Ligi Kuu England…. Kumeanza kuchangamka!
Muktasari:
- Lakini, kuna pengo la pointi tano baina ya timu inayoshika namba tatu kwenye msimamo na ile iliyopo kwenye nafasi ya nne. Ni mwendo wa kubanana, ukizubaa tu umepigwa gepu la maana.
LONDON, ENGLAND: POINTI sita zimezitofautisha timu namba moja na mbili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England. Na pointi moja zaidi imeitofautisha timu iliyopo kwenye nafasi ya tatu.
Lakini, kuna pengo la pointi tano baina ya timu inayoshika namba tatu kwenye msimamo na ile iliyopo kwenye nafasi ya nne. Ni mwendo wa kubanana, ukizubaa tu umepigwa gepu la maana.
Na tamu zaidi, kuna pointi mbili tu zinazozitenganisha timu iliyopo kwenye nafasi ya nne na ile ya sita. Hii inaitwa zubaa uachwe.
Manchester United iliyopo kwenye nafasi ya nne imepata nafasi ya ama kuzipa presha timu inayoshika namba tatu kwenye msimamo au zile mbili zilizopo chini kwenye namba tano na sita ikiwa ni kwenye mchakamchaka wa kuwania kumaliza ndani ya Top Four.
Na kitu kinachovutia zaidi, Man United itakabiliana na moja ya timu zile zinazoorodheshwa kwenye Big Six, Tottenham Hotspur, kipute kitakachofanyika alasiri ya Jumamosi huko uwanjani Old Trafford.
Man United itaingia uwanjani kusaka ushindi wa nne mfululizo chini ya kocha wa muda, Michael Carrick. Je, itakuwaje? Mambo ni moto.
Ushindi kwa Man United utapunguza pengo la kuifikia Aston Villa kwenye nafasi ya tatu na kubaki pointi mbili, huku chama hilo la Villa Park linalonolewa na Mhispaniola Unai Emery likiwa na kibarua cha kuikabili Bournemouth ugenini baadaye Jumamosi.
Man United itahitaji kushinda nyumbani ili kuzikimbia Chelesea na Liverpool kwenye vita hiyo ya Top Four. Na bahati nzuri kwao ni kwamba Liverpool inakabiliwa na kibarua kigumu cha kuvaana na Manchester City iliyopo kwenye vita ya kusaka ubingwa, ikiifukuzia Arsenal kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo.
Man City itaifuata Liverpool uwanjani Anfield, Jumapili huku tayari ikiwa na majibu ya matokeo ya wapinzani wao kwenye mbili za ubingwa, Arsenal ambayo itarusha kete yake Jumamosi uwanjani Emirates kwa kukabiliana na Sunderland.
Uzuri wa kipute hicho cha Anfield ni kwamba kila timu itakuwa imeshafahamu matokeo ya wale wanaochuana nao kwenye vita binafsi, ambapo Liverpool itakuwa imeshajua Man United na Chelsea zimepata matokeo gani, huku Man City ikifahamu pia matokeo ya Arsenal na Aston Villa. Patamu hapo.
Chelsea itajimwaga kwenye uwanja wa ugenini kukabiliana na Wolves.
Mechi nyingine za Jumamosi, Burnley itakipiga na West Ham United, wakati Fulham itakuwa nyumbani kucheza na Everton huku Newcastle ikimaliza ubishi na Brentford. Kwa Jumapili ukiweka kando mechi itakayopigwa Anfield, kipute kingine kitazikutanisha Brighton na Crystal Palace katika moja ya mechi zinazotazamiwa kuwa na upinzani mkali.
Rekodi zinaonyesha kwamba Man Unitd na Spurs zimekutana mara 67 kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, huku mechi 15 zilimalizika kwa sare.
Man United imeshinda 39, mara 24 nyumbani na 15 ugenini, wakati Spurs imeshinda 13, nane nyumbani na tano ugenini. Kwa takwimu hizo, mzani unaonekana kuegemea upande mmoja. Hata hivyo, mechi tano za mwisho, Spurs imeshinda tatu na sare mbili.
Kuhusu Liverpool na Man City, rekodi zinaonyesha kwamba timu hizo zimekutana mara 57 kwenye Ligi Kuu England, ambapo Liverpool imeshinda 23, mara 18 nyumbani na tano ugenini, wakati Man City imeshinda 13, mbili ugenini na 11 nyumbani, huku mechi 21 zilishuhudia timu hizo zikitoka sare. Mechi tano za mwisho, Man City imeshinda moja, wakati Liverpool mbili na mara mbili zilitoka sare. Mambo ni moto.
Vinara wa ligi, Arsenal wanaweza kuwa katika presha ndogo kwenye mechi dhidi ya Sunderland kutokana na rekodi zinavyosoma, ambapo mara 33 ilizokutana kwenye Ligi Kuu England, sare ni 11, huku The Gunners ikishinda 19, mara 11 nyumbani na nane ugenini, wakati Sunderland imeshinda tatu tu, zote nyumbani. Hakika Ligi Kuu England imefika matamu wakati kila timu ikishuka uwanjani kucheza mechi yake ya 25.