Kuhusu Isak... Mambo saba yatajwa
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden alisisitiza anataka kujiunga na Liverpool kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili na majogoo hao wamepanga kuja na ofa mpya ya Pauni 130 milioni wiki ijayo.
NEWCASTLE, ENGLAND: SAKATA la staa Alexander Isak na timu yake ya Newcastle United limezidi kushika sura mpya tangu atoke hadharani na kutoa kauli kali kuhusu mustakabali wake wa uhamisho.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden alisisitiza anataka kujiunga na Liverpool kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili na majogoo hao wamepanga kuja na ofa mpya ya Pauni 130 milioni wiki ijayo.
Isak aliushambulia uongozi wa Newcastle akidai “uaminifu umepotea” na akataka ruhusa ya kuhamia Anfield.
Hata hivyo, Newcastle ilijibu na ikisisitiza hatouzwa isipokuwa itakuwa “kwa masilahi ya klabu” na kuweka wazi ikiwa anataka kurejea kikosini milango ipo wazi.
Baada ya vita ya maneno mitandaoni, Jumatano staa huyu alionekana akiingia na gari yake katika kiwanja cha mazoezi cha Newcastle na nje alikutana na mashabiki waliokuwa wakimtusi na kumwambia maneno mabaya ikiwa ni sehemu ya kuonyesha hasira zao baada ya staa huyo kulazimisha kuondoka.
Hata hivyo, wakati sakata hilo linaendelea, tovuti ya The Sun imefichua mambo saba ambayo yanaweza kufanyika ili kuondoa sintofahamu iliyopo sasa.
Jambo la kwanza ni Newcastle kukubali kumuuza kwani Liverpool inataka kulipa Pauni 130 milioni kiasi kinachoonekana kikubwa ikilinganishwa na pesa ambazo wao walitoa ili kumnunua kutoka Real Sociedad, Euro 70 milioni mwaka 2022.
Suala la pili ni Isak kuendelea kugoma kwani inaweza kuishawishi Newcastle kumwachia lakini ikishindikana inaweza kuwa hasara kwake kwani anaweza kutupwa nje ya kikosi.
Jambo la tatu ni Newcastle kukaa naye chini na kumpa mkataba mpya mnono ambao utamfanya kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi.
Suala hilo linaweza kumshawishi akabakia kwani mara kadhaa kuna wachezaji ambao hutaka kuondoka lakini timu huwa zinawasainisha mkataba mpya na kuendelea kubakia nao.
Mfano iwahi kutokea mwaka 2014, Wayne Rooney alipotaka kuhamia Chelsea lakini akaishia kusaini mkataba mpya na Manchester United.
Suluhisho la nne ni Isak kubaki kwa mwaka mmoja, kisha kuuzwa dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa dau kubwa lakini kwa timu ambayo sio ya Ligi Kuu England.
Mfano kama huu ulitokea kwa Luka Modric, ambaye alitaka kujiunga na Chelsea mwaka 2011 lakini Tottenham ilimuuza kwenda Real Madrid mwaka uliofuata.
Vivyo hivyo, Cristiano Ronaldo alizuiliwa kuondoka Man United mwaka 2008, kabla ya kuuzwa Madrid mwaka 2009 kwa dau la rekodi.
Njia nyingine inaweza kuwa ni hii ya kumtoa kwa mkopo wa muda mfupi na kurudi. Hii iliwahi kufanyika kwa Victor Osimhen ambaye msimu uliopita alikuwa katika sintofahamu na Napoli na hakuwa anataka kurejea tena hapo, Chelsea ilikuwa ikimhitaji lakini dili likafeli katika dakika za mwisho, katika kuhakikisha anapata sehemu ya kucheza alikubali kwenda kwa mkopo Galatasaray ambayo msimu huu amejiunga nayo mazima.
Vilevile anaweza kutolewa kwa mkopo wa muda mfupi kama ilivyokuwa kwa Diego Costa ambaye alikosana na Kocha Antonio Conte baada ya Chelsea kushinda taji mwaka 2017.
Costa alikimbilia Brazil kabla ya kurejea Ulaya Januari 2018 na kutua Atletico Madrid.
Mwisho ikiwa ni kuhusu pesa, klabu za Mashariki ya Kati hususani Saudi Arabia zinaweza kutatua suala hili kwani zinaweza kutoa kiasi cha pesa kinachohitajika na Newcastle na kumnunua ingawa haionekani ikiwa staa huyo atakubali kwenda Saudia kwa kwa sasa.
Vilevile, wamiliki wa Newcastle ndio wamiliki wa timu nyingi za Saudia, hivyo hata akiuzwa pesa zitakazopatikana hazitoweza kutambulika kama faida katika masuala ya kanuni za matimizi ya kifedha.