Kwa Casado ni ofa tu zinasubiriwa Barca
Muktasari:
- Mchezaji huyo kutoka akademi ya klabu hiyo hajapata muda mwingi wa kucheza chini ya kocha Hansi Flick na yupo tayari kuondoka kutafuta nafasi zaidi nje ya klabuhiyo, kwa mujibu wa gazeti la Sport.
BARCELONA, HISPANIA: WAKATI msimu unakaribia kumalizika na tetesi za uhamisho zimeanza kusikikaa, Marc Casado ni mmoja wa wachezaji ambao hawana nafasi ya uhakika katika msimu ujao kwenye kikosi cha Barcelona.
Mchezaji huyo kutoka akademi ya klabu hiyo hajapata muda mwingi wa kucheza chini ya kocha Hansi Flick na yupo tayari kuondoka kutafuta nafasi zaidi nje ya klabuhiyo, kwa mujibu wa gazeti la Sport.
Siyo mara ya kwanza kusikika kwa tetesi za kuondoka kwa Casado, kwani amewekwa pembeni katika safu ya kiungo hasa baada ya kurejea kwa kiwango kizuri kinachoonyeshwa na Marc Bernal. Jeraha lake kubwa msimu uliopita liliathiri mipango ya Flick ambaye alilazimika kumtumia Casado kama chaguo la dharura.
Na kutokana na kupata nafasi wakati huo mchezaji huyo aliendelea kuimarika, lakini msimu huu anapata ugumu zaidi kuingia katika mipango ya kocha. Casado hakutaka kuondoka, lakini huenda amebadilisha mawazo anataka kusepa sasa.
“Nina uhakika kwamba kwa muda wote nitakapoweza kuvaa jezi hii na kuitetea nembo hii, hilo litakuwa kipaumbele changu. Ni ndoto niliyokuwa nayo tangu utotoni na natumaini nitaifurahia zaidi. Najiamini na najua ninachoweza kuipa timu hii," alisema Januari, mwaka huu baada ya kuchukua nafasi ya Pedri katika mechi dhidi ya Real Oviedo kwenye Ligi Kuu Hispania.
"Nitatumia kila dakika nayopewa. Ni muhimu kuisaidia timu wakati nafasi inapojitokeza. Kila dakika nayoweza kuingia uwanjani nikiwa na jezi hii nitaipigania hadi mwisho.”
Takwimu zinaonyesha Casado amecheza mechi 29 kwa dakika 1,276 na yupo nafasi ya 17 katika orodha ya wachezaji wa kikosi hicho. Amecheza zaidi tu kuliko Ronald Araujo (aliyekuwa nje kutokana na msongo wa mawazo), Bernal (aliyerejea kutoka jeraha la muda mrefu), Andreas Christensen (anayekumbwa na majeraha ya mara kwa mara), Joao Cancelo (aliyewasili Januari), Roony Bardghji (ambaye pia hapewi nafasi mara nyingi na anatarajiwa kuondoka) na Gavi mwenye jeraha la muda mrefu).
Casado ameanza katika kikosi cha kwanza mara 12 bila kumshawishi kocha Flick kikamilifu. Hata hivyo, kwa mujibu wa Sport, mchezaji huyo amebadilisha mawazo katika miezi ya hivi karibuni kwani hali yake haijaimarika.
“Kuna mabadiliko makubwa katika hali yake ambayo kwa hatua hii ya msimu yanaonekana kuwa magumu sana ndiyo yanaweza kubadilisha uamuzi ambao tayari umefikiwa. Ikiwa hali itabaki hivi, na ofa nzuri itawasili kwa pande zote, basi kuondoka kwake kunaweza kukamilika majira ya joto,” kinasema chanzo cha gazeti hilo kutoka Barcelona.