Vinicius Jr, afanyiwa upasuaji kurekebisha kidevu
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Brazil TMC, Vinicius alielekea moja kwa moja kwa daktari bingwa wa ngozi mjini Goiania mara tu aliporejea nchini humo baada ya mapumziko mafupi akiwa na mpenzi wake ambaye wamekuwa wakiachana na kurudiana, Virginia Fonseca.
BRASILIA, BRAZIL: Nyota wa Real Madrid na Brazil, Vinicius Jr amefanyiwa upasuaji wa kurekebisha umbo la kidevu ikiwa ni wiki chache baada ya Brazil kuondolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Kwa mujibu wa Brazil TMC, Vinicius alielekea moja kwa moja kwa daktari bingwa wa ngozi mjini Goiania mara tu aliporejea nchini humo baada ya mapumziko mafupi akiwa na mpenzi wake ambaye wamekuwa wakiachana na kurudiana, Virginia Fonseca.
Picha kadhaa za mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 akiwa amebadilika baada ya kufanyiwa upasuaji huo zimesambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, huku mashabiki wengi wakishangazwa na mabadiliko ya mwonekano wake.
Virginia alichapisha picha yao wakiwa katika ukumbi wake mpya wa mazoezi jana Jumatatu, jambo lililoonyesha kuwa wawili hao wamefufua uhusiano wao baada ya kuachana kabla ya Kombe la Dunia.
Wakati huohuo, mmoja wa marafiki wa Vinicius alichapisha video ikimuonyesha akiwa na mwonekano mpya alipokuwa akisaini jezi ya Real Madrid kwa ajili ya shabiki.
Katika picha nyingine iliyosambaa mtandaoni, Vinicius alionekana akiwa amesimama pamoja na Dk. Alessandro Alarcao, daktari aliyefanya upasuaji huo mjini Goiania.
Upasuaji huo hutumia vichocheo maalumu (fillers) kuchonga na kuboresha umbo la uso ili kufanya kidevu kionekane tofauti.
Vinicius aliamua kufanya hivyo baada ya kudhihakiwa sana kuhusu kidevu chake wakati wa Kombe la Dunia.
Inaonekana nyota huyo wa Real Madrid ameridhishwa na mwonekano wake mpya, kwani katika picha zote zilizopigwa baada ya upasuaji anaonekana akitabasamu.
Mashabiki walijawa na mshangao kwenye mitandao ya kijamii kutokana na mabadiliko hayo ambapo mmoja aliandika:"Ubongo wangu unashindwa kuamini kwamba huyu ndiye Vini Jr wa sasa."
Mwingine ametania:"Sitaamini mpaka nimuone akiingia uwanjani kucheza akiwa hivi."
Shabiki mwingine aliandika kwa mshangao:"Jamani, huyu ni nani tena?"
Mwingine amesema:"Mungu wangu! Simtambui kabisa."
Naye mwingine alitania: "Vinicius Jr ndiye mtu wa kwanza katika historia kufanana na toleo lake lililotengenezwa na akili bandia (AI)."
Brazil na Vinicius walikuwa na kampeni ngumu katika Kombe la Dunia kabla ya kuondolewa na Norway katika hatua ya 16 bora kwa kufungwa mabao 2-1.
Baada ya kumaliza vinara wa Kundi C, licha ya kuanza mashindano kwa sare dhidi ya Morocco, Brazil ilihitaji bao la dakika ya 96 kuiondoa Japan katika hatua iliyofuata.
Hata hivyo, katika mchezo dhidi ya Norway uliochezwa New Jersey, kikosi hicho cha kocha Carlo Ancelotti kilizidiwa ubora, Erling Haaland akifunga mabao mawili mwishoni mwa mchezo na kuipa Norway ushindi, huku Neymar akifunga bao la kufutia machozi kwa mkwaju wa penalti katika dakika za mwisho.
Licha ya kuondolewa mapema, Vinicius alikuwa na mashindano mazuri binafsi, akifunga mabao manne.
Baada ya kumaliza mapumziko yake ya baada ya Kombe la Dunia, Vinicius anatarajiwa kurejea Madrid kuanza maandalizi ya msimu wa 2026/27 akiwa na Real Madrid.