jin-gyu na Oh Hyeon-gyu.