Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ghafla nimemkumbuka Mino Raiola, kiboko ya hofu zetu

PAZIA Pict


KUNA watu walikuwepo na wameondoka. Na unajua kabisa wameondoka. Ni katika kauli ile ile maarufu ya Wazungu. Walisema ‘tough time never last, but tough people do.' Wakimaanisha nyakati ngumu huwa hazipiti, lakini watu wagumu wanapita.


Nimemkumbuka rafiki yetu Cermino ‘Mino’ Raiola. Tangu jioni ile ya April 30, 2022 umauti ulipomkumbuka juu ya kitanda katika Hospitali ya San Raffaele pale Milan, kuna watu wamepumua kwelikweli. Hawawezi kuendelea kusema hadharani kwa sababu marehemu hakumbukwi sana kwa mabaya.


Mino, kibonge kama alivyo alikuwa wakala mtata. Juzi nimemkumbuka sana baada ya kuona tu dili mbalimbali za usajili kule kwa Wazungu zikiendelea bila malalamiko kutoka kwa makocha wala mashabiki. Labda ni dili la Alexander Isak tu kidogo ndilo ambalo lina utata wa hapa na pale.

Dunia ya soka kule kwa Wazungu imekuwa salama baada ya umauti kumkuta Raiola pale San Raffaele kisha akazikwa pale Monte Carlo. Dunia imekuwa salama kwa baadhi ya mashabiki, makocha na mabosi wa timu mbalimbali.

PAZ 01

Mino alijua kuwavuruga. Nashangaa sasa hivi anayetamba katika masuala ya uhamisho wa wachezaji ni mtu anayeitwa Fabrizio Romano ambaye ni mwandishi wa habari. Zamani, kabla umauti haujamkumba, Mino Raiola angekiweka kipindi kama hiki katika mikono yake. Kiurahisi tu.

Katika orodha ya wateja wake lazima angelazimisha wachezaji kadhaa wanahama au wanasaini mikataba mipya kwa lazima ili apate kamisheni yake. Mashabiki wengi wa soka walishangilia kifo chake hasa wale ambao alizidhuru klabu zao.

Mfano Manchester United aliwadhuru mara mbili kupitia kwa Paul Pogba. Aliwahi kulazimisha kumuondoa bure akampeleka Juventus wakati ule Pogba akiwa kinda. Na baadaye akamrudisha katika utawala wa Jose Mourinho kisha baada ya muda akalazimisha kumuondoa tena kumpeleka Juve.

Katika uhamisho wa kwanza wa Pogba akiwa kinda kwenda Juventus Sir Alex Ferguson alimchukia Raiola kuliko kitu kingine chochote. Akamuita ‘tapeli - takataka’. Raiola hakujali sana. Wala hakujali kwamba Sir Alex alikuwa anamuandaa Pogba kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Paul Scholes ambaye umri ulikuwa unamkamata.

PAZ 02

Dunia ya soka inapumua kwa sasa. Najaribu kufikiria kwamba baada ya wateja wake wengi kwa sasa kuishiwa pawa sijui Raiola angeibuka na wateja gani wapya ili asumbue tena. Kina Romelu Lukaku, Zlatan Ibrahimovic, Moise Kean, Marco Verratti na wengineo wameishiwa pawa.

Wateja wake wawili ambao angetamba nao kwa sasa ni Erling Halaand na Gianluigi Donnarumma. Manchester City wanaishi kwa raha sana na Haaland kwa sasa, lakini kama Raiola angekuwepo si ajabu angelazimisha kumtia sokoni hata katika Ligi Kuu  Saudi Arabia ilimradi apate kamisheni yake.

Angeweza kupiga simu mbili tatu kwa magazeti maarufu ya Hispania, Marca na AS kwa ajili ya kutengeneza mahitaji ya Haaland ionekane kama vile anatakiwa na Real Madrid ili kutengeneza idadi ya Galacticoz katika viunga vya Santiago Bernabeu. Lazima mashabiki wa Manchester City wangekaa tumbo joto.

PAZ 03

Vinginevyo kama uwezekano wa kutoondoka kabisa usingekuwepo, basi Raiola angelazimisha Haaland awe mchezaji anayelipwa zaidi Manchester City na Ulaya. Ni tofauti na mkataba ambao aliuingia na City baada ya Raiola kufariki dunia. Namfahamu Raiola. Lazima angeanzisha zogo lisilo na msingi mpaka City wangemchukia. Asingependa amani.

Wachezaji wanawapenda mawakala kama Raiola. Wachezaji wanajali pesa na Raiola licha ya kupata chake, lakini alikuwa anahakikisha wachezaji wanapata dili nzuri kuliko walizozitegema. Matokeo yake sio yeye tu, hata wachezaji wengine wanawapenda mawakala wao kuliko timu kwa sababu hii.

Kitu kingine ambacho kimepotea baada ya Raiola kutoweka ni kwamba lazima angeibuka na bidhaa nyingine adimu zilizo sokoni kwa sasa. Angeweza kuibuka hata na Lamine Yamal na kuleta usumbufu usio na maana pale Barcelona. Angeweza kuibuka na Gavi au Pedri na akaleta kasheshe kubwa isiyokuwa na kichwa wala miguu.

PAZ 04

Kule Real Madrid angeweza kumuweka mikononi Vinicius Junior au Hendrick na kuleta kasheshe kubwa isiyokuwa na kichwa wala miguu.

Pale Arsenal kuna makinda wanaitwa Myles Lewis-Skelly, Ethan Nwaneri na Max Dowman. Hapa usingeshangaa kuona Raiola anaibuka na mmoja na kumuweka kwapani kisha anaanza kuwasumbua Arsenal. Ni kama vile mtoto hawakumlea wao.

Kitu hikihiki aliwafanyia AC Milan. Donnarumma aliibuka katika timu yao ya vijana wakamkuza akawa mahiri kwelikweli. Raiola alichofanya ni kuhakikisha Donnarumma hasaini mkataba mpya na AC Milan kama vile alivyofanya kwa Pogba na United. Mwishowe akaenda zake PSG na kuwaacha AC Milan wakiwa wamefura kwa hasira.

PAZ 05

Hiyo ndio kazi ya Raiola. Kila dirisha kubwa la majira ya joto lilipokaribia jina la Raiola lilikuwa maarufu kama ilivyo kwa Romano. Tofauti ni kwamba Romano ni mwandishi anayetoa habari wakati Raiola ni wakala aliyekuwa anaanzisha vurugu.

Aendelee kupumzika kwa amani. Alijua kutingisha waajiri wa wateja wake. Vilevile alikuwa mmoja kati ya mawakala ambao walisababisha watu wengine wapende kazi hii. Fikiria ulipokuwa unasikia kwamba katika dili moja la mchezaji wake kuhama angeweza kupata hata kitita cha Pauni 15 milioni peke yake na kukiweka mfukoni.

Na ungetamani zaidi kuwa wakala pale ambapo ungemuona akiendesha magari ya kifahari pamoja na kula raha na wateja wake kina Pogba katika kumbi mbalimbali za starehe kule Las Vegas, Marekani. Huyo ndiye Mino Raiola. Super agent ambaye tulimpoteza miaka mitatu iliyopita pale Hospitali ya San Raffaele iliyopo Milan. Nimemkumbuka sana.