Liverpool kumechangamka, Wirtz akabidhiwa yake
Muktasari:
- Wachezaji wote hao wapya watakuwa kwenye mwonekano mpya kabisa baada a Liverpool kutambulisha uzi wao mpya wa msimu wa 2025/26 na hizo zitakuwa toleo lao la kwanza la jezi katika mkataba wa miaka 10 wa Adidas.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL iko moto, ikitambulisha jezi mpya wa msimu wa 2025-26, zitakazovaliwa na majembe yao ya maana huku kiungo wao ghali, Florian Wirtz akikabidhiwa Namba 7, iliyokuwa ikivaliwa na Luis Diaz, aliyetimkia zake Bayern Munich dirisha hili la majira ya kiangazi.
Mjerumani, Wirtz ni mmoja wa mastaa saba wapya waliojiunga na klabu hiyo ya Anfield dirisha hili la uhamisho wa wachezaji.
Wachezaji wote hao wapya watakuwa kwenye mwonekano mpya kabisa baada a Liverpool kutambulisha uzi wao mpya wa msimu wa 2025/26 na hizo zitakuwa toleo lao la kwanza la jezi katika mkataba wa miaka 10 wa Adidas.
Katika utambulisho huo wa jezi mpya, Liverpool ilitangaza pia namba mpya kwa wachezaji wao ambao zitaonekana mgongoni kwenye jezi zao.
Wirtz, ambaye aliwasili Anfield kwa ada iliyovunja rekodi ya uhamisho Uingereza, Pauni 116 milioni na amekabidhiwa jezi Namba 7, iliyokuwa ikivaliwa na mshambuliaji Luis Diaz.
Staa wa Colombia, Diaz ameachana na Liverpool akimtimkia Bayern Munich. Awali kulikuwa na madai Wirtz alikuwa akitaka kumvua Namba 10 kiungo Alexis Mac Allister, kitu ambacho alikikanusha, licha ya kwamba alikuwa akivaa jezi yenye namba hiyo alipokuwa Bayer Leverkusen.
Wirtz alisema: “Nani anasema nataka Namba 10. Nawaheshimu wachezaji. Msiamini kila kitu kinachoandikwa.”
Wirtz si mchezaji pekee mpya ambaye atakuwa na namba mpya kwenye jezi yake. Mchezaji mwenzake wa zamani wa Leverkusen, Jeremie Frimpong amekabidhiwa jezi Namba 30, kama ambayo alikuwa akivaa alipokuwa Ujerumani.
Wakati huo, straika Mfaransa, Hugo Ekitike atajiandaa kuvaa jezi Namba 22 baada ya uhamisho wake wa Pauni 79 milioni kutoka Eintracht Frankfurt.
Beki wa zamani wa Bournemouth, Milos Kerkez amekabidhiwa jezi Namba 6, ambayo ilikuwa wazi huko Anfield tangu alipoondoka Thiago Alcantara. Kuna mabadiliko pia kwenye eneo la makipa.
Kipa Giorgi Mamardashvili, ambaye alisajiliwa miezi 12 iliyopita, lakini alikuwa kwa mkopo kwenye klabu yake ya zamani wa Valencia, amekabidhiwa jezi Namba 25. Makipa wenzake Freddie Woodman na Armin Pecsi watavaa Namba 28 na Namba 41 mtawalia kwa ajili ya msimu ujao.
Ukiweka kando wachezaji wapya, wachezaji wa zamani waliokuwa kwenye kikosi hicho ambao watakuwa na namba mpya za jezi zao, akiwamo Conor Bradley, ambaye amebadili kutoka Namba 84 na sasa atavaa Namba 12, wakati staa wa kutokea kwenye akademia yao, Trey Nyoni atavaa Namba 42 badala ile ya awali, Namba 98. Liverpool pia bado ipo sokoni kunasa saini ya straika wa Newcastle United, Alexander Isak, ambaye atakuwa na jukumu la kuchagua namba yake ya jezi wakati atakapotua huko Anfield.
Liverpool itaanza kampeni yake ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu England kwa kumenyana na Bournemouth, Agosti 15, lakini kabla ya hapo, itacheza mechi ya pre-season dhidi ya Athletic Bilbao na ile ya Ngao ya Jamii dhidi ya Crystal Palace uwanjani Wembley.