Arsenal Vs Man United… Mechi ya ufundi wa dakika 90
Muktasari:
- Patachimbika. The Gunners haijapoteza mchezo wa ligi katika Uwanja wa Emirates tangu Mei mwaka jana. Unaona jinsi ilivyo mechi ngumu.
LONDON, ENGLAND: MICHAEL Carrick alianza kazi yake kwa changamoto kubwa alipokutana na Manchester City katika mchezo wake wa kwanza.
Kocha wa muda wa Manchester United aliweza kuvuka kikwazo hicho kwa mtindo mzuri.
Lakini, mambo yanakuwa magumu zaidi katika mchezo wake wa pili, safari ya ugenini kukutana na vinara wa Ligi Kuu England, Arsenal.
Patachimbika. The Gunners haijapoteza mchezo wa ligi katika Uwanja wa Emirates tangu Mei mwaka jana. Unaona jinsi ilivyo mechi ngumu.
Kwa hiyo, Carrick ataendelezaje mwanzo wake wa ndoto na kuathiri mbio za ubingwa wa Arsenal? Au je, kikosi cha Mikel Arteta ni imara kupita kiasi?
Katika kipute hicho cha Ligi Kuu England, Arsenal na Man United uwanjani Emirates kitakachopigwa Jumapili, kuna mambo kadhaa ya kiufundi ya kuangazia.
JE, KIUNGO CHA WACHEZAJI WAWILI CHA MAN UNITED KITAWEZA KUKABILIANA NA KIUNGO CHA WACHEZAJI WATATU CHA ARSENAL?
Watu wengi wanauliza kama Man United inaweza kuhimili kiungo cha Arsenal kinachoundwa na Martin Odegaard, Declan Rice na Martin Zubimendi.
Ukimwingiza mshambuliaji kwenye mfumo, Arsenal mara moja wanaonekana kama wanacheza kwa mpangilio wa 3-2-3-2.
Ili kukabiliana na hili, Bruno Fernandes atakuwa na kazi kubwa sana, huenda akahitaji msaada wa mchezaji wa pembeni anayevutwa ndani kusaidia ulinzi.
Inaweza kuonekana kama Michael Carrick atapaki basi (kujilinda kwa wingi), lakini ni lazima ufanye kitu fulani kukabiliana na kiungo hicho cha Arsenal.
Huenda Man United wakaunda kiungo cha boksi (box midfield) kwa kumleta beki wa pembeni au mchezaji wa pembeni kama Patrick Dorgu kuingia katikati ili kuunda faida ya idadi ya wachezaji wanne dhidi ya watatu.
Kinachohisiwa Dorgu atashuka nyuma kutoa msaada wa ziada dhidi ya Bukayo Saka, huku bado akitoa chaguo la pasi ya haraka kwenye mashambulizi ya kushtukiza. Ikiwa Man United itakaa nyuma ya mpira na kuondoka na sare, kwa uhalisia huo utakuwa matokeo mazuri kwao. Mechi ya kifundi sana hii.
KWA NINI MASHAMBULIZI YA ARSENAL YANAONEKANA KUELEMEA UPANDE MMOJA?
Arsenal inaonekana kushambulia zaidi upande mmoja, hasa upande wa kulia alipo Saka.
Nadhani hili linahusu Jurrien Timber anapocheza kama beki wa kushoto, kwa sababu huwa anaingia katikati kama beki anayegeuka (inverted full-back).
Tofauti na Riccardo Calafiori, ambaye alikuwa beki wa kushoto anayepanda sana pembeni, Timber hujiunga na mstari wa mbele katikati, hali inayowaacha bila upana upande wa kushoto. Hii huwafanya wapinzani kujilinda kwa urahisi zaidi kwa sababu kama kuna mchezaji mmoja tu ndani ya boksi, ni rahisi kumzuia.
Ili kutatua hilo, ingependeza Noni Madueke arudishwe kucheza upande wa kushoto ili kutoa chaguo la mguu wa kushoto linaloweza kushambulia kwa pembeni.
William Saliba anaugusa mpira mara nyingi, lakini Arsenal wanahitaji awe na ushawishi katika maeneo hatari zaidi badala ya kumpasia Saka tu.
Dhidi ya Manchester United, lazima iwe upana, upana, upana ili kuvunja ule mfumo wa ulinzi wa wachezaji watano.
Katika mechi tatu zilizopita, mashambulizi ya Arsenal yalikuwa: 24% kushoto, 29% katikati na 47% upande wa kulia.
GYOKERES AU JESUS MBELE NA NINI KIMEWATOKEA KINA EZE?
Bila shaka Viktor Gyokeres ndiye ataanza mbele na atajaribu kumvuta Lisandro Martínez kutoka kwenye nafasi yake ya ulinzi. Gyokeres atafanya mbio nyingi sana juu na chini katika eneo hilo ili kuingia kwenye nafasi hatari.
Hata hivyo, Gabriel Jesus anakupa ule uchezaji wa kuunganisha pasi kwenye ukingo wa boksi, kama tulivyoona wakati Eberechi Eze alipomchezea pasi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kuhusu Eze, ukweli ni Odegaard ndiye chaguo la kwanza na lazima acheze kwa sababu yeye ndiye nahodha.
Eze si winga wa asili wa kushoto na huchukua nafasi zinazofanana na Declan Rice wanaposhambulia. Lakini bado ni chaguo la ajabu kutoka benchini ikiwa watahitaji kubadilisha mbinu katika dakika 20 za mwisho.
Hebu fikiria Eze akishambulia eneo hilo pamoja na Gyokeres na Saka mwishoni mwa mchezo, hilo ni jambo la kutisha sana. Bila shaka mabeki wa Man United watakuwa kwenye wakati mgumu.
Lakini, Man United kama itakwenda Emirates na kucheza kwa kiwango kile ilichokionyesha dhidi ya Man City na Carrick akaweka ufundi wake, bila shaka kocha Arteta atakuwa na wakati mgumu. Ni mechi nzuri ya kutazama. Carrick ana rekodi ya kumfunga Arteta. Je, atafanyaje sasa hivi?
REKODI ZAO ZIKOJE KWENYE LIGI?
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, Arsenal iliyoketi kileleni imeiacha Man United kwa pointi 15. Hivyo, inaingia uwanjani Emirates ikiwa haina hofu yoyote ya tishio la nafasi yake hiyo.
Lakini, inawezekana Arsenal imekuwa bora kwa misimu ya karibuni, kwenye rekodi zake za jumla za mechi ya Man United ubao unasoma tofauti kabisa.
Rekodi za jumla zinasoma, Arsenal na Man United zimekutana mara 67 kwenye Ligi Kuu England na mara 19 ni sare, huku Arsenal ikishinda 22 na Man United 26.
Katika ushindi wa Arsenal, mara 16 ilikuwa nyumbani na sita ugenini, wakati Man United ilishinda nyumbani mara 18 na nane ugenini. Lakini, kwa rekodi za mechi tano za mwisho, Arsenal imeshinda nne na sare moja tu. Je, safari hii itakuwaje? Ngoja tuone.
RATIBA KAMILI YA EPL WIKIENDI
Leo, Jumamosi
West Ham v Sunderland
Burnley v Tottenham
Fulham v Brighton
Man City v Wolves
Bournemouth v Liverpool
Kesho, Jumapili
Brentford v Nottm Forest
Crystal Palace v Chelsea
Newcastle v Aston Villa
Arsenal v Man United
Jumatatu, Januari 26
Everton v Leeds United