Kylian Mbappe ajifunza udereva
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo wa Real Madrid na Ufaransa, 27, ana mkusanyiko wa magari kibao ya kifahari yenye thamani ya Pauni 2 milioni, lakini hajawahi kuendesha mwenyewe hata moja kwa mikono yake.
MADRID, HISPANIA: SUPASTAA Kylian Mbappe ameonekana akipata mafunzo ya kuendesha gari katika shule ya mafunzo ya magari ya jirani huko Hispania.
Mshambuliaji huyo wa Real Madrid na Ufaransa, 27, ana mkusanyiko wa magari kibao ya kifahari yenye thamani ya Pauni 2 milioni, lakini hajawahi kuendesha mwenyewe hata moja kwa mikono yake.
Mashabiki walimwona Mbappé akiingia kwenye gari la mafunzo, ambalo lina gharama sawa na matairi ya BMW i7 yake mpya, katika mji wa Alcorcon kusini mwa Madrid. Kivutio zaidi, mwalimu wake ni shabiki wa Atletico Madrid.
Mwalimu huyo alisema: “Mimi ni shabiki mkubwa wa Atletico, lakini Kylian hakuwa mgumu kabisa kushughulika.”
Wachezaji wengi wa zamani na wa sasa wa Atletico walipata leseni zao katika shule hiyo hiyo. Shule ya Lara Driving School imekuwa ikipokea simu nyingi na maombi ya mashabiki kuleta jezi zao ili Mbappé azisaini pale anaporudi.
Sasa ni vigumu sana kwa Mbappé kuendelea na mafunzo yake bila kuvamiwa na mashabiki. Mashabiki pia wameguswa Mbappé, atakayefikisha miaka 28 mwaka huu, hajawahi kuwa na leseni ya kuendesha gari.
Mmoja aliandika kwenye X: “Nadhani kama hajapata bado kwa nini asipate. Lakini, wengi wanapata baada ya kufikisha miaka 18, sivyo?”
Mbappé ana mkusanyiko mkubwa wa magari ya kifahari ikiwamo Ferrari SF90, lakini hawezi kuendesha kwa sababu hana leseni.
Mwingine alisema: “Ni vichekesho kufikiria mtu ambaye anaweza kumzidi beki mtaalamu kwa km 35/h sasa hivi anaanza kujifunza kuendesha gari.”
Mbappé amekuwa akipewa huduma ya dereva kutokana na kushindwa kupata leseni katika kipindi cha msukumo wa maisha yake alipopanda kufahamika kimataifa. Alizungumzia ukosefu wake wa leseni mwaka 2023 na kusema kuwa hakukuwa kipaumbele kwake, aliposema: “Ni moja ya hasara za kufanikisha mapema, nilikosa mambo rahisi kama kuwa na leseni ya kuendesha. Nadhani kila mtu ana moja. Kwa watu wengi leseni ni wajibu, lakini siyo kwangu. Ingawa ni ishara ya uhuru, nilikuwa na uhuru mapema kwa sababu nilikuwa na madereva tayari. Haikuwahi kuwa kipaumbele.”
Mbappé amekuwa na msimu mwingine mzuri katika La Liga, akifunga mabao 23 katika mechi zote aliocheza msimu huu. Yeye yuko kwenye njia ya kushinda Tuzo yake ya pili ya Pichichi akiwa na Real Madrid.